Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; Do More Great Work (Acha Kuwa Bize Na Anza Kufanya Kazi Yenye Maana)

$
0
0
Linapokuja swala la kazi, wapo watu wanaoonekana kuwa bize sana, lakini mwisho wa siku hakuna kazi kubwa wanayokamilisha. Wanaiona siku inakwisha, wamechoka kweli lakini wakiangalia walichokamilisha hawakioni. Hapa ndipo wengi wanapokata tamaa na kuona labda wao hawawezi kufanya kazi kubwa na bora.



Tatizo kubwa linalopelekea watu kushindwa kufanya kazi iliyo bora ni kukosa vipaumbele kwenye mipango yao, kutokujua kipi wafanye na kipi waache ili kuweza kupata matokeo bora. Hili ndiyo lililomsukuma mwandishi Michael Stanier kuja na njia za kutuwezesha wote kufanya kazi bora sana, kazi ambazo tuliitwa kuzifanya hapa duniani. Ametushirikisha njia hizo, ambazo ni mikakati ya kufanya kwenye kitabu chake DO MORE GREAT WORK.

Karibu kwenye uchambuzi wa leo ambapo nitakwenda kukushirikisha yale muhimu ambayo nimejifunza kwenye kitabu hichi, ambapo tukiweza kuyafanyia kazi, tutaboresha zaidi kazi zetu na kuweza kupata matokeo bora.

1. Wakati tunaoishi ni changamoto kikazi.

Tunaishi kwenye wakati ambao kufanya kazi zetu siyo rahisi. Hii inatokana na muda wetu kusongwa na mambo mengi ambayo hayana mchango kwenye kazi zetu. Tukianza na vikao mbalimbali ambavyo vinaweza kuwa vya kikazi, ila havina mchango mkubwa kwenye kazi zetu. Bado kuna mitandao ya kijamii ambayo nayo imekuwa sehemu ya maisha yetu. Bila ya kuwa makini na kujipanga vizuri utashangaa kuona siku zinakwenda na hakuna kazi kubwa ambayo mtu unakuwa umefanya.

SOMA; WHY WE WORK (Nadharia Ya Nini Kinawasukuma Watu Kufanya Kazi).

2. Aina tatu za kazi;

Kwenye kazi tunazofanya, tunaweza kuzigawa kwenye makundi matatu kulingana na namna tunavyozifanya kazi hizo.

Kundi la kwanza ni kazi mbovu. Hizi ni kazi ambazo hazina maana kwetu wala kwa yeyote yule. Ni kazi ambazo kitendo cha kuzifanya tu ni kuamua kupoteza muda, na maisha pia, kwa sababu hakuna chochote ambacho kazi hizi zinaongeza kwenye maisha yetu. Hizi ni kazi ambazo mtu unapaswa kuziacha mara moja.

Kundi la pili ni kazi nzuri. Hizi ni zile kazi zetu za kawaida, zile ambazo tunafanya kila siku na kupitia kazi hizi tunatekeleza yale majukumu ya kila siku. Ni kazi ambazo mara nyingi tunazifanya kwa mazoea na wakati mwingi wala hatuhitaji kufikiri sana. Kazi hizi hazina shida, ila hatupaswi kuweka muda wetu mwingi kwenye kazi hizi pekee, kwa sababu hazitusukumi kwenda mbele.

Kundi la tatu ni kazi bora. Hizi ni zile kazi za kipekee sana ambazo tukizifanya tunapata matokeo makubwa na ya kipekee kabisa matokeo yake yanaongeza thamani kubwa kwetu na wale wanaozitegemea. Kazi hizi siyo rahisi, na pia hazina uhakika, unahitaji kufanya mambo ambayo hujazoea kufanya, na yenye hatari ya kushindwa. Hizi ndiyo kazi zinazokufikisha kwenye mafanikio makubwa. Unahitaji kuweka muda wako kwenye kazi hizi ili kufanikiwa.

3. Uko wapi sasa?

Baada ya kujua kwamba kazi zipo za aina tatu, kila mtu atapenda kuwa kwenye kufanya kazi bora. Lakini kabla ya kufika huko, lazima ujue uko wapi kwa sasa. Lazima ujue ufanyaji wako wa kazi sasa, unakuzalishia kazi za aina gani. Kwa kujua ulipo, ndiyo unaweza kupanga kwenda mbali zaidi.

Ili kuju ulipo, angalia kazi zako unazofanya kila siku, na kwenye kila kazi jiulize je unafanya kazi mbaya, nzuri au bora. Kwa zile mbaya achana nazo kabia, zile nzuri zipangilie vizuri na zile bora zitengee muda wa kutosha.

