Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Hii Ndio Falsafa Muhimu Unayotakiwa Kumpatia Mgeni Wako.

$
0
0
Habari ya leo mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu kuwa hujambo na unaendelea kuboresha maisha yako bila kusahau kugusa na maisha ya watu wengine, leo ni siku bora na ya kipekee kwetu tunakwenda kufanya makubwa na kutegemea kupata makubwa zaidi.
Mpendwa rafiki, tunaalikwa kutumia vema muda wetu wa leo katika kuzalisha yale mambo chanya, pia unaweza kujiondoa kwa makusudi kabisa katika yale mambo hasi ambayo yanakupotezea muda bure katika maisha yako. Nitume nafasi hii niweze kukukaribisha tena katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza wote kwa pamoja yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo.

Katika somo letu la leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja falsafa unayotakiwa kumpatia mgeni wako au tunaweza kusema leo tutajifunza falsafa ya mgeni. Je falsafa ya mgeni ni ipi? 

Karibu tusafiri pamoja ili tuweze kuifahamu wote kwa pamoja falsafa hii muhimu kwa wageni wetu.

Mpendwa msomaji, katika hali ya kawaida kila mtu ameshawahi kufikiwa na mgeni nyumbani kwake, au hata sehemu nyingine iliyokusudiwa kukutana na mgeni wako. Mara nyingi mgeni anayekuja kukutembelea kwako huwa ni mtu wa pekee sana kwetu kwani anatumia nguvu, muda, hata fedha kuweza kuja kukutembelea wewe. Ni japo la kipekee sana linalojenga urafiki, undugu, ujirani hata ujamaa pale mtu wako wa karibu anapoamua kuja kukutembelea huwa linajenga mahusiano imara sana.

Wageni wetu huwa tunapenda kuwapa heshima pale wanapotutembelea sehemu tunazoishi na kujihisi watu wa furaha sana pale tunapotembelewa hususani na mgeni ambaye hamjaonana muda mrefu hivyo kila mmoja anakuwa na shauku na mwenzake. Tunapaswa kujifunza kitu kimoja ambacho leo nimependa tushirikishane kuhusiana na wageni ambacho ni falsafa ya mgeni.

SOMA; Kama Wewe Ni Mgeni Wa Maisha Ya Mafanikio, 2017 Fanya Mambo Haya Matatu Tu, Usijisumbue Na Mengine.

Ndugu msomaji, falsafa ya mgeni ni ukarimu, pale mgeni yeyote anayekuja kutembelea sehemu au mahali unapoishi huna budi kumwonesha ukarimu wa hali ya juu. Kama tunavyojua watalii wanavyooneshwa ukarimu basi nasi wageni wetu wanaotutembelea tunapaswa kuwaonesha ukarimu wa hali ya juu mpaka mwenyewe ashangae. Mtendee ukarimu mpaka ajihisi mwenyewe yuko sehemu salama hapa duniani, tunajua ukarimu huwa unamfanya mgeni ajihisi anapendwa na hata kuthaminiwa.

Ndugu, pale mgeni anapokuwa amekuja kukutembelea basi jitoe kumhudumia kwa ukarimu unaanza kumkaribisha kwa uso wenye tabasamu na kumuonesha upendo hata kama alikuwa ana huzuni tabasamu lako na furaha uliyokuwa unamuonesha wakati wa kumpokea inaondoka yenyewe. Mgeni akija kwako usimwangalie tu, bali ongea naye vizuri, mwangalie usoni onesha mawasiliano ya macho kwa macho unapokuwa na mgeni wako kwani huo ndiyo uhai wa mawasiliano.

Mwandalie chochote mgeni wako pale anapokuwa amekuja kukutembelea kama unaweza kumpatia maji basi mpatie, kama unaweza kumpatia juisi basi mpatie, matunda, chakula, chai na vingine kulingana na mazingira uliyopo na kutegemeana na hali ya hewa pia. Angalia wakati uliopo unapaswa kumpatia kitu gani mgeni wako na mpatie. Huwa si falsafa nzuri mgeni kuja kwako na kumwangalia tu, hakikisha unajitoa kwake kumhudumia na kumwonesha ukarimu kama vile siku nyingine hatokuja kwako na usimwache mgeni aje kwako na kumwacha aende tu bila hata kumpatia chochote naye ahisi amekarimiwa.

Kwa hiyo, tunaalikwa kuwaonesha ukarimu wageni wetu pale wanapokuja kututembelea sehemu tunazoishi, mbali na hayo mgeni anapokuja kwako unatakiwa kumpa muda wa kukaa naye siyo kumwacha peke yake na wewe kuendelea na shughuli zako. Unakuta watu wengine mgeni akienda kwake anamwashia tv na kumwacha hapo na yeye anaendelea na mambo yake. Je mgeni anakuja kukutembelea kwako au kukusalimu amefuata kuangalia tv? Au kupewa juisi na kuachwa sebuleni? Hapana amekufuata wewe na hivyo mpe heshima ya kuthamini muda wake, thamani ya muda wake na ule utu wa kuja kwako huwezi kuulipa kwa gharama yoyote ile.

SOMA; Hii Ndiyo Nyumba Adimu Sana Kupatikana Katika Zama Hizi Za Taarifa.

Mpendwa msomaji, epuka kumkera mgeni wako na mambo kama vile kuwa bize na simu muda wote, huna muda naye, umenuna muda wote kama vile hukutaka mtu kuja kwako, acha kisirani chako muoneshe mgeni uso wa furaha, tabasamu. Kaa naye rudisha fadhila kwa mgeni wako na shukuru kwa mgeni kuja kukutembelea kwani kuna watu wanatamani hata kutembelea na mgeni hawapati hivyo ukipata nafasi itumie vema.

Rafiki, pia napenda kutoa angalizo kwa mgeni, huenda mwenyeji amekuonesha ukarimu wa hali ya juu na alikukirimia vizuri ulivyokwenda kwake sasa na wewe unatumia nafasi hiyo kwenda kila siku hapana hapo utakua unamuuzia mwenyeji wako na kumkomoa. Wengine wanatumia ni fursa sasa kama alihudumiwa vema alivyoenda kwa Fulani naye anataka kwenda kila siku huko ni kukomoana na kuumizana. Waswahili wanasema wema usizidi uwezo , mhudumie pale mkono wako unapofika na kama huwezi acha hakiko ndani ya uwezo wako.

Hatua ya kuchukua leo, kila mtu anaweza kuwa mgeni katika maisha yako, hivyo tumejifunza kuwaonesha falsafa ya ukarimu wageni wetu pale wanapokuja kututembelea pale tunapoishi. 

Mkarimu kama ndiyo siku yako ya mwisho kumuona hapa duniani na mfanye ajihisi yuko sehemu salama.

Kwa kuhitimisha, tumealikwa kuishi kwa upendo na kuonesha ukarimu kwa wageni wetu pale wanapokuja kutusalimia majumbani mwetu. Thamani ya mtu anayekuja kwako huwezi kuilipa hivyo unaweza kumlipa kwa kumpa muda wako na kutoa ukarimu wa hali ya juu kwake. Mgeni ni kama mtalii anapokuja kwako, usipomwonesha ukarimu hawezi tena kurudi kwako, hivyo ukarimu ndiyo lugha ya mgeni.

Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>