Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; LITTLE RED BOOK OF SELLING (Misingi 12.5 Ya Kubobea Kwenye Mauzo.)

$
0
0
Ukweli ni kwamba, kila mtu ni muuzaji, iwe umeajiriwa, umejiajiri au unafanya biashara. Kila mtu kuna kitu anauza, kitu ambacho anawashawishi wengine wakubaliane naye. Mwajiriwa anauza ujuzi na muda wake kwa mwajiri. Mfanyabiashara anauza bidhaa na huduma zake kwa wateja. Kiongozi anauza maono na ndoto zake kwa wafuasi wake. Na mwanasiasa anauza sera zake kwa wananchi wanaomchagua.
 

Pamoja na kuuza kuwa eneo muhimu la maisha yetu, ni wachache sana wanaochukua muda na kujifunza namna ya kuwa bora kwenye mauzo. Na hata wale ambao kazi zao kuu ni mauzo, wamekuwa wanafanya kwa mazoea na hivyo kushindwa kufanikiwa.

Mwandishi Jeffrey Gitomer ambaye pia ni mtu wa mauzo (salesman) mwenye mafanikio, anatushirikisha misingi kumi na mbili na nusu ambayo kila mtu akiijua na kuifuata, basi atakuwa muuzaji (salesperson) bora sana. Kitabu hichi kimelenga zaidi kwa wale wanaofanya kazi za mauzo, lakini kinaweza kukusaidia kwenye kila eneo la maisha yako, kwa sababu misingi hii inatumika kwenye kila eneo la maisha, kazi, biashara, na hata maisha binafsi.

Jeffrey anasisitiza kitu kimoja muhimu, hakuna mtu ambaye anapenda kuuziwa, bali kila mtu anapenda kununua. Kuuziwa ni pale unaposukumwa kufanya maamuzi ya kununua. 

Kununua ni pale unapochagua wewe kufanya manunuzi, kwa sababu ni kitu unachotaka. 

Watu wengi wa mauzo wamekuwa wanaweka nguvu kuwasukuma watu kununua, na wanawapoteza. Lakini kama watawawezesha wao wenyewe waone umuhimu wa kununua, watapata wateja wengi wanaonunua.

Karibu tujifunze misingi hii kumi na mbili na nusu.

SOMA; Mauzo Ya Kilimo Cha Bustani Nje Ya Nchi Yaongezeka Kwa Asilimia 38 Mwaka Jana (2014)

MSINGI WA 1; JISUKUME WEWE MWENYEWE.

1. Chochote unachotaka kwenye maisha yako, utakipata kama utaamka na kwenda kukifanyia kazi. Hakuna mtu yeyote atakayekuletea kile unachotaka kama wewe mwenyewe hutaweka juhudi. Kila mtu anajali mambo yake zaidi ya mambo ya wengine. Watu wengi wa mauzo wamekuwa wakilalamika mauzo ni magumu, wateja hawanunui, uchumi ni mbovu, lakini ukweli ni kwamba, hakuna kitu kitakuja kama hutajisukuma mwenyewe kuweka juhudi.

2. Chochote unacholalamikia, chukua hatua. Kama mwajiri wako hakujali, tafuta mwajiri mwingine. Kama wateja ulionao sasa hawanunui, tafuta wateja wengine, au jua kwa nini hawanunui na badilika. Kama wateja hawapokei simu zako, tafuta njia nzuri zaidi ya kuwafikia. Kama kampuni yako haikupi kompyuta ya kuweza kurahisisha kazi zako, maduka yanauza kompyuta, kanunue. Kulalamika ni kupoteza muda wako, kuchukua hatua ndiyo kutakusaidia.

3. Tumia muda wako vizuri. Muda wako ni rasilimali muhimu sana, upangilie vizuri kwenye kazi zako na kujifunza pia. Na pia tumia muda ambao wenzako hawafanyi kazi kuweka juhudi zaidi. Kwa mfano watafute wateja wako kabla ya muda wa kazi kuanza, na baada ya muda wa kazi kuisha, wakati huo ni watu wachache wa mauzo kama wewe watakuwa wanatafuta wateja. Tenga muda wa kujifunza kuhusu mauzo kila siku, kadiri unavyojifunza ndivyo unavyozidi kuwa bora.

MSINGI WA 2; JIANDAE KUSHINDA AU ANAYEJIANDAA ATAKUSHINDA.