4. Ufanisi wa nyuma, ni kielelezo kizuri cha matokeo ya mbeleni.

Katika kupanga namna unavyoweza kufanya kazi bora zaidi baadaye, angalia ufanisi wako wa nyuma. Ni wakati gani umeweza kufanya kazi bora, ulikuwa katika mazingira gani, na ulikuwa unafanya nini? Hapo ni sehemu nzuri ya kuanzia na kukupa mwanga wa wapi unaweza kufanya kazi bora zaidi.

SOMA; Kama Unatafuta Kazi, Acha Kufanya Makosa Haya Ili Kuipata Kazi Hiyo.

5. Njia mbili za kufanya kazi bora.

Zipo njia mbili za kufanya kazi iliyo bora sana.

Njia ya kwanza ni kuangalia wapi fursa zilipo na kuanza kuzifanyia kazi. Hapa unaangalia fursa mpya ambazo zitakuwezesha wewe kupiga hatua zaidi.

Njia ya pili ni kuangalia huwa unakuwaje wakati unafanya kazi bora, na kuwa hivyo mara nyingi uwezavyo. Yaani unavyokuwa unafanya kazi bora, kuna tabia za kipekee unakuwa nazo. Ukiweza kuzitengeneza tabia hizo mara kwa mara utaweza kufanya kazi bora.

6. Kuwa na kufanya.

Mara nyingi watu huwa wanakazana kufanya lakini hawawezi kufanya kazi iliyo bora. Kazi bora inaanza na kuwa kabla ya kufanya. Na njia bora ya kuwa ni kuwa na mashujaa ambao unawaangalia, wale ambao wamefanya kazi bora kwenye lile eneo unalotaka kufanya kazi bora. Unapokuwa na mashujaa hawa, unajifunza kwao na kujaribu kufanya kama wao wanavyofanya. Kwa njia hii unaweza kufanya kazi bora.

7. Shujaa wako angefanya nini?

Wakati unapopanga kufanya kazi bora, lazima utakutana na changamoto au vikwazo. Utafika wakati na kukwama usijue kipi cha kufanya. Huu ni wakati mzuri wa kuwatumia mashujaa wako. Pale unapokwama, mchukue mmoja wa mashujaa wako na jiulize je yeye angefanya nini kwenye wakati kama huo. Na kwa kuwa umeshajifunza wengi kuhusu mashujaa wako, tayari utakuwa unajua tabia zao kwenye nyakati mbalimbali na hivyo kujua kipi cha kufanya.

8. Kipi hakipo sawa?

Kile ambacho kinakuumiza pia kinaweza kukuhamasisha. Katika maisha yako, kazi na hata biashara yako, ni vitu gani unaona havipo sawa? Vitu gani vinakukera sana? Vitu hivi vinaweza kuwa sehemu nzuri ya kuanzia kwa kuvirekebisha na kuweza kufanya kazi iliyo bora. Angalia vitu vyote vinavyokuzuia wewe kufikia au kupata kile unachotaka, virekebishe na utaweza kufanya kazi bora.

9. Nini kinahitajika?

Msukumo mwingine mkubwa wa kufanya kazi bora ni kuangalia ni nini kinahitajika. Kwenye maisha yako, kazi na hata biashara, angalia kipi ambacho wewe binafsi na wengine mnahitaji. Weka juhudi kwenye kufanyia kazi kile kinachohitajika, na ukiweza kukitoa utakuwa umefanya kazi bora sana.

10. Unayojali wewe na wanayojali wao.

Kama umeajiriwa, zipo kazi ambazo wewe unazijali sana na zipo ambazo huzijali. Na pia zipo kazi ambazo mwajiri wako anazijali na zipo ambazo hazijali. Tukichanganya kazi hizi tunapata makundi manne.

Kundi la kwanza ni kazi unazojali wewe na mwajiri wako anazijali. Hizi ni kazi ambazo unapaswa kuzipa kipaumbele, kwa sababu zina manufaa kwa kila mtu.

Kundi la pili ni kazi unazojali wewe ila mwajiri hazijali. Hizi zinaweza kuwa kazi bora sana ila mwajiri wako hajazioana au kuzijua. Hivyo unahitaji kuzifanya, lakini baada ya kufanya zile za ambazo mwajiriwa anajali. Au kama ukishindwa kuzifanya hapo, unaweza kuzifanya nje ya ajira.

Kundi la tatu ni kazi ambazo wewe huzijali, lakini mwajiri anazijali. Hizi ni kazi unazofanya lakini unajua hazina maana yoyote kwako. Kwa kazi hizi unaweza kuongea na mwajiri wako ili uzipunguze kwako maana haziwezi kuzalisha kazi bora kwako.

Kundi la nne ni kazi ambazo wewe huzijali na wala mwajiri hazijali. Hizi ni kazi unazopaswa kuacha kufanya mara moja, maana zinapoteza muda wako na wa kila mtu.

