Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; Winning Arguments (Mbinu Za Kushinda Majadiliano Kwa Hoja).

$
0
0
Moja ya sifa yetu binadamu ni kwamba, hakuna kitu kimoja ambacho wote kwa pamoja tunaweza kukubaliana. Kwenye jambo lolote lile, lazima kutakuwa na pande mbili, upande unaokubali na kuona ni sahihi, na pia upande unaokataa na kuona siyo sahihi. Haya yapo wazi kwenye dini, siasa na hata tamaduni za maisha yetu ya kila siku.
 

Hata kwa mambo ambayo tunaweza kuona ni ya kawaida kabisa, zinaweza kuibuka hoja za kufanya isionekane kawaida kama ilivyo. Kwa mfano kumtesa mtu ni kinyume kabisa na haki za binadamu, na haikubaliki kwenye utawala wa sheria. Lakini vipi iwapo mtu ameweka mabomu ambayo yatalipuka na kuua watu, lakini hataki kusema mabomu yapo wapi? Je kumtesa mpaka aseme ni sahihi? Kwa haraka unaweza kusema ni sahihi, lakini wapo watakaokuambia una uhakika gani ni kweli yeye anahusika? Kwa nini usitumie njia nyingine kupata bila ya kutesa? Na muhimu zaidi akishateswa mmoja, kutesa kutaonekana ni njia sahihi kutumia.

Katika hali kama hizi tunawezaje kushinda ubishi na majadiliano ambayo tunajikuta tumeingia? Mwandishi Stanley Fish anatupa mbinu za kushinda ubishani na majadiliano kwenye kitabu chake WINNING ARGUMENTS. Karibu tujifunze kwa pamoja ili tuweze kujua asili ya mabishano na namna ya kuyashinda.

1. Ukweli (fact) na maoni (opinion) ni vitu ambavyo havina uhalisia kwenye mabishano au mjadala. Kila upande unashikilia wanachosema wao ndiyo ukweli na wanachosema upande wa pili ni maoni. Hivyo kuchukua kile mtu anachosema ni ukweli kwa sababu anapingana na mwingine, ni kubeba uongo. Kujua ukweli hasa, inabidi uondoke kwenye mtazamo wa kubishana na uingie kwenye mtazamo wa kujifunza.

SOMA; Hizi Ndizo Aina Tatu (3) Za Kushindwa Katika Maisha Na Kazi.

2. Kinachowafanya watu wanaingia kwenye mabishano au malumbano mara nyingi siyo hoja wanazobishania bali mitazamo ambayo ipo ndani yao, namna ambavyo wamezoea mambo yalivyo. Wapo watu wanaweza kukataa jambo siyo kwa sababu wanalielewa vizuri, bali kwa sababu haliendani na vile wanavyojua au kuamini wao kwa muda mrefu.

3. Sisi kama binadamu, tuna ukomo sana kwenye kuuona ukweli, mara nyingi hatuoni au kufikia ukweli, kwa sababu kila tunachokiona tunakihukumu kulingana na mitazamo yetu binafsi. Hivyo tunaona vitu siyo kama vilivyo, bali kama tunavyotaka kuviona. Hivyo wanapokutana watu wawili ambao wana mitazamo tofauti, ni vigumu sana kuweza kuafikiana, kwa sababu kila mtu anaona kile anachotaka kuona.

4. Kitu kimoja ambacho lazima tukubaliane kabla hatujaendelea kujadili kuhusu ubishani na malumbano ni kwamba, hatuwezi kudhibiti na kufuta kabisa malumbano. Kwa sababu kama tulivyoona, watu hawawezi kuwa na mtazamo mmoja wote. Mfano mzuri ni kwenye siasa, wakati wa uchaguzi, huwa zinatokea pande mbili kuu, kila upande ukimnadi mgombea wao na kumkosoa mgombea wa upande mwingine. Tunategemea baada ya uchaguzi malumbano hayo yaishe kabisa, lakini huwa hayaishi, bali hoja tu ndiyo zinabadilika. Hoja zinahamia kwenye utendaji wa yule aliyeshinda, kwenye kama anatekeleza ahadi au la, na mengine mengi. Hivyo kwa namna yoyote ile, tusijidanganye kuwa kuna wakati wote tutakubaliana.

