Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Uchambuzi Wa Kitabu; So Smart But... (Jinsi Watu Wenye Akili Wanavyopoteza Heshima Zao Na Jinsi Ya Kurudisha Heshima).

$
0
0
Moja ya vitu vinavyotutofautisha binadamu na viumbe wengine, ni uwezo mzuri wa kuwasiliana. Hivyo mawasiliano yetu ndiyo yanayojenga kila kitu tunachotaka kwenye maisha. Kupitia mawasiliano ndiyo tunaweza kuwa na mahusiano mazuri na wengine na kuweza kushirikiana kwenye mambo mbalimbali.


Lakini mawasiliano siyo rahisi, mawasiliano siyo kuongea au kuandika tu kile unachotaka. Mawasiliano ni dhana pana, inayohusisha maneno, matendo na hata hisia.

Watu wengi wenye akili na wasomi, wamekuwa wakipoteza heshima zao kwenye kazi, biashara na hata maisha kwa ujumla, kwa kushindwa kutumia vizuri mawasiliano. 

Wanashindwa kwenda vizuri na wengine na hilo linawanyima fursa nyingi kwenye maisha yao.

Mwandishi na mshauri wa mawasiliano, Allen Weiner anatushirikisha uzoefu wake wa zaidi ya miaka 30 kwenye kuwashauri na kuwafundisha watu njia bora kabisa za mawasiliano.

Kupitia kitabu hichi cha SO SMART BUT... anatueleza sitofahamu wanazokutana nazo watu, hasa walioajiriwa, ambao wanaweza kufanya kazi zao vizuri sana, lakini inapokuja kwenye mawasiliano, hawawezi. Wanajikuta wanapoongea jambo wanawakasirisha wengine, au wanaonekana wana dharau, au kuwafanya wengine wasiwe na hamasa ya kuwasikiliza. Allen ametushirikisha mbinu za kuboresha mawasiliano yetu, ili tuweze kushirikiana na wengine vizuri na kuweza kufanikiwa.

Haya hapa ni mambo muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hichi, yapitie na uone unawezaje kuyatumia kwenye maisha yako ili kuboresha maisha yako.

1. Watu wote wanaofikia kilele cha fani au kazi zao, bila kujali ni fani au kazi gani, ni watu ambao wanaweza kuwasiliana vizuri. Hata viongozi wakuwa wa biashara, kampuni, mashirika na hata serikali, ni wale ambao wanaweza kuwasiliana vizuri, wanaoweza kuwaambia wengine kitu na wakaeleweka. Hivyo mtu yeyote ambaye anataka kufanikiwa, ni lazima afanyie kazi mawasiliano yake, maana hayo ndiyo yatamwezesha kufanya makubwa kupitia wengine.

2. Katika mawasiliano kuna mambo matano muhimu unayopaswa kuzingatia ili uweze kueleweka, kuaminika na kuheshimika.

Moja ni ujuzi, lazima ujue kwa kina kile ambacho unasema au kuandika.

Mbili ni tabia, tabia yako inaathiri kile unachosema na namna unavyokitoa kwa wengine.

Tatu ni utulivu wako katika kuwasilisha ujumbe wako. Kama unaonekana kuwa na wasiwasi na kutokujiamini, watu hawatapokea ujumbe wako.

Nne ni namna unavyojumuika na wengine.

Tano ni tabia yako inapokuja kwa watu wengine, je unapokuwa na wengine, huwa unapenda kuongea au unapenda kukaa mwenyewe? Msukumo wa kuongea na wengine, unakusaidia kueleweka kwenye mawasiliano yako.

3. Ukiacha kile unachoongea, mwili wako nao unatoa viashiria vingi vya mafanikio. 

Unaweza kuwa unaongea kitu muhimu, lakini namna ulivyokaa au kusimama, namna ulivyoweka uso wako na namna unavyowaangalia au kutowaangalia wengine, ujumbe huo 
usichukuliwe kwa uzito unaotaka.

Unapoongea na wengine, kwanza kabisa kuwa na utulivu, waangalie usoni, ongea kwa sauti na kujiamini, usijishike shike maeneo mengine ya mwili na usionekane kama una wasiwasi au hofu.

4. Watu hupenda kusema usihukumu kitabu kwa ganda la nje, mpaka ukisome kwanza, 

lakini kwenye mawasiliano, watu wanakuhukumu kwa mwonekano wako wa nje. Namna watu wanavyokuona, kuanzia mavazi, sura, matumizi yako ya viungo na kadhalika, watu wanavichukulia kwa uzito. Njia pekee ya kuwafanya watu wasikuhukumu kwa mwonekano wako, ni kuwa na ujumbe mkali sana ambao watu wanauhitaji au wamehamasika kuufuatilia.