11. Njia mbili za kufanya kazi usiyopenda kufanya.

Katika makundi hayo manne ya kazi kutokana na kujali kwako na kwa mwajiri wako, zipo kazi ambazo wewe huzijali, ila mwajiri wako anazijali. Kazi hizi kuzifanya wewe hakukuwezeshi kufanya kazi bora, hivyo ni bora kuwatafuta wengine wanaoweza kufanya. Kama hakuna anayeweza kufanya ila wewe tu, basi unaweza kutumia njia hizi mbili;

Njia ya kwanza ni kufanya kwa kiasi cha kutosha. Mara nyingi huwa tunakazana kuweka juhudi kubwa sana kwenye kila tunachofanya. Ila kufanya hivyo kwenye kazi ambayo huipendi, hakubadili chochote. Hivyo badala ya kuweka juhudi kubwa sana, weka juhudi ambazo zitazalisha kiasi cha kutosha.

Njia ya pili ni kutumia uvivu. Watu wavivu ni watu wenye ufanisi mkubwa sana, kwa sababu huwa wanatafuta njia rahisi na ya haraka ya kufanya mambo. Hivyo jiambie kama ungekuwa mvivu, ungewezaje kufanya kazi hiyo ambayo huipendi? Kwa njia hii utapata njia rahisi na ya haraka ya kufanya.

SOMA; Hii Ndio Kazi Inayolipa Sana Ambayo Hata Wewe Unaweza Kuifanya.

12. Njia tatu za kufanya kazi unayopenda ila mwajiri haipendi.

Katika makundi manne ya kazi tuliyoyaona hapo juu, kuna kazi ambayo wewe unapenda sana kuifanya, ila mwajiri wako haiendi. Hii ni kazi ambayo kwa kuifanya itakuwa bora na hivyo kukusaidia wewe na mwajiri wako kupiga hatua kubwa. Lakini mwajiri haitaki au haijui na hivyo anakutaka wewe ufanye kazi aliyokuajiri kufanya. Hapa unaweza kutumia njia tatu kufanya ile kazi unayopenda kufanya;

Njia ya kwanza ni kuifanya kwa chinichini. Hapa unaifanya kwa muda wako wa ziada, na hauingiliani kabisa na kazi za mwajiri wako.

Njia ya pili ni kuibadili na kuiweka kwa namna itakavyoendana na kazi anazopenda mwajiri wako. Hapa unaangalia namna gani inaingiliana na kazi zako za kawaida, na kuichanganya kwenye kazi hizo.

Njia ya tatu ni kuifanya kazi hiyo mahali pengine. Kama ulipo sasa huwezi kabisa kuifanya, na ni kazi ambayo unaijali sana na kuweza kuwa bora, unaweza kutafuta sehemu nyingine ambapo utaweza kuifanya. Iwe ni kwa kuajiriwa au kujiajiri mwenyewe.

13. Chagua kipi unachokwenda kufanya.

Katika kutathmini kazi bora, yapo mengi sana ambayo unaweza kufanya na muda wako. Wakati mwingine unashindwa kujua uanzie wapi. Hapa ni muhimu uchague kile ambacho utakwenda kufanya, kulingana na umuhimu wake na mahitaji yako pia. Bila ya kuchagua, hutaweza kupiga hatua kwa sababu kila mara utakuwa na mengi ya kufanya.

14. Usiogope kukosea kuchagua.

Kinachowafanya wengi kushindwa kuchagua, ni kuogopa kukosea kuchagua. Kutokana na mengi ambayo watu wanaweza kufanya, wanapata wakati mgumu kipi wachague kufanya na kuacha mengine yote. Kuondokana na hofu hii, kumbuka kwamba huhitaji kuwa mkamilifu, badala yake unahitaji kufanya na kuboresha. Hivyo chagua pale unapoweza kuanzia sasa na anza. Mbeleni utagundua kuna mambo hukuzingatia na utaendelea kuyaboresha zaidi.

15. Ruhusu mawazo ya nje.

Mara nyingi watu hushindwa kufanya kazi bora kwa sababu wanakosa mawazo mapya. 

Wanaendelea kutumia mawazo yale yale waliyozoea kuwa nayo kila siku. Wanaona mawazo ya nje hayawafai wao, hivyo kwa mawazo yao hayo wanaendelea kufanya kile ambacho wamezoea kufanya.

Ili kuweza kufanya vitu vya tofauti unahitaji kuwa na mawazo tofauti na uliyozoea kuwa nayo. Unahitaji kuruhusu mawazo ya nje ili uweze kufanya mambo tofauti.
Jinsi ya kuruhusu mawazo ya nje, chukua tatizo aua changamoto yako, na tembelea maduka ya jumla huku ukiangalia namna bidhaa zimepangwa, bidhaa zilizopo na namna watu wanachagua. Kwa kuangalia hivi, utapata mawazo yanayoweza kuendana na kile unachotaka kufanya.

