Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; NOBLE PURPOSE (Furaha Ya Kuishi Maisha Yenye Maana.)

$
0
0
Hakuna kitu ambacho kimewasumbua wengi kama njia sahihi ya kuwa na furaha kwenye maisha. Watu wamejaribu njia nyingi sana ambazo kwa nje zinaonekana kuleta furaha, lakini mwisho wanajikuta wanarudi pale pale, wanakuwa na raha ya muda mfupi na baadaye wanarudi kwenye mateso.
 

Watu walifikiri kuwa na fedha nyingi kunaleta furaha kwenye maisha, wakapambana sana wakazipata, lakini wakagundua bado. Wapo ambao wanakimbilia kutumia vilevi na madawa ya kulevya ili kupata furaha, lakini wanakuwa na raha ya muda mfupi, baadaye wanarudi kule kule walikokuwa.

Sasa swali kubwa likawa ni je hakuna namna ya kujihakikishia furaha? Je binadamu wamezaliwa kuwa na mateso maisha yao yote?

Hapa ndipo wanasaikolojia walipofanya tafiti, na kugundua kwamba chanzo kikuu cha furaha kwenye maisha, ni kuishi maisha yenye maana, kwa mtu mwenyewe. Yaani kama unataka kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha, basi ishi maisha yenye maana.

Swali jingine linakuja, maisha yenye maana ndiyo maisha gani? Ni jibu ni maisha yenye maana ni yale maisha ambayo mtu ana kusudi kubwa la maisha yake, na kusudi hilo lina msaada kwa wengine, na anafanyia kazi kusudi hilo.

Mwanasaikolojia na mwandishi William Damon, anatushirikisha kwenye kitabu chake cha NOBLE PURPOSE, namna ya kuishi maisha yenye maana, kulijua kusudi lako linalowasaidia wengine wengi na kuliishi kwenye maisha yako.

SOMA; Kauli Kumi(10) Zitakazobadili Mtazamo Wako Kuhusu Furaha Na Kukuwezesha Uwe Na Furaha Ya Kudumu.

Karibu sana tujifunze kupitia kitabu hichi;

1. Mshairi Cyprian Norwid alipata kuandika kwamba ili kuwa na maisha ya furaha, mtu anahitaji vitu vitatu kwenye maisha yake; moja ni kitu ambacho anaishi kwacho, yaani kitu ambacho maisha yake yapo kwa ajili ya kitu hicho. Pili ni kitu ambacho anaishi nacho. Na tatu ni kitu ambacho yupo tayari kufa kwa ajili ya kitu hicho. Kukosa kimoja kati ya hivyo vitatu ni tatizo, kukosa viwili ni majanga.

2. Pamoja na mahitaji ya msingi ya mtu ya kuhakikisha anaishi na kuzaliana, hivyo kuhakikisha anapata chakula, ulinzi na kujamiiana, mtu anahitaji kitu kikubwa zaidi, kitu kilichopo zaidi ya mahitaji haya ya msingi, ambacho kinamfanya kila siku awe na shauku ya kupiga hatua. Kitu hiki ni kusudi la maisha.

3. Kusudi la maisha ni kile kitu ambacho mtu ameitwa kufanya, kile kitu ambacho mtu anaweza kukifanya vizuri zaidi ya wengine, kile ambacho kila mtu anafurahia pale mtu huyo anapokifanya. Kusudi hili la maisha linaweza kupatikana kwenye kila eneo la maisha. Linaweza kupatikana kwenye kazi, biashara, familia, jamii na maeneo mengine mengi.

4. Njia ya kwanza ya kujua kusudi la maisha yako ni kujibu maswali haya matatu muhimu.
Swali la kwanza ni wewe ni nani? Usijibu jina lako, bali jibu wewe ni nani hapa duniani. Unajiona katika nafasi gani kwenye dunia hii.

Swali la pili ni kwa nini upo hapa duniani? Uko hapa kufanya nini, uko hapa kwa madhumuni gani?

Swali la tatu ni unataka kufanya nini na maisha yako? Unataka kuacha alama gani hapa duniani, ili hata utakapoondoka watu wajue kuna mtu aliwahi kupita hapo ulipo?
Jibu maswali hayo matatu na utaona namna unavyoweza kufanya makubwa zaidi. Uzuri hakuna majibu sahihi na ambayo siyo sahihi, jipe majibu na anza kuyaishi.

SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.