5. Usahihi wako wa lugha na uchaguzi wa maneno pia unahusika sana kwenye kukamilisha mawasiliano yako. Kama unatumia maneno ambayo yamekosewa kosewa, watu wanachukulia haupo makini. Kama unatumia maneno magumu ambayo wengi hawayaelewi, wewe unaweza kuona ni sifa kwa kuonekana unajua, lakini watu hawatakuelewa.

Tumia lugha sahihi na kwa umakini, tumia maneno ambayo kila unayemlenga atakuelewa, hiyo ndiyo njia ya kuwa na mawasiliano bora.

6. Yapo maeneo matano yanayojenga heshima kwenye mawasiliano;

Eneo la kwanza ni chanzo cha mawasiliano au ujumbe husika.

Eneo la pili ni ujumbe ambao unawasilishwa.

Eneo la tatu ni muktadha wa mawasiliano, eneo ambalo mahusiano yanahusisha.

Eneo la nne ni asili ya mpokeaji wa ujumbe ambao unawasilishwa.

Eneo la tano ni muda wa ujumbe huo unaowasilishwa.

Hivyo unapowasiliana, jiangalie wewe, zingatia ujumbe unaotaka kutoa, kwa eneo unalotaka kuhusisha, kwa watu sahihi na muda sahihi wa ujumbe huo.

7. Ujumbe wowote unaowasilishwa una sifa tano muhimu za kuzingatia wakati wa kuwasilisha.

Sifa ya kwanza ni ujumbe wenyewe, ile dhana kuu ambayo unataka watu waipate.

Sifa ya pili ni upana wa ujumbe au dhana husika, hapa unaangalia ukubwa wa kile unachowasilisha.

Sifa ya tatu ni kina cha dhana husika, hapa unatoa maelezo ya kina ya ujumbe unaotoa.

Sifa ya nne ni kuangalia urefu wa dhana husika, hapo unaangalia madhara yake kwa marefu.

Sifa ya tano ni maono yanayohusiana na ujumbe unaotoa, hapa ni kule mbali ambapo unaangalia.

8. Unapopewa nafasi ya kuwasilisha mada yako kwa mtu ambaye hana muda mrefu wa kusikiliza, unapaswa kutumia muda mfupi iwezekanavyo, chini ya dakika tano kuweza kumpa mtu picha kamili ya unachotaka aelewe ili aweze kufanya maamuzi. Ujumbe wako unapaswa kuwa na maeneo matano;

Eneo la kwanza ni tatizo au fursa, hapo unaeleza tatizo ni nini au fursa ni nini.

Eneo la pili ni kinachosababisha tatizo, au kinachovutia kwenye fursa.

Eneo la tatu ni madhara ya tatizo iwapo halitafanyiwa kazi au hasara kama fursa haitafanyiwa kazi.

Eneo la nne ni suluhisho la kuchukua ili kutatua tatizo, au hatua za kuchukua ili kunufaika na fursa.

Eneo la tano ni hatua ya kuchukua.

Kwa ujumbe au jambo lolote unalotaka kuwasilisha kwa wengine, zingatia maeneo hayo matano, utaeleweka ndani ya muda mfupi na watu watajua kwa nini wachukue hatua, na hatua ipi wachukue.

9. Viongozi wanaoheshimika wana maono ya aina ya tatu.

Maono ya kwanza ni maono ya ndani, hapa wanakuwa wanajijua wao wenyewe, kwa uimara wao na udhaifu wao.

Maono ya pili ni maono ya karibu, hapa wanakuwa wanawajua vizuri watu wanaowazunguka na namna ya kuwasiliana nao.

Maono ya tatu ni maono ya mbali ambayo yanahusisha kuwa na ndoto kubwa ambazo wanazifanyia kazi na namna ya kuziwasilisha kwa wengine na wakazielewa.

10. Unapokuwa na utulivu wewe binafsi, unapunguza msongo wa mawazo kwa wengine. 

Kama wewe ni kiongozi, na kwenye mawasiliano yako unaonesha hali ya wasiwasi au hofu, unapeleka hilo kwa walio chini yako na hata walio juu yako. Hivyo kwenye mawasiliano, hakikisha unakuwa na udhibiti wa kutosha kwako wewe binafsi.