5. Aristotle anasema kwamba ili hoja iweze kuwashawishi watu, inahitaji kuwa na vitu vitatu;

Kitu cha kwanza ni mantiki ya hoja (logos) hii ni ile dhana ambayo hoja imebeba, ule unaoweza kuwa ukweli au maoni ya hoja husika.

Kitu cha pili ni maadili ya mtu anayetoa hoja husika (ethos), hapa tabia na maadili ya mtu anayetoa hoja, inaweza kushawishi watu kukubali au kukataa.

Kitu cha tatu ni hisia ambazo mtoa hoja anakuwa ameziweka kwenye hoja yake (pathos) , hapa wengi hutumia hofu au tamaa kuwafanya watu waamini kile wanachosema.

Hivyo kama unataka kutoa hoja yenye ushawishi na itakayokuwezesha kushinda, japo kwa muda, zingatia vitu hivyo vitatu.

6. Katika kujipanga ili kutoa hoja zenye ushawishi, lazima ujue ni aina gani ya mabishano au malumbano unayokumbana nayo. Kwenye kitabu hichi, malumbano yamegawanyika kwenye makundi ya malumbano ya kisiasa, malumbano ya kindoa, malumbano ya kielimu na malumbano ya kisheria. Kila eneo lina taratibu zake za kulumbana, kutotumia taratibu za eneo husika kunaweza kukupelekea wewe kushindwa. Kwa mfano malumbano ya kwenye siasa yanaruhusu watu kudhalilishana, lakini huwezi kufanya hivyo kwenye malumbano ya kielimu au kindoa.

SOMA; Kuboresha Maisha Yako Anza Kwa Kufanya Hivi.

7. Malumbano yangekuwa rahisi na yenye mwisho iwapo kutolewa kwa ushahidi kungekubalika na pande mbili zinazolumbana. Lakini hilo halitokei kwa sababu ushahidi unapoletwa, malumbano yanahamia kwenye ushahidi huo, iwapo ni ushahidi wa kweli au la, iwapo unafaa au haufai. Ushahidi unaweza kutuliza mambo kwa muda, lakini baadaye malumbano yanaweza kuibuka tena pale watu wanapokuja na ushahidi unaopinga ushahidi wa mwanzo.

8. Njia rahisi ya kumaliza malumbano, ambayo ilitumika zamani ilikuwa kutumia nguvu ya mamlaka fulani. Kwamba hii ni mamlaka na inasema hivi. Mfano sheria ya nchi inasema hivi, au kanisa linasema hivi, au kitabu cha dini kinasema hivi. Lakini sasa hivi kila mamlaka inahojiwa, sheria za nchi zinahojiwa na hata kupambanuliwa kama kweli zinamaanisha kile ambacho watu wanaelewa. Kadhalika mamlaka za dini zinahojiwa kila wakati, na haya kufikia hatua ya watu kuhama dini au kuanzisha dini zao. Hivyo kutumia mamlaka kumaliza malumbano, haiwezekani.

9. Malumbano na mabishano kwenye uwanja wa siasa ni mabishano makali sana. Kwa sababu haya hayana msamaha, maneno makali yanaweza kutolewa. Pande mbili hushutumiana kwa uhalifu, uongo, usaliti, udhaifu na mengine mengi. Hivyo kushinda kwenye malumbano ya kisiasa, lazima uweze kuvumilia shutuma zinazotumwa kwako, na kuonesha shutuma za wengine.

10. Mfano mzuri wa mtu aliyeweza kuwashangaza watu kwenye kushinda malumbano ni Raisi wa Marekani, Donald Trump, wakati wa kampeni kila mtu alimshangaa, kila mtu alisema hatafika mbali. Kwa sababu hakuwa na hoja kubwa anazozungumza, wala mikakati mikubwa, lakini aliweza kuwashinda wengine wengi kuanzia kwenye chama chake na uchaguzi mkuu kwa ujumla. Yeye alijua kitu kimoja ambacho anaweza kukisimamia, na kukisema hicho mara zote. Alichosimamia ilikuwa ni kwamba yeye siyo mwanasiasa, hivyo hana muda wa kudanganya, kama watu wanataka kuendelea kudanganywa na wanasiasa, waendelee kuwasikilia. Ameweza kushinda kwa muda, lakini bado malumbano yanaendelea kuhusu uraisi wake.

