Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

USHAURI; Jinsi Unavyoweza Kukamilisha Mipango Yako Licha Ya Kuwa Na Changamoto Nyingi.

$
0
0
Karibu tena rafiki yangu kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto ambazo zinatuzuia kufikia mipango yetu na mafanikio kwenye maisha. Kwa kuwa changamoto ni sehemu ya maisha, hapa hatujifunzi kuzikimbia, bali kupambana nazo ili tuweze kuzivuka na kufanikiwa.
 

Leo nataka nikuulize swali moja, hivi umewahi kuona kama vile ukiwa na fedha dunia inataka kukunyang’anya fedha hizo? Yaani ukiwa huna fedha, wala hakuna anayekusumbua, lakini ukishakuwa tu na fedha, basi matatizo ya kila aina yataibuka. Hata watu ambao walikuwa hawajawasiliana na wewe miaka mingi, watawasiliana na wewe na kukupa matatizo yao, ambayo utaona yanafaa kabisa kusaidiwa. Unawasaidia wengi uwezavyo, fedha zinaisha na mipango yako unakuwa hujaifanyia kazi!

Hii ni moja ya changamoto inayosumbua watu wengi na kuwarudisha nyuma, hasa vijana wengi wanaotokea familia masikini na wao kuwa ndiyo wamepiga hatua. Wanakuwa na watu wengi nyuma yao ambao wakiwa na shida yoyote, wanajua wa kuwasaidia ni mtu huyo pekee. Licha ya changamoto kama hizi, bado ni lazima wewe ufanikiwe, na mipango yako itimie. Hili ndiyo tutakwenda kupata ushauri kwa leo. Lakini kabla ya kujua nini cha kufanya, tusome kwanza maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia juu ya hili;

SOMA; Changamoto Ya Wategemezi Wengi Na Changamoto Ya Kipato Kuwa Sawa Na Matumizi.

Nidhamu binafsi imekuwa shida kwangu. Kila nikipanga kufanya kitu nashindwa kukikamisha ipasavyo, Ukweli ni kwamba nina majukumu mengi sana na yote yanisubiri, sasa najikuta nafanya hili kisha naacha, nafanya lile najikuta tena nimeishia njiani, majukumu mazito pia yanazaliwa kwangu kila kukicha. kwa mfano kama nimepanga, kukusanya fedha ili nianzishe mradi au biashara ghafla linajitokeza jukumu zito ambalo linanihusu mimi 90% sasa najikuta tena ile pesa niliyotenga nimeitumia kutatua jukumu lile. Sasa hii naona ni changamoto kwangu naomba kushauriwa tafadhali. Edger Y. P.

Tumesoma wote changamoto hii ya Edger ambayo naamini sehemu kubwa ya watu wanaosoma hapa pia wanapitia changamoto ya aina hii. Unapanga mambo yako vizuri, lakini fedha zinapofika, matatizo nayo yanabisha hodi, na unajikuta ukitumia fedha zote na kushindwa kutimiza mipango yako.

Sasa twende tukaangalie namna gani ya kuweza kutatua changamoto hii, ili uweze kutekeleza majukumu yako kwa wale wanaokutegemea, na pia uweze kutekeleza mipango yako mikubwa ya maisha.

Hatua ya kwanza; pitia majukumu yako yote, na chagua yale ambayo utawajibika moja kwa moja.

Haijalishi una mizigo mingi kiasi gani kwenye maisha yako, kama ikitokea unakufa leo, hakuna mzigo hata mmoja ambao utaondoka nao. Na hata wale wanaokutegemea wewe moja kwa moja, hawatakufa na wewe. Hii ni kutaka kukuonesha ya kwamba, unahitaji kuwajibika na mizigo yako na wale wanaokutegemea pia, lakini isiwe kikwazo chako kuwa na maisha.

Hivyo hatua ya kwanza kabisa kwako kuchukua ni kupitia majukumu yako yote, pitia mahitaji ya wale wote ambao wanakutegemea wewe moja kwa moja. Kwa kila jukumu na hitaji, angalia lipi ni muhimu kabisa ambalo linakuhitaji wewe moja kwa moja ulifanyie kazi. 

Angalia yapi ambayo yanaweza kufanywa na wengine, na angalia yapi ambayo yanaweza kusubiri kwa kuwa siyo dharura na wala siyo haraka.

SOMA; Hii Ndio Changamoto Kubwa Inayokuzuia Wewe Kutatua Changamoto Zako.

Kama ni wazazi na ndugu wanaokutegemea, kama wapo ambao wana uwezo wa kujishughulisha, wape njia wanazoweza kujishughulisha nao pia, ili kupunguza utegemezi usio wa lazima. Kwa zoezi hili, utabaki na yale majukumu muhimu sana, ambayo siyo nje ya chakula, afya na elimu. Usije ukaniambia moja ya majukumu yanayokusubiri ni michango ya harusi au kuandaa sherehe sijui za nini. Hayo futa kabisa, kama uwezo wako hauruhusu usilazimishe, muhimu ni kuhakikisha mahitaji ya msingi kabisa ya kuwawezesha watu waendelee kuishi yanafikiwa.

Kwa zoezi hili utapunguza mzigo mkubwa sana, nakuambia hilo kwa sababu kwa jamii zetu, watu wakishajua fulani anaweza kutusaidia, basi kila aina ya shida watakayopata hawatafikiria mara mbili, bali wataileta moja kwa moja kwako. Sasa unapoweka vigezo vya mambo gani unaweza kusaidia kwa kipindi ambacho bado wewe mwenyewe hujakaa vizuri, watu watajifunza kuja kwako kwa yale ambayo ni muhimu zaidi.

Hatua ya pili; kabla hujaanza kufanya jambo, lijue mpaka mwisho, na gawa majukumu madogo madogo ya kukamilisha.

Tabia ya kuanza mambo na kuachia njiani, kuanza mengine na kuachia njiani pia inatokana na kuanza mambo bila ya kujipanga vizuri. Wala haihusiani na kuwa na majukumu mengi au kipato. Kwa sababu kabla hujaanza jambo lolote, lazima uwe umeshaliona mpaka mwisho wake, umeshajua utafikaje pale, na pia kujipanga kwa tahadhari zozote. Usipate tu wazo, au kuambiwa tu kitu na kukimbilia kufanya, lazima ufanye tathmini, wewe mwenyewe unajijua hivyo lazima ujiangalie kwanza.

Kingine muhimu ni kutokuanza mambo mengi kwa wakati mmoja. Anza jambo moja kwa wakati, na nenda nalo mpaka mwisho wake, kabla ya kuanza jambo jingine. Ni bora kufanya mambo mawili na kuyakamilisha, kuliko kufanya mambo kumi na yote ukaishia njiani.

Anza yale ambayo unaona unaweza kumaliza, na kama huwezi subiri. Anza jambo moja kwa wakati, weka juhudi zako mpaka uone matokeo yake.

SOMA; Biashara Rahisi Kufanya, Ambayo Haina Changamoto Na Faida Ni Kubwa.

Hatua ya tatu; weka fedha zako kwenye eneo ambalo huwezi kuzipata kwa haraka.

Ukisema unakusanya mtaji kwa kuweka fedha benki, niamini, hutafikisha huo mtaji, kwa sababu utakapopata shida kidogo, ni rahisi kwenda benki na kutoa fedha ili kutatua shida ile. 

Lakini inapotokea tatizo na huna fedha benki, inakulazimisha wewe kufikiria njia nyingine za kulitatua. Kwa sababu hii, hakikisha hukai na fedha za mipango ya baadaye benki, badala yake ziweke kwenye maeneo ambayo