Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; MINDFRIK (Jinsi Unavyoweza Kutawala Ulimwengu Wako Wa Ndani Ili Kufanikiwa Kwenye Ulimwengu Wa Nje.)

$
0
0
Kila mtu anapenda mafanikio, lakini ni wachache ambao wanaweza kuyafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yao. Licha ya kila mtu kujua wapi anataka kufika, licha ya juhudi kubwa ambazo kila mtu anaweza kuweka, bado kipo kikwazo kikubwa cha mafanikio ambacho wengi hawakijui.
 

Kikwazo hicho ni fikra na mitazamo yetu ya ndani juu ya maisha na mafanikio kwa ujumla. 

Mwandishi T. Harv Eker, ametuandalia kijitabu kidogo ambacho kinatupa mbinu za kuweza kuutawala ulimwengu wetu wa ndani, yaani mitazamo na fikra zetu ili tuweze kufanikiwa kwenye ulimwengu wa nje.

Karibu tujifunze kwa pamoja namna tunavyoweza kutawala ulimwengu wetu wa ndani na kufikia mafanikio makubwa.

1. Watu wanaishi vile wanavyoishi siyo kwa sababu wanapenda, ila kwa sababu ndiyo namna pekee ya kuishi wanayoijua, waliyofundishwa kwenye malezi waliyopata. Hawajui kama ipo njia nyingine ya kuwawezesha kuwa na maisha bora na ya mafanikio kwao. Ipo njia ya kipekee kwa kila mmoja wetu kuweza kuipita, njia hii ni maalumu kwa kila mtu na ina mafanikio yake. Ni muhimu ujiue njia maalumu kwako na uache kufuata zile zinazofuatwa na kila mtu.

SOMA; Hizi Ndizo Nguvu Tatu Za Kukupa Maisha Unayoyatamani.

2. Mtu yeyote anayetaka kuipata njia yake ya kipekee ya maisha ya mafanikio, anaweza kuipata, kama kweli amejitoa kuipata. Wengi hawaipati njia hii kwa sababu hawajitoi kuitafuta, ni rahisi kuishi kwa mazoea kuliko kutengeneza maisha ya kipekee. Kupitia kitabu hichi utakwenda kujifunza namna ya kutengeneza maisha ya kipekee kwako,

3. Moja ya mambo muhimu yatakayokuwezesha kuishi maisha yako kwa upekee na kama utakavyo, ni kuweza kuwa kwenye wakati uliopo. Watu wengi wanapoteza maisha yao kwa kuishi jana, ambayo imeshapita na hawawezi kuibadili au kuishi kesho, ambayo bado haijafika na hivyo hawawezi kuiathiri, huku wakisahau leo, wakisahau muda huu walionao. Anza kuishi leo, anza kuchukua muda kwenye huu wakati ulionao, na yaweke mawazo yako kwenye kile unachofanya sasa.

4. Kuna tofauti kubwa ya kimtazamo kati ya waliofanikiwa na wale wanaokazana bila ya mafanikio. Na hii iko hivi, wale ambao wanakazana na maisha na hawana dalili za mafanikio mtazamo wao uko hivi; PATA, FANYA, KUWA. Wanajiambia nikipata kitu hiki, nitafanya hivi na nitakuwa vile. Mfano nikipata fedha, nitafungua biashara na nitakuwa tajiri. Hii ni njia ambayo ipo kinyume kwa sababu huwa mambo hayaendi hivyo. Wanaofanikiwa wana mtazamo wa KUWA, FANYA, PATA. Wao wanaanza kuwa jinsi wanavyotaka kuwa, wanachagua kufanya kile wanachotaka kufanya na kuweza kupata chochote wanachotaka.

5. Mafanikio yoyote kwenye maisha yanaanzia ndani, yanaanzia kwenye mtazamo na fikra ambazo mtu anazo. Mtu anaweza kuwa na kila kitu kinachohitajika ili afanikiwe, lakini kama ndani siyo imara, ataanguka tu. Umekuwa unaona kila siku watu ambao wana kila fursa ya mafanikio, lakini hawafanikiwi, tatizo siyo nje, tatizo ni ndani.

