Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

USHAURI; Hatua Za Kuchukua Pale Marafiki Au Watu Wa Karibu Wanakukatisha Tamaa Kwenye Wazo Lako La Biashara.

$
0
0
Habari za leo rafiki?

Karibu tena kwenye mtandao wetu wa AMKA MTANZANIA na karibu sana kwenye kipengele hichi cha ushauri wa changamoto. Kama ambavyo nimekuwa nakuambia siku zote, changamoto zipo hapa na sisi, haziendi popote, tukitatua changamoto moja inakuja nyingine.


Hivyo usijidanganye kwamba ipo siku changamoto zote zitakwisha kabisa, siku hiyo ni pale utakapokufa.

Wapo watu wengi ambao wamekuwa wanapanga kuingia kwenye biashara, lakini kikwazo kikubwa kimekuwa wale watu wanaowazunguka. Wanakuja na mawazo ya biashara lakini watu hao wanawakatisha tamaa kwamba hayafai. Watu hawa ni wale wa karibu sana na hivyo kuwa na ushawishi mkubwa mno. Watu hawa ni marafiki, ndugu, na hata wenza kwenye ndoa.

Wengi wamekuwa wakipokea maoni ya watu hawa wa karibu kama ndiyo ukweli na kushindwa kabisa kuchukua hatua. Kitu ambacho kimewapelekea kubaki pale ambapo wapo. Lakini hii haipaswi kuwa hivi, maoni ya watu wa karibu hayapaswi kuwa mwisho wa ndoto yako, bali yanapaswa kuwa kichocheo. Karibu kwenye makala ya leo ya ushauri tujifunze mambo ya kufanya pale watu wako wa karibu wanapokukatisha tamaa kwenye wazo lako la biashara.

Kabla hatujaangalia nini cha kufanya, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hilo;

Changamoto yangu nataka kununua pikipiki ya biashara ila rafiki yangu ananikatisha tamaa. Sijui nifanye nini. Athumani B. S.

Hivi ndivyo ambavyo imekuwa inatokea kwa wengi, unakuja na wazo lako la biashara ambayo unataka kufanya, lakini watu wako wa karibu wanalipokea kwa kukuonesha kwa nini wazo hilo halifai au halitakufaidisha. Ni rahisi sana kuwasikiliza watu hawa na kutokuchukua hatua, lakini hiyo siyo njia sahihi.

Zifuatazo ni hatua unazopaswa kuchukua pale watu wako wa karibu wanapokukatisha tamaa kuhusu wazo lako la biashara.

Hatua ya kwanza; angalia wasifu wao.

Anza kwa kuangalia wana sifa gani ya kuweza kukuambia yale ambayo wanakuambia juu ya biashara unayopanga kufanya. Je wao wameshafanya biashara kama hiyo? Je wamekuwa karibu na mtu aliyefanya biashara kama hiyo? Au wamekuwa wanaona tu kwa mbali na kusikia? Na swali muhimu kabisa, je wao wameshakuwa kwenye biashara yoyote?

Haya ni maswali muhimu kuanza nayo ili kujua msingi wa wale wanaokukatisha tamaa upo wapi. 

Wengine wanakukatisha tamaa kutokana na uzoefu ambao wao wenyewe wanao, ila wengi wanakukatisha tamaa kutokana na hofu ambazo wao wanazo.

SOMA;   Hii Ndio Siri Ya Kupata Marafiki Bora Watakaokuwezesha Kufikia Malengo Yako.

Wanaokukatisha tamaa kwa uzoefu ni wale ambao wameshafanya biashara husika, au walishafanya biashara nyingine yoyote. Hawa wanaweza kuwa wameshajifunza mengi kuhusu biashara unayotaka kufanya, na hivyo wanaona namna unavyokwenda kuumia.

Wanaokukatisha tamaa kwa hofu ni wale ambao hawajawahi kufanya biashara kabisa, ila wanajua biashara unayokwenda kufanya ni mbaya. Hawa wamejawa na hofu, na hofu hizo ndiyo zimewafanya wao wenyewe washindwe kuanza biashara hivyo hawawezi kuvumilia kukuona wewe ukiwa unaanza biashara. Wakati mwingine wana taarifa nyingi za kusikia, ambazo hawana uhakika nazo.

Je uchukue hatua gani ukishajua wasifu wa yule anayekukatisha tamaa?

