Kila kitu dunia ambacho unakiona kina mafanikio makubwa, kina msingi wake ambao umefanya hadi unaona hayo mafanikio, unayoyaona sasa. Hakuna kitu ambacho kimewahi kuleta mafanikio makubwa duniani kikawa na msingi mbovu.
Kwa tafsiri hiyo ili uwee kufanikiwa kwa viwango vya juu, ni lazima ujue namna ya kujenga msingi wako imara utakao beba mafanikio hayo makubwa. Huwezi kusema unataka mafanikio makubwa, wakati una msingi wa mafanikio madogo madogo tu.
Hiyo utakuwa ni sawa na mtu anayetaka kujenga ghorofa wakati msingi alio uweka ni wa nyumba ya kawaida. Nafikiri hapo moja kwa moja kitakuwa ni kitu ambacho hakitawezekana, ghorofa hilo ni lazima litandoka.
Hata katika maisha ya mafanikio, ni vyema na lazima kujenga msingi imara utakaosaidia kukupa mafanikio makubwa. Je, unafahamu msingi imara wa mafanikio makubwa unajengwa kwenye mambo gani?
Kama kwako hilo linakupa shida usipate tabu, fuatana nasi katika makala haya kujifunza jinsi unavyoweza kujenga msingi imara wa mafanikio yako kwa kuzingatia mambo kadhaa tutakayokwenda kuangalia hapa.
1. Thamani.
Kila kitu unachokifanya, lazima kitoe thamani fulani ndio kikupe mafanikio. Bila kitu hicho kutoa thamani hakiwezi kukupa mafaniko hata ulie machozi ya namna gani. Utahangaika sana kutafuta mafanikio na hutayapata kama hutoi thamani kubwa .
Haijalishi umeajiriwa au umejiajiri, lazima utoe thamani. Huu ni msingi mkubwa sana wa mafanikio kwa sababu, hakuna mafanikio yoyote dunia utakayoweza kuyapata bila ya kutoa thamani. Kwa jinsi unavyozidi kutoa thamani kubwa ndivyo mafanikio yako yanakuwa makubwa zaidi.
![]() |
Weka imani sahihi kwa kile unachokifanya. |
2. Imani.
Pia mbali na thamani kama msingi mkubwa wa mafanikio, pia msingi mwingine wa mafanikio upo kwenye imani yako. Je, unakiamini kitu hicho unachokifanya? Unapata picha gani kwa jinsi unavyokifanya kitu hicho. Je, una picha ya mafanikio au picha ya kushindwa kichwani mwako?
Siku zote ni ngumu sana kuweza kufanikiwa kama imani yako haiko sawa, yaani hauamini kama utaweza kufanikiwa. Watu wote wanaofanikiw a wananamini sana vile wanavyovifanya na pia wanajiamini wao wenyewe kwamba wanaweza. Hivi ndivyo unavyotakiwa kufanya kujenga imani imara itakayokupa mafanikio.
3. Tabia.
Pia mafanikio yanajengwa katika msingi mwingine wa tabia. Kama unatabia mbovu kama vile ukosefu wa nidhamu binafsi, matumizi mabaya ya pesa, matumizi mabaya ya muda na tabia zinginezo, basi ujue kabisa unajirudisha nyuma kimafanikio na itakufanya ushindwe kufanikiwa.
Hivyo kwa kadri unavyojenga tabia zako na kuwa bora, hapo ndipo unajitengenezea msingi mwingine imara wa kuweza kusimamisha maisha yako na kuwa maisha bora kabisa. Kila wakati fanya ufanyalo na kuweza kujenga msingi wako imara wa tabia ili ufike unakotaka kufika.
4. Maarifa.
Mafanikio yanajengwa pia kutokana na maarifa tunayoyapata kila siku. Ndio maana unaona tunajifunza kila siku hapa kupitia AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA, lengo kubwa ni kujenga msingi mwingine wa maarifa ili kujihakikishia mafanikio ya kudumu.
Kama upo kwenye safari halali ya mafanikio na una nia hii kweli, huwezi kukwepa hata siku moja kujijengea misingi hiyo minne imara ya mafanikio ili kufikia mafanikio makubwa. Kushindwa kuwa na msingi hiyo ni sawa na kukataa mafanikio yako mwenyewe.
Chukua hatua na kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa.
Kwa kujifunza zaidi kuhusu maisha na mafanikio pia tembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
IMANI NGWANGWALU,
0713 04 8035,