6. Hatua ya kwanza ya kujenga uimara ndani yako ni kupunguza kelele za akili yako. Popote unapokuwa, akili yako imekuwa inakupigia kelele. Kelele hizi zinakuja kwa mfumo wa mawazo mbalimbali ambayo akili yako inakuwa nayo. Sehemu kubwa ya mawazo haya huwa ni hasi, unaiona fursa nzuri kabisa lakini akili inaanza kukuambia vipi kama utashindwa, au kuja na hofu nyingine zinazokuzuia kuchukua hatua. Usipoweza kudhibiti akili yako, itakuwa kikwazo cha kwanza kwako kufanikiwa.

SOMA; Siri Hii Itakusaidia Kuondokana Na Msongo Wa Mawazo Wa Kukosa Muda Katika Ulimwengu Huu Wa Utandawazi - 3

7. Hapo ulipo una nafsi mbili, una nafsi yako ya kweli, na nafsi yako ya uongo. Nafsi yako ya kweli ni vile wewe ulivyo, jinsi ulivyo tofauti na wengine, uwezo mkubwa na wa kipekee ulionao na vipaji ulivyonavyo. Nafsi yako ya kweli ni ule utofauti ulionao na wengine. Nafsi yako ya uongo ni vile ulivyofundishwa kuwa, namna ulivyotengenezwa na jamii, na kulazimishwa kufanya vitu ambavyo hujawahi kujua kwa nini unavifanya, unafanya tu kwa sababu kila mtu anafanya. Au sababu inayokufanya ufanye, haiendani na kile unachokitaka wewe. Huwezi kufanikiwa kamwe, hata kama utapewa fursa kubwa kiasi gani, kama bado unaishi kwenye nafsi yako ya uongo. Na cha kushangaza, wengi sana wanaishi kwenye nafsi zao za uongo.

8. Ulikuja hapa duniani ukiwa tupu kabisa, hukuwa unajua chochote unachojua sasa, ulikuja akili yako ikiwa kama daftari jipya. Baada ya kuingia kwenye maisha haya, ulianza kuandika vitu kwenye akili yako, ambavyo huenda mpaka leo unavitumia. Kwa mfano, ulipokuwa mdogo, hukuweza kusema unasikia njaa, hivyo ulipopata njaa ulimwangalia mama usoni akawa hakuelewi, huenda ukaonesha vitendo kwamba una njaa hakukuelewa, mwishoni ukalia kidogo hakuelewa, ndipo ulipolia kwa sauti kubwa na hapo akaelewa kwamba una njaa. Hivyo uliandika hili kwenye akili yako kwamba kadiri ninavyolia kwa sauti ndiyo watu watanijali zaidi, na huenda umeishi na hilo mpaka leo, kitu kidogo unapiga kelele ili wengine waje. Hilo ni moja, jiulize yapi mengine umeandika kwenye akili yako ambayo hayana maana kubwa kwako?
 

9. Uko hivyo ulivyo sasa, na haiba ambayo unayo sasa kutokana na hitaji lako la kuendelea kuwa hai. Kama umekulia kwenye mazingira ambayo ni magumu na ili uwe hai lazima upambane sana, utakuwa na haiba ya upambanaji. Kama umekulia kwenye mazingira ambayo kila kitu ni haba, utakuwa na mtazamo wa uhaba kwenye kila kitu muhimu kwenye maisha yako. Kitu kingine muhimu sana kujua ni kwamba asilimia 90 ya vile ulivyo sasa, umejifunza ukiwa mtoto. Mengi umeyabeba kutoka kwa wazazi, jamii, vyombo vya habari, walimu na kila kinachokuzunguka. Sasa kwa kuwa wale ulioiga kwao nao wameiga, ndiyo maana inakuwa vigumu sana kwako kufanikiwa kama hutabadili yote hayo.