Kama anakukatisha tamaa kwa uzoefu, fanya utafiti wako zaidi na kuona namna gani unaweza kufanya kwa ubora. Unaweza pia kumuuliza yeye binafsi akushirikishe uzoefu alionao kwenye biashara hiyo husika. Hapa utajifunza na kujua hatua gani sahihi kwako kuchukua.

Kama anakukatisha tamaa kwa hofu, achana naye, tafuta mwenye uzoefu na ongea naye. Ni bora ujaribu ushindwe kuliko kumsikiliza mtu anayekukatisha tamaa wakati yeye mwenyewe hajawahi kufanya kitu kama kile unachokwenda kufanya wewe.

Hatua ya pili; waambie wakupe wazo mbadala.

Mtu yeyote anayekukatisha tamaa, anayekuambia hiyo biashara unayokwenda kufanya haikufai au utapata hasara, usimwitikie tu na kusema ndiyo, hata kama ni mzazi wako. Badala yake mpe jukumu gumu ambalo litamfanya afikiri na wewe ufikiri zaidi, na hapo mtapata kitu bora zaidi.

Akishakueleza kwa nini biashara hiyo haifai, mwambie asante sana kwa maoni haya mazuri uliyonipa, sasa naomba unisaidie maswali mawili tu ili niweze kupiga hatua;

SOMA; Faida Ya Kuwa Na Marafiki Wenye Mitizamo Chanya.

Swali la kwanza kwa nini unasema biashara hii niliyochagua haifai au nitashindwa? Hapo akupe sababu zake za msingi za kusema hivyo.

Swali la pili ni biashara gani ambayo naweza kufanya kama hii haiwezekani? Hapa akupe kwa kina bishara anayofikiri unaweza kufanya na ikawa bora kwako.

Maswali haya ni muhimu sana kumwuliza kila anayekukatisha tamaa kwenye wazo lako la biashara. Na ikiwa mtu atashindwa kuyajibu kwa kujiamini, basi achana naye mara moja, hajui kile anachokisema na mbaya zaidi hana msaada wa hatua gani uchukue.

Mtu ambaye anajua vitu gani huwezi kufanya, ila hajui vitu gani unaweza kufanya, ni mtu hatari mno, usimtegemee kuwa mshauri mzuri. Mshauri mzuri ni yule ambaye anajua kipi bora kufanya, akikuambia hiki hakifai, anaweza kukuambia kipi kinafaa na mkaanza kujadili hapo.

Hatua ya tatu; angalia kipi cha kufanyia kazi kwenye ushauri wa mtu anayekukatisha tamaa.

Hata kama yule anayekukatisha tamaa hajafikia zile sifa za wewe kumsikiliza, yaani kuwa na uzoefu au kuweza kutoa wazo mbadala, bado kuna kitu unaweza kujifunza kupitia ushauri wake wa kukukatisha tamaa. Angalia ni nini kimemsukuma kuhusu ushauri wake huo. Wakati mwingine watu hawa wanakupenda sana na hawataki kukuona ukiumia kama ambavyo wameona wengine wakiumia. Au wakati mwingine watu hao hawataki kukuona wewe unapiga hatua kubwa. Yote hayo yanawezekana hivyo hakikisha unachimba kwa undani ili kuujua ukweli.

Angalia pia ni vitu gani unaweza kuboresha zaidi kutokana na maoni ya watu kwenye lile wazo lako. Kama utaamua kulifanyia kazi basi angalia unaliboreshaje ili kuepuka kuumia kama ambavyo watu wanakushauri. Na kama utaamua kuachana nalo basi kuwa na mbadala wa nini unafanya, ili usiache kabisa kuingia kwenye biashara.

Mwisho kabisa nikuambie hivi rafiki yangu, kwa vyovyote vile chukua hatua, iwe ni kwa kuboresha wazo ulilonalo ili kuepuka yale unayoshauriwa ni mabaya, au kwa kuangalia wazo jingine mbadala la kufanya. Usiache kabisa kuchukua hatua kwa sababu ya ushauri wa wengine kwenye biashara unazopanga kufanya. Ni bora uchukue hatua na ushindwe, utakuwa umejifunza zaidi kwa vitendo na hivyo kuwa na uzoefu mkubwa zaidi. Kuendelea kubaki hapo ulipo sasa, hakuna msaada wowote kwako. Lazima uwe na hatua yoyote ile ya kuchukua, ili kutoka hapo ulipo sasa.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>