11. Kuna wakati ambapo malumbano yanaisha pale ambapo upande mmoja unaona kile ambacho hawakuwa wanakiona kwa kipindi chote cha malumbano. Hapa ni pale unapotolewa ushahidi ambao hauwezi kupinga kwa namna yoyote ile. Hivyo unapokuwa kwenye malumbano, angalia ni kitu gani ambacho wengine hawakioni, na waoneshe, inaweza kukusaidia mkaanza kufikiria kwa upande mmoja.

Mwandishi anatoa mfano wa hadithi ambapo kijana alipelekwa mahakamani kwa kosa la kumuua baba yake. Mwanamke ambaye ni jirani alitoa ushahidi kwamba alisikia wakilumbana na mtoto akamwambia baba yake nitakuua, baada ya muda baba akakutwa amekufa kwa kuchomwa kisu. Majaji 11 kati ya kumi na mbili walisema kijana ana hatia na iko wazi, ila mmoja alisema hana hatia. Kila mtu alimshangaa kwamba amekosa utu, anakataaje kesi ambayo iko wazi kabisa. Ndipo alipowapa ushahidi ambao haupingiki, kwa mfano baba anaonekana amechomwa kisu kutoka juu, lakini mtoto ni mfupi kuliko baba, hivyo asingeweza kumchoma kisu kwa namna hiyo. Pia kwa kuangalia mwanamke aliyetoa ushahidi anavaa miwani, na wakati anashuhudia hayo ilikuwa usiku, hivyo ni dhahiri hakuwa anaona vizuri. Baada ya ushahidi huu na mwingine uliotolewa, wengi walibadilika na kusema kijana hana hatia.

SOMA; Tumia Kanuni Hizi Tatu(3) Za Muhimu Sana Ili Uweze Kumfanya Mteja Asikukimbie Kwenye Biashara Yako

12. Wakati mwingine, malumbano hasa ya kisiasa, huwa yanashindwa kwa sababu wakati wake unakuwa bado haujafika. Kuna pande zinashindwa kwa sababu hoja wanazotetea haziendani na nyakati ambazo wanaishi, lakini baadaye hoja hizo huja kukubalika na kutumika.

13. Njia nyingine ambayo inaweza kumaliza malumbano kwenye hoja fulani, ni kwa watu kubadilika kutoka kwenye msimamo wao wa awali. Kama ambavyo tumeona, kitu ambacho kinapelekea malumbano siyo hoja husika, bali imani na mtazamo wa watu juu ya jambo husika. Pale mtu anapobadili msimamo wake, hawezi kuendelea tena kulumbana. Hivyo kama unaweza kuwashawishi watu wakabadili misimamo yao kwanza, malumbano hayatachukua muda.

14. Kinachoamua kama malumbano yatachukua muda mrefu au mfupi, ni idadi ya vitu ambavyo ni vya uhakika katika hoja zinazotolewa. Kadiri vitu vingi vinavyokuwa vya uhakika, malumbano yanakosa nguvu. Lakini kama vitu siyo vya uhakika, malumbano yanahamia kwenye vile vitu ambavyo siyo vya uhakika.

15. Kitu kimoja kinachokosekana kwetu binadamu ni kwamba hakuna kitu kimoja kinachokubalika na watu wote duniani. Hakuna fedha moja inayotumika na kila mtu duniani, hakuna dini moja inayoaminiwa na kila mtu, hakuna utamaduni mmoja unaokubalika na kila mtu. Hivyo malumbano yanaendelea mpaka pale watu wengi zaidi wanapokubaliana na kitu kimoja.