10. Ili kuweza kushinda nafsi yako ya uongo na kuingia kwenye nafsi yako ya kweli lazima ulewe kwamba wewe siyo kanda iliyorekodiwa, bali wewe ndiye unayeicheza hiyo kanda, hivyo unaweza kuibadili muda wowote unaotaka. Lazima uelewe kwamba wewe siyo akili yako, bali wewe ndiye unayeiongoza akili yako, hivyo muda wowote unaweza kubadili fikra na mitazamo uliyoibeba kwa muda mrefu kwenye maisha yako. Uhuru wako unakuja pale unapoweza kujitofautisha wewe kama wewe na chochote unachofikiri ni wewe. Jua wewe uko juu ya chochote kinachohusika na wewe, na unaweza kubadili chochote kwenye maisha yako.

11. Samaki hawezi kujua yupo kwenye maji mpaka pale anapotolewa nje ya maji. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwako, huwezi kujua kama unaishi kwenye nafsi ya uongo mpaka pale utakapotoka kwenye nafsi hiyo na kuonja maisha ya nafsi yako ya kweli. Umeishi kwenye nafasi ya uongo mpaka umeshaamini kwamba hayo ndiyo maisha pekee yaliyopo kwako wewe. Ni uongo, yapo maisha makubwa sana kwako, ondoka kwanza kwenye hayo maisha uliyotengenezewa, na anza kutengeneza maisha yako mwenyewe.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa FLIGHT PLAN The Real Secret Of Success.

12. Una njia mbili za kuondoka kwenye nafsi yako ya uongo na kuanza kuishi nafasi yako ya kweli. Njia ya kwanza ni kuibadili akili yako taratibu, kuanza kujifunza mambo mapya, kutengeneza mitazamo chanya na kujijengea tabia mpya za mafanikio. Njia ya pili ni kuukwepa kabisa mfumo uliojengewa wa kuendeshwa ka hofu na matatizo na kuanza kuishi kwenye mfumo unaoendeshwa kwa upendo na kusudi. Hapa ndipo unapoamua kuwa nahodha wa meli ya maisha yako, kuhakikisha unadhibiti kila kitu kwenye maisha yako.

13. Njia ya haraka ya kufikia nafsi yako ya kweli, ni kutuliza akili yako ambayo inaishi kwenye nafsi ya uongo. Kama tulivyoona, nafsi yako ya uongo inaishi kwenye hofu na matatizo, anza kuondokana na mawazo hayo, anza kufikiria ni kipi unapenda kwenye maisha yako, anza kufikiria kusudi lako kubwa la maisha, na utahamisha mawazo yako kutoka kwenye nafsi ya uongo na kwenda kwenye nafsi ya kweli.

14. Huhitaji kwenda popote ndiyo uweze kuondoka kwenye nafsi yako ya uongo na kuishi kwenye nafsi yako ya kweli. Ukweli ni kwamba hapo ulipo sasa, ndipo unapopaswa kuwa, ila unachohitaji kufanya ni kudhibiti akili yako, kuhamisha mawazo yako na kuanza kuziona fursa bora zaidi.

15. Ukishaanza kuishi kwenye nafsi yako halisi, kuna hisia unazipata ambazo ni za tofauti kabisa. Kuna wakati unapata hisia ya kufanya jambo fulani, ambalo huwezi kuelezea kwa nini, na ukilifanya linakuwa zuri sana kwako. Wengine wanaweza kusema una bahati, lakini ukweli ni kwamba kwa kuishi kwenye nafsi yako ya kweli, unakuwa umepata nafasi ya kuungana na uwezo mkubwa kabisa wa asili. Wengine wanaweza wakahofia kufanya jambo fulani kwa sababu wao bado wanaishi kwenye nafsi za uongo, ila wewe ukapawa na msukumo wa kulifanya, na ukafanikiwa sana. Hii siyo bahati, bali ni uwezo uliopo ndani ya kila mmoja wetu anapoishi nafsi yake ya kweli.