16. Fikiri na tenda tofauti.

Ili kufanya kazi iliyo bora, unahitaji kufikiri na kutenda tofauti na unavyofanya kazi ya kawaida. Kwa sababu miili yetu huwa inafanya mambo kwa mazoea, unavyofikiri na kutenda, ndivyo unavyofanya. Hivyo namna unavyoichukulia kazi, pale unapofanyia kazi, kote kunaleta kazi ya kawaida.

Kufanya kazi bora, fikiria tofauti kabisa na unavyofikiria ukiwa unafanya kazi zako, na tenda tofauti kabisa. Moja ya njia z akutenda tofauti, ni kuchagua sehemu tofauti ya kufanyia kazi bora. kwa mfano ofisini unaweza kuwa na meza mbili, meza moja ya kazi za kawaida, na meza nyingine ya kazi bora. unapofika kwenye meza ya kazi bora, akili yako inajiandaa kabisa kufanya kazi bora.

17. Changamoto ya kuanza kitu kipya.

Ili kufanya kazi bora, unahitaji kufanya vitu vipya, vitu ambavyo hujazoea kufanya. Ila kufanya huku vitu vipya kuna changamoto zake. Changamoto hizi ndiyo zinawazuia wengi kufanya na hivyo kuendelea kufanya waliyozoea kufanya na kuishia kufanya kazi za kawaida.

Changamoto kubwa ni kukosea kwa sababu ni kitu kipya, ambacho hujazoea kufanya. Wengi hawapendi kukosea.

Changamoto nyingine ni kupingwa na wengine kwa kile unachofanya. kwa sababu unapofanya mambo mapya, kuna ambao wataathirika, na hawatakuachia kirahisi. Wataibuka kukupinga na wengine kukukosoa au kukukatisha tamaa.

Unahitaji kujitoa na kuwa tayari kushindwa na kupingwa ili uweze kufanya mambo mapya na kuweza kufanya kazi bora.

18. Haraka ya kufanya inakuzuia kufanya kazi bora.

Kwenye maeneo mengi ya kazi, watu hukimbilia kufanya kazi mara moja kabla hata hawajaitafakari vizuri. Pia watu wanafanya kazi kwa haraka kwa sababu kufanya kunaonekana kama ndiyo uzalishaji. Lakini mara nyingi kufanya kwa haraka kunazalisha kazi ambayo ni ya hovyo au ya kawaida.
Ili kufanya kazi bora, unahitaji kuitafakari kazi kabla ya kuifanya, kujua kama kweli ni muhimu kwako na maeneo yapi muhimu kuanzia. Pia unapofanya, usifanye ili kuonekana unafanya, bali fanya kwa sababu ni muhimu kufanya.

19. Usiangalie matokeo, angalia uzuri wa kazi.

Kitu kingine ambacho tunasukumwa kufanya ni kupima kazi zetu kwa matokeo tunayopata. 
Tunaangalia kiasi gani tumezalisha kwa muda gani na gharama gani. Hii ni msukumo hasa kwa wale ambao wanataka kufanya kazi za kawaida. Ila kwenye kufanya kazi bora, matokeo hayapaswi kuwa msukumo, bali uzuri wa kazi. Mchakato mzima wa kazi una mchango mkubwa kwenye kuzalisha kazi bora. Pale ambapo mtu anapenda na kufurahia kila hatua ya kazi anayopiga, anaweza kufanya makubwa zaidi. Lakini yule anayeangalia matokeo pekee, ataishia kufanya kazi ya kawaida ili tu kupata matokeo.

20. Wote tunahitaji msaada.

Hakuna mtu anayeweza kufanya kila kitu yeye mwenyewe. Na kwenye kufanya kazi bora, hakuna mtu anayeweza kufanya kazi bora peke yake. Unahitaji msaada wa watu wengi sana ili kuweza kukamilisha kazi bora. Unahitaji utaalamu wa wengine, ushauri na hata rasilimali ambazo wewe huna. Bila ya msaada wa wengine, huwezi kufanya kazi bora.

21. Maeneo matatu ya kuangalia msaada.

Eneo la kwanza ni kwa watu wanaokupenda, hawa ni ndugu jamaa na marafiki. Hawa watakusaidia kukutia moyo na hata kwa mengine yaliyopo ndani ya uwezo wao.

Eneo la pili ni wenye utaalamu. Hawa ni watu ambao wanaweza kufanya yale muhimu unayohitaji ila huwezi kuyafanya wewe mwenyewe.

Eneo la tatu ni watu wenye ushawishi, hawa watakutambulisha wewe kwa watu wanaoweza kukusaidia zaidi.
Unahitaji watu kutoka maeneo hayo matatu ili kuweza kufanya kazi bora.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>