11. Matumizi yako ya muda pia yanachangia sana kwenye mawasiliano yako. Kama umechelewa eneo ambalo ulipaswa kufika kwa muda fulani, wengi wanakuchukulia hujajipanga vizuri au huzingatii mambo. Kama unachukua muda mrefu kuwasilisha kuliko ulivyotegemewa, inawaonesha watu hujajipanga.

12. Kama umeandaa mada unayowasilisha kwa wengine kwa njia ya masomo ya kwenye kompyuta (power point) usitumie muda mwingi kusoma kila ulichoandika, badala yake waelezee watu. Na ili kuepuka hilo, usiweke maelezo mengi ambayo yatawafanya watu wakazane kuyasoma, badala yake weka pointi tu, na maelezo toa wewe, ili watu wakufuatilie wewe.

13. Unapowasilisha jambo mbele ya watu, labda mbele ya jukwaa, usizunguke zunguke jikwa zima bila ya ulazima. Kufanya hivyo inaonesha una wasiwasi au hujiamini. 

Kusimama sehemu moja na kutumia mikono yako kuonesha vitendo, inawafanya watu kukufuatilia kwa makini.

14. Unapoongea na wengine, ongea kwa namna ambayo inaonesha unaheshimu mawazo yao pia. Kuongea kama vile wewe ndiyo pekee unayejua kila kitu, au ndiyo pekee ambaye upo sahihi, inaonesha dharau kwa wengine na mawasiliano yako hayatakuwa mazuri.

15. Unapotaka kumkosoa mtu kwa kitu alichosema, kosoa kile alichosema tu, usimhusishe yeye wala chochote kinachohusiana na yeye. Wengi hukimbilia kuwakosoa watu, na hilo huwaumiza na kupelekea mawasiliano kuvunjika.

16. Kupitia mawasiliano yako, hakikisha unajenga uaminifu, kama umeahidi kitu tekeleza. 

Pia usidanganye, kwa sababu ukidanganya, watu watakuja kujua ukweli, na wakishajua ulidanganya, itakuwa vigumu sana kwao kuamini tena chochote unachosema. Watajiuliza sasa anasema kweli au anaongopa tena?

17. Kitu kingine kinachochangia mawasiliano kuwa mazuri na kueleweka ni kukubalika kwako au kupenda na wengine. Watu ambao wanakubalika na wengine, huwa na ushawishi mkubwa kwao. Njia ya kukubalika na wengine ni kujenga marafiki ya urafiki, na kujali wengine.

18. Watu wanapenda kuthaminiwa, na kuonekana wa muhimu. Unaweza kutumia hitaji hili la watu katika kujenga mawasiliano mazuri. Kwa mfano kila mtu ana maoni juu ya jambo husika, na wakiombwa ushauri, hufurahia kutoa kile wanachojua au kuamini wao. 

Hivyo unaweza kuanza mawasiliano na mtu kwa kauli; naomba ushauri wako juu ya hili.... mtu atakuwa tayari kukusikiliza na hapo unaweza kufikisha ujumbe wako.

19. Njia nyingine ya kuwafanya watu wakusikilize au kukufuatilia kwa makini unapowasilisha kitu, ni kutoa hadithi. Kabla hujaingia kwenye ujumbe unaotaka kutoa, anza na hadithi, inaweza kuwa mfano halisi au hadithi tu ya kutungwa, ambayo inaendana na ujumbe unaotaka kutoa. Binadamu ni viumbe tunaopenda hadithi, kwa kuanza tu na hapo zamani za kale, watu wanaacha kila walichokuwa wanafikiri na kusikia hadithi inayofuata.

20. Unahitaji kuwa na hamasa kubwa ndani yako juu ya kile unachowasilisha. Hamasa hiyo inaambukizwa kwa wale unaowawasilishia na wanahamasika kuchukua hatua. Lakini kama kitu hakikuhamasishi, watu hawatapata msukumo wa kuchukua hatua. Hivyo ujumbe wowote unaotaka watu wauelewe vizuri na kuchukua hatua, hakikisha unakuhamasisha wewe kwanza, uanze kuwasha moto ndani yako.

Haya ni machache kati ya mengi niliyojifunza kwenye kitabu hichi kinachohusu mawasiliano. Weka mkazo sana kwenye mawasiliano yako, yaboreshe kila siku, watu waweze kukuelewa kwa ujumbe unaotoa na waweze kuchukua hatua.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>