4. Fanya kazi yako. Usiende kwa mteja na kuanza kumuuliza maswali ambayo ungeweza kuyapata kwa kufanya kazi yako, kama kufuatilia taarifa zao au tovuti yao. Usimuulize mteja wako sasa hivi ananunua wapi, hilo ni jukumu lako. Ijue bidhaa au huduma yako vizuri sana na inawezaje kuwasaidia wateja wako.

5. Fanya kazi wakati wengine wamelala. Na hapa ndipo unapoweza kuwazidi wengine, kwa sababu kama hufanyi hivyo, wapo wanaofanya. Mchana fanya kazi yako ya kuwasiliana na kukutana na wateja, usiku na asubuhi sana fanya kazi ya kupata taarifa sahihi za wateja wako. Chelewa kulala na wahi kuamka, utapata muda wa ziada wa kujua zaidi na kuwafikia wateja wengi zaidi.

MSINGI WA 3; JENGA JINA LAKO, SIYO UNAMJUA NANI, BALI NANI ANAKUJUA WEWE.

6. Tengeneza jina lako, na wateja watakuwa wanakutafuta wewe, badala ya kuwatafuta wateja kwa nguvu. Jina lako linapokua, wateja wanakuthamini zaidi na kutaka kufanya biashara na wewe.

7. Zipo njia nyingi za kujenga jina lako, na kwa zama hizi ni rahisi sana.
Sajili jina lako kwenye mtandao (domain name) kama unaitwa Ali Juma, basi sajini www.alijuma.com Hakikisha mtu akitafuta jina lako kwenye mtandao anapata taarifa zako.

Kuwa na tovuti na au blog ambayo utakuwa unaandika mambo yanayoendana na biashara unayofanya. Wateja wanapotafuta suluhisho kwenye mtandao, wanakutana na wewe.
Andika makala kwenye magazeti na majarida yanayopatikana ulipo.

Tafuta nafasi ya kupata vipindi vya redio na tv, na ongea kama mtaalamu kwenye eneo lako.

Kadiri unavyojulikana na wengi kupitia kile unachofanya, ndivyo unavyowavutia wengi kufanya kazi na wewe.

8. Usishindane, bali jijengee jukwaa lako. Kwenye kujenga jina, watu wengi wamekuwa wanashindana na wengine ambao wana majina. Hilo halitakusaidia, badala yake jijengee jukwaa lako, ambapo watu watakuona wewe kama wewe.

SOMA; Siri Ya Kutambua Kampuni Nzuri Ya Kuwekeza Ili Upate Faida.

MSINGI WA 4; MUHIMU NI THAMANI NA MAHUSIANO, SIYO BEI.

9. Watu wengi wamekuwa wanafikiri kinachowafanya wateja wanunue ni bei ndogo, na hivyo kukimbilia kupunguza bei. Mwishowe wanakuwa na wateja wasio makini, na faida inakuwa ndogo na hivyo kushindwa kutoa huduma nzuri. Wateja wanasukumwa kununua na vitu viwili vikuu;

Kitu cha kwanza ni thamani, kama kweli wanaona thamani kwenye kile unachowauzia, yaani wana kihitaji, watanunua. Hivyo waoneshe watu thamani kwenye kile unachowauzia, kwa namna kitakavyowasaidia.

Kitu cha pili ni mahusiano. Kabla mteja hajanunua unachouza, anakununua wewe kwanza. 

Kwa maneno mengine, mteja anakukubali kwanza ndiyo anunue. Hivyo jenga mahusiano mazuri na wateja wako. Wateja wasikuone kama mtu unayetaka kuwauzia na kupata faida pekee, bali wakuone kama rafiki yao.

10. Ongea thamani zaidi kuliko sifa, tengeneza mahusiano pia. Watu wengi wanapopata nafasi ya kuongea na wateja, hutumia muda mwingi kuelezea sifa za bidhaa zao na kampuni zao. Hayo yote hayamhusu mteja, anachotaka kujua ni namna gani unachomuuzia kinamsaidia.

MSINGI WA 5; TENGENEZA MTANDAO WAKO.

11. Unahitaji kujenga mtandao mkubwa wa wale wanaokujua na kujua kile unachofanya. Kadiri mtandao wako unavyokuwa mkubwa ndivyo unavyoweza kupata wateja wengi zaidi.