5. Katika kujua kusudi la maisha yako, kuna vitu vitatu muhimu unavyohitaji kuangalia.
Cha kwanza ni ule uwezo mkubwa ambao upo ndani yako. Kila mtu ana uwezo wake wa tofauti kabisa.

Cha pili ni uhitaji wa dunia kwa huduma ambayo unaweza kutoa kwa uwezo mkubwa ambao unao.

Cha tatu ni namna mtu anavyofurahia kufanya kile anachoweza kufanya, yaani anavyopenda kukifanya.

6. Unapolijua kusudi lako la maisha, chochote unachokifanya kinaacha kuwa kazi na badala yake kinakuwa wito. Kazi yako inapokuwa wito, inakuridhisha kwa kiasi kikubwa sana. Kazi inakuridhisha kuliko hata yale mapato unayopata, na unaporidhika na kazi, unaifanya kwa ubora kitu kinachopelekea kipato kuongezeka.

7. Maisha ambayo hayana kusudi, ni maisha ambayo hayafai kuishi, kwa sababu kila siku mtu anapelekwa kama upepo, haridhishwi na kile anachofanya na hana furaha. Hivyo kujua na kutengeneza kusudi la maisha yako ni kitu muhimu sana. Kama hujui kusudi lako, basi sasa tayari unalo kusudi, nalo ni kujua kusudi la maisha yako. Yaani sasa hivi una kusudi la kujua kusudi la maisha yako.

8. Ili kusudi liwe bora, ni lazima liwe linatoa mchango kwa maisha ya wengine, lazima liwe linafanya maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Kwa sababu wapo watu wanaoua kwa kusudi, wakijua wanafanya maamuzi bora kabisa. Kusudi bora lazima lifanye maisha ya wengine kuwa bora zaidi. Usiwe mbinafsi na kujifikiria wewe mwenyewe zaidi.

9. Hatupati kila tunachotaka kwenye maisha yetu, kwa wakati tunaotaka. Kuna wakati tunakosa na kuna wakati tunachelewa kupata kile tunachotaka. Unapokuwa na kusudi la maisha, haya yote hayawezi kukuangusha, kwa sababu unajua mlango mmoja ukifungwa, mingine inafunguliwa. Ila kwa wale wasio na kusudi, kukosa au kuchelewa kunazua malalamiko makubwa kwao.

10. Unapoishi kusudi la maisha yako, unahitaji kuwa mnyenyekevu. Kuwa na kusudi hakukufanyi wewe kuacha kuwa mwanadamu, hata kama kusudi lako ni zuri kiasi gani. Wewe ni binadamu na kila binadamu ana nafasi ya kukosea. Usipokuwa tayari kusikiliza, kujifunza na kurekebisha, unaweza kuwa na kusudi zuri lakini ukaleta matokeo mabaya sana. Unyenyekevu ni muhimu.

11. Unapoishi maisha ya kufanyia kazi kusudi lako, lazima uwe na misingi ambayo unaisimamia, bila hivyo unaweza kujikuta unaondoka kwenye njia ya kusudi lako. Siyo kwamba ukishakuwa na kusudi basi dunia itakuacha ufanye yako. Vitakuja vishawishi vingi vya kukufanya wewe uache kusudi lako, vitakuja vishawishi vingine vya kukufanya utafute njia ya mkato ambayo siyo sahihi. Jiwekee misingi ambayo utaiishi, na kamwe usiivunje.

SOMA; Njia Muhimu Za Kulinda Furaha Yako Wakati Wote.

12. Unapoweka lengo kwamba unachotaka ni furaha, huipati furaha, unapofanya kitu kwa kusudi la kupata furaha, furaha huwa haiji. Bali furaha ni zao la maisha yenye maana, inakuja wakati wewe unafanya yako, pale ambapo mawazo yako yote yamemezwa na kile unachofanya, huoni wala kufikiria kingine bali kile unachofanya, hapo ndipo unashindwa kutofautisha furaha na mateso, maisha yako yanakuwa bora sana.
Ipo misingi tisa muhimu unayohitaji kuwa nayo kwenye kuishi kusudi la maisha yako.

13. Msingi wa kwanza; hujawahi wala hujachelewa kuanza kuishi kusudi la maisha yako. Wapo watu ambao wanafikiri umri wao bado, na hivyo kuona wana muda wa kutosha mpaka waje kuanza kuishi kusudi la maisha yao. Wapo watu ambao wanaona muda wao umeshapita, na hivyo hawawezi tena kuishi kusudi la maisha yao. Ukweli ni kwamba hakuna kuchelewa wala kuwahi kwenye kuishi kusudi la maisha yako. Wakati wowote unapokuwa tayari, anza kufanyia kazi kusudi lako.