16. Msongo wa mawazo (stress) ni kitu ambacho kinatoka ndani ya mtu na kinamuumiza mtu mwenyewe. Yaani hakuna mtu anayeweza kukuumiza na stress zake, bali unatengeneza stress zako na zinakuumiza sana. Msongo wa mawazo ni matokeo ya akili yako kubishana na wewe mwenyewe. Na hii inatokea sana kwa wale wanaoishi kwenye nafsi za uongo. Kwa sababu hawana uhakika na kile wanachofanya, wanajikuta wakifikiri mara nyingi, pamoja na hofu juu ya kile wanachofanya. Dawa ya msongo wa mawazo ni kuanza kuishi nafsi yako ya kweli.

17. Kanuni ya maisha ni hii; MAWAZO yako yanapelekea HISIA unazokuwa nazo na hisia zako ndiyo zinaathiri MATENDO yako na matendo ndiyo yanaleta MATOKEO unayopata kwenye maisha yako. Hivyo kama hupati matokeo mazuri, tatizo halijaanzia kwenye kile unachofanya, bali linaanzia kwenye mawazo yako, lipo ndani kabisa kwenye mtazamo wako.

18. Unapoishi kwenye nafsi yako ya kweli, unafika wakati unaweza kufanya jambo bila hata ya kuwaza sana, kwa sababu una imani kwenye kile unachofanya. Na hii ndiyo inayopelekea wale wanaoishi kwenye nafsi zao za kweli kufanikiwa sana. Wakati wengine wakiwaza sana mpaka kuwa na msongo wa mawazo, wale wanaofanikiwa wanaweza kujikuta wakifanya tu jambo na likaleta matokeo makubwa sana. Siyo kwa sababu wana bahati, ila kwa sababu wameonja maisha ya juu sana, maisha ambayo hayaendeshwi kwa hofu bali kwa imani na upendo.

19. Mabadiliko yoyote kwenye maisha ni kujitambua. Huwezi kubadilika kama hujajitambua, huwezi kuishi kwenye nafsi yako ya kweli kabla hujajua kwamba unaishi kwenye nafsi yako ya uongo. Kwa siku saba zijazo, fuatilia mawazo yako kwa karibu sana. Kuwa na kijitabu popote unapokuwa, na kila baada ya muda mfupi, kila baada ya saa moja, jiulize unafikiria nini na una hisia gani kwa wakati ule, kisha andika kile unachofikiria na hisia ulizonazo. Hii ni hatua ya kwanza kabisa ya kujua pale ulipo ili uweze kubadilika.

20. Kusudi kuu la kijitabu hiki, lilikuwa kukuwezesha wewe kuishi maisha ambayo yamejengwa kwenye misingi ya upendo na kusudi badala ya maisha yaliyojengwa kwenye misingi ya hofu na matatizo au wajibu. Watu wanaoishi kwenye nafsi zao za kweli, wanafanya kila wanachofanya kwa sababu wanapenda kufanya na wana kusudi la kufanya. Iwe ni kazi, biashara, familia na kila kitu, wanapenda kweli na wana makusudi makubwa ya kufanya, hivyo hawachoki kufanya. Watu wanaoishi kwenye nafsi zao za uongo, wanafanya kila wanachofanya kwa sababu ya hofu na majukumu au matatizo. Iwe ni kazi au biashara, mtu anafanya kwa sababu ana hofia asipofanya atakosa fedha na maisha yatakuwa magumu. Anafanya kwa sababu ni wajibu kufanya na siyo kwa sababu kuna mchango mkubwa anatoa kwa wengine. Hii inawafanya waone maisha yao ni mzigo na mateso mpaka siku wanayoondoka hapa duniani. Chukua hatua sasa ya kuhama kutoka kwenye nafsi ya uongo na kuanza kuishi nafsi yako ya kweli. Jua kusudi la maisha yako ni nini, na jua vitu gani unapenda kwenye maisha yako, kisha jitoe kadiri ya uwezo wako kuhakikisha unafanya vile unavyopenda na unatimiza kusudi lako. Hakuna mwingine anayeyaishi maisha yako ila wewe mwenyewe.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>