12. Kujenga mtandao wako, jihusishe na mambo ya kijamii, hudhuria maonesho ya kibiashara, hudhuria makongamano na mafunzo ya biashara. Yote hayo ni maeneo ambayo watu wanapatikana. Pata nafasi ya kuongea na pia ongea na watu wapya, wape kadi yako ya biashara na omba kadi zao. Endeleza kukuza mahusiano kuanzia hapo.

MSINGI WA 6; HAKIKISHA UNAONGEA NA MTU MWENYE KUFANYA MAAMUZI.

13. Hakikisha unayeongea naye na kumshawishi anunue ndiye mtu wa mwisho kufanya maamuzi. Kwa sababu huyo ndiyo mtu sahihi kwako. Kama unaongea na mtu ambaye inabidi akamshawishi tena mtu wa juu yake ndiyo manunuzi yafanyike, umeshapoteza. 

Hakikisha unakutana na yule mwenye kufanya maamuzi, huyo ndiyo unayeweza kuweka juhudi zako.

14. Kama anayefanya maamuzi ya mwisho ni mgumu kumfikia, kwa sababu labda msaidizi wake anakuzuia, basi unahitaji kuweka juhudi za ziada mpaka uhakikishe unamfikia anayefanya maamuzi. Hapo utahitaji kujua maeneo yake mengine anayokuwa kama hayupo kazini, au kujua anapaki gari lake wapi na kuwahi kabla hajafika. Kuwapata watu hawa ni muhimu, kwa sababu wewe pekee ndiye unayeweza kuwaeleza na kuwashawishi na hata kujibu maswali yao kwa usahihi na wakawa tayari kununua.

Msingi wa 7; ULIZA MASWALI MAZURI.

15. Kinachowatofautisha wale wanaopata wateja wanaonunua na wale wanaoshindwa, ni aina ya maswali ambayo watu wanauliza. Ukiuliza maswali mazuri, wateja watakupa majibu mazuri na utaweza kuwauzia kile kitakachowasaidia. Ukiuliza maswali ha hovyo, mteja atakupa majibu ya hovyo na utaipoteza nafasi.

16. Maswali mazuri ni yale ambayo yanamfanya mteja aache kufikiria kile ambacho alikuwa anafikiria, na kufikiri kuhusu ulichomuuliza. Hivyo maswali lazima yawe ambayo mteja anajieleza na wewe utaweza kujua vizuri anahitaji nini. Ukiuliza maswali ya kujibu ndiyo au hapana, mteja hafikirii chochote na hutaweza kujua kwa hakika anahitaji nini, hivyo hutauza.

SOMA; Jinsi Ya Kutengeneza Biashara Isiyokutegemea Wewe Moja Kwa Moja Na Kupata Uhuru Wa Kibiashara.

MSINGI WA 8; MFANYE MTEJA ATABASAMU AU KUCHEKA.

17. Watu wengi wamekuwa wanachukulia kazi ya mauzo kama kazi ya kuwa makini muda wote, na hivyo kila wakati kuwa na sura ya umakini na kufanya yale ya kitaalamu tu. Lakini wateja ni binadamu, na mtu anapotabasamu au kucheka, basi inakuwa rahisi kwake kununua. Hivyo kuwa na namna ya kuwachekesha au kuwafurahisha watu wakati unaongea nao, kwa kucheka tu wanaweza kununua hata kama hawakuwa na mpango huo.

18. Tumia hadithi fupi za kuchekesha, lakini zisiwe za kutafsiriwa vibaya au za kuwadhihaki wengine. Tumia zaidi vitu vinavyokuhusu wewe kutengeneza hadithi hizo fupi za kuchekesha. Unapoongea na mtu au watu, unaweza kuanza na hadithi hiyo itakayowafanya wacheke na hivyo kuwafanya wakubaliane na wewe zaidi.

SIRI YA 9; TUMIA UBUNIFU KUJITOFAUTISHA NA KUTAWALA.

19. Kama unafanya kile ambacho kila mtu anafanya, hakuna atakayekuona na utapotezwa kabisa. Ila unapokuwa mbunifu na kuja na njia bora zaidi, utajitofautisha na kuweza kutawala kwenye eneo lako.

20. Ubunifu ni sayansi ambayo unaweza kujifunza, kwa kusoma vitu vingi na hata kuhoji na kudadisi kila kitu. Ipo njia nzuri ya kuchochea ubunifu, kwa njia hii, kila unachokiangalia jiulize maswali haya;

Je kingebadilishwa kingekuwaje?