14. Msingi wa pili; kusudi la maisha yako lipo hapo ulipo tayari, huhitaji kwenda mbali kulitafuta, anza na maisha yako, anza na vile vitu unavyopenda kufanya, anza na vile vitu ambavyo huwezi kuvivumilia. Pia waangalie wale wanaokuzunguka, wananufaika na nini kutoka kwako.

15. Msingi wa tatu; tafuta mtu wa kukuongoza kwenye kuishi kusudi la maisha yako, angalia watu ambao wameshafika pale unapotaka kufika wewe, na jifunze kutoka kwao. Kama unaweza kupata wa kukuongoza moja kwa moja itakuwa vizuri. Ukikosa kabisa chagua katika wale ambao walishapita, kisha jifunze kupitia maisha waliyoishi kwa maandiko waliyoacha.

16. Msingi wa nne; ikiwezekana pata msaada kwa watu wanaoendana na wewe, wanaofikiri kama unavyofikiri wewe. Kwa bahati mbaya sana tunaishi kwenye jamii ambazo wengi hawaishi makusudi ya maisha yao, hivyo wanawakatisha tamaa wale wanaojaribu kufanya hivyo. Unahitaji kutafuta wale ambao nao wanaishi makusudi ya maisha yao, na kwenda nao pamoja. Hawa watakupa moyo kwenye safari ya kuishi kusudi la maisha yako.

17. Msingi wa tano; epuka kupotezwa na malengo unayoweka. Baadhi ya malengo ambayo watu wanayaweka kwenye kuishi kusudi la maisha yao, yanawapoteza kabisa na kufanya maisha yao kuzidi kuwa magumu na ya hovyo. Kwa mfano mtu anayesema kusudi lake ni kuondoa kabisa umasikini duniani, na atakuwa na furaha akikamilisha hilo, ameshajiandaa kutokuwa na furaha. Haijalishi anafanyia kazi lengo hilo kiasi gani, siyo kazi rahisi kufuta kabisa umasikini duniani.

18. Msingi wa sita; kuwa mnyenyekevu. Haijalishi kusudi lako ni kubwa au zuri kiasi gani, endelea kuwasikiliza watu, endelea kujifunza na endelea kubadili pale unapokosea. Ukijiona wewe ndiyo wewe, utajipoteza wewe mwenyewe.

19. Msingi wa saba; usiangalie mwisho pekee, angalia na njia pia. Kinachowafanya wengi wanakosa furaha kwenye maisha, ni kuangalia mwisho na kusahau njia. Wanaona furaha ni kama kitu unachopata pale mwisho, hivyo wanasahau njia, na hata wakifika mwisho, wanakuta sivyo walivyotegemea. Unapoishi kusudi la maisha yako, njia ni muhimu kuliko hata mwisho. Hakikisha njia unayotumia ni sahihi na unaipenda na kuifurahia.

20. Msingi wa nane; sherekea kusudi lako na shukuru kwa kila unachopata. Chochote unachopata kwenye maisha yako, ni bahati, kwa sababu wapo wengi kama wewe ambao walitaka kupata ila hawajaweza kwa sababu mbalimbali. Hivyo sherekea na furahia, na muhimu zaidi shukuru kwa kile ulichopata. Unapokuwa mtu wa shukrani unapata zaidi.

21. Msingi wa tisa; wasaidie wengine kuishi kusudi la maisha yao. Unapoweza kuishi kusudi la maisha yako, wawezeshe wengine, hasa vijana na wao kuishi kusudi la maisha yao. Chagua vijana ambao utawaongoza na kuwasimamia ili waweze kufikia kusudi la maisha yao. Ni jambo bora sana mafanikio yako yanapokuwa mwanga kwa mafanikio ya wengine.

22. Una maisha hayo uliyonayo tu, hivyo usiyapoteze kwa kuishi bila kusudi la maisha yako. Jua kusudi lako, na liishi kila siku, utakuwa na maisha yenye furaha, utawasaidia wengi na kufanya maisha yao kuwa bora, utafanikiwa sana na utakapoondoka, utaacha alama hapa duniani. Je hutaki yote hayo? Kama unayataka, chukua hatua sasa.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>