16. Kuna makundi makuu mawili ya watu, kuna wale wanaoamini kwenye mfumo na wale wasioamini kwenye mfumo. Wanaoamini kwenye mfumo wanaoamini kwamba mabadiliko yanatokana na kupiga hatua kutoka chini kwenda juu. Wasioamini kwenye mfumo wanaamini kwamba mabadiliko yanatokea pale jamii inapoamua kubadilika kulingana na hali zinazokuwepo. Katika malumbano mengi, wapo watu wa misimamo ya pande hizo mbili.

17. Malumbano kwenye mahusiano ya ndoa ni moja ya malumbano ambayo kila mtu anapaswa kuyajua vizuri na namna ya kwenda nayo. Kwa sababu malumbano haya yanaingiza na hisia pia, ni rahisi sana kuumiza hisia za mwenzako kwa maneno unayotoa kwenye malumbano. Hivyo kujua wakati gani wa kusema na wakati gani wa kusikiliza, ni muhimu. Ndoa ambayo majuto, kushutumiana na kukosoana vimetawala, ni ndoa inayokuwa na matatizo kila siku.

Zipo sheria tano za malumbano ya ndani ya ndoa.

18. Sheria ya kwanza; malumbano yanatokana na haiba ambazo watu wanakuwa wamejitengenezea wenyewe. Kama tulivyojifunza, mara nyingi malumbano siyo kwenye hoja, bali kwenye mitazamo au misimamo ya watu. Kwenye ndoa pia, malumbano yanatokana na haiba ambazo watu wanakuwa wamejitengenezea, au namna wanavyokuwa wanawachukulia wengine wanawachukuliaje. Kwa mfano mtu anaweza kusema ameniambia hivi kwa sababu ananidharau, kumbe hata hakuna dharau yoyote imetumika, ni vile ambavyo amechukulia yeye.

19. Sheria ya pili; malumbano kwenye ndoa hayana mwanzo unaojulikana, na mpaka unakuja kujua mpo kwenye malumbano, umeshachelewa. Malumbano ya ndani ya ndoa huwa hayajulikani yalianzaje, mnajikuta tayari mnalimbana tena kwa jambo ambalo huenda ni dogo sana.

20. Sheria ya tatu; malumbano siyo kwenye jambo linaloonekana, bali kwa mambo yaliyofichika. Wanandoa wanajikuta kwenye malumbano, lakini siyo juu ya kile ambacho wanalumbana, bali juu ya kile ambacho kipo ndani yao. Wanaume wanaumizwa sana na kuaibishwa, hivyo kama lipo jambo ambalo mke wake amefanya na linamwaibisha litamuumiza. Wanawake wanaumizwa na hofu, hofu ya kuachwa au kuwa kwenye wakati mgumu. Hivyo wanandoa wanaweza kuwa wanabishana kwa jambo dogo, kumbe chini wana maumivu yao yanayowafanya waendelee kulumbana.

21. Sheria ya nne; kujaribu kufafanua ulichosema na kusababisha malumbano, kunaweza kusababisha malumbano zaidi. Kwenye malumbano ndani ya ndoa, unaweza kusema kitu fulani kwa nia nzuri, ila mwenzako akaelewa vibaya na kutafsiri tofauti. Kitu utakachokimbilia kufanya ni kujaribu kufafanua, na hapo ndiyo unaweza kuharibu mambo zaidi. Ukishakosea kusema na mwenzako akatafsiri vibaya, usiendelee kufafanua, badala yake sikiliza anasema nini, mwelewe ili muweze kufikia makubaliano.

22. Sheria ya tano; kujua sheria hizi za malumbano ndani ya ndoa, hakukuzuii wewe kuingia kwenye malumbano ndani ya ndoa yako. Kwa sababu licha ya kuzijua, bado kuna wakati utapatwa hasira au jambo litakukera na kujikuta umesema kitu ambacho kimemuumiza mwenzako. Hivyo kuzijua ni hatua moja, kuweza kuziishi inategemea zaidi uzoefu na kuendelea kujifunza.

Malumbano ni sehemu ya maisha yetu, hatuwezi kuyakimbia malumbano, hivyo tunahitaji kujua njia bora ya kwenda nayo. Tumia haya uliyojifunza hapa kwenye malumbano mbalimbali unayojikuta umeingia kwenye maisha yako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>