Je kingeongezwa kingekuwaje?

Je kingepunguzwa kingekuwaje?

Je kingefanywa kinyume kingekuwaje?

Maswali hayo yatakufanya ufikiri tofauti na wengine na hivyo kuwa na ubunifu.

MSINGI WA 10; PUNGUZA HATARI YA WATEJA.

21. Wateja wanaweza kuwa wanasita kununua kile unachotaka kuwauzia, hata baada ya kuwapa maelezo kamili na namna kitawasaidia. Hii inatokana na kuona hatari kwenye manunuzi hayo. Labda anafikiria bei yako itakuwa kubwa kuliko maeneo mengine, au kitu kikiharibika atapata hasara, au huenda hatakihitaji sana kwenye maisha yake, au wengine watamwona amefanya maamuzi ya kijinga.

22. Kuweza kuwauzia wateja wengi zaidi, ondoa hatari yao inayowazuia kununua. Na njia ya kufanya hivyo ni kuwapa uhakika wa manunuzi hayo. Kama hatari yake ni bei basi unaweza kumwonesha wengine wanauzaje na wewe ukampa sababu zaidi za kununua kwako, hata kama ni ghali. Kama wasiwasi wake ni kupata hasara iwapo kitaharibika au kutomfaa, mpe nafasi ya kukirudisha kile alichonunua na kurejeshewa fedha zake. Kwa njia hii utauza zaidi.

MSINGI WA 11; PATA USHUHUDA WA WATEJA WAKO, UTAKUSAIDIA KUUZA.

23. Moja ya watu muhimu sana unaowasahau kwenye mauzo yako, ni wateja wakoa mbao walishanunua kwako na wakanufaika. Hawa unaweza kuwatumia kuwafikia wateja wengi zaidi. Ukiwa na ushuhuda wa wateja wako walionufaika, watu watashawishika zaidi kununua kwako. Ukiwaambia watu sifa zako wewe mwenyewe unajisifia, lakini wengine wanapowaambia watu sifa zako, huo ni ushuhuda mzuri.

24. Ushuhuda wa wateja wako unapaswa kuwa na vitu vifuatavyo;
Kueleza namna ambavyo alichonunua kilimsaidia kutatua matatizo aua changamoto zake.
Kuondoa hatari ambayo wateja wengine wanaweza kuwa nayo, kwa kusema mtu alikuwa na wasiwasi lakini alipopata alichonunua, alinufaika zaidi.

Mwisho ushuhuda uwe na himizo la mtu kuchukua hatua, mtu kununua ili naye anufaike.

MSINGI WA 12; YAJUE VIZURI MAZINGIRA YAKO.

25. Popote ulipo, yajue vizuri mazingira yako, jua vizuri kila kinachokuzunguka. Kwa njia hii utaweza kuziona fursa zaidi na hata mambo yanapobadilika, unaona kwa haraka zaidi. Jua vizuri ulipo, jua kila kinachoendelea.

26. Unapouza, hisia zako zinaweza kukusaidia au kukuzuia kuuza. Unapokuwa na hisia chanya, za kujiamini na kuwa na mategemeo chanya, mteja anahamasika kununua. Unapokuwa na hisia hasi, za hofu, kukataliwa au kutokuwa na uhakika, mteja hapati hamasa ya kununua.

MSINGI WA 12.5; JIUZULU NAFASI YAKO YA MENEJA MKUU WA DUNIA.

Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda mwingi kufuatilia mambo ambayo hayana mchango wowote kwenye kile wanachofanya. Kufuatilia habari, maisha ya wengine na mitandao ya kijamii, kunachukua muda mwingi wa watu. Huo ni muda ambao mtu ungeweza kuutumia kujiboresha zaidi kwenye kile unachofanya, kwa kujifunza na kuongoza juhudi zaidi ili kupata matokeo bora zaidi.

Jiuzulu nafasi hii ya umeneja mkuu wa dunia, siyo kwamba wewe usipofuatilia mambo yanayoendelea basi dunia itasimama. Dunia haina hata muda na wewe, kila mtu anapambana na yake, pambana na yako pia, maana hayo ndiyo muhimu zaidi kwako.

Hii ndiyo misingi 12.5 ya kukuwezesha kuwa muuzaji bora kabisa. Lakini pia unaweza kuitumia kwenye kila eneo la maisha yako na ukawa na maisha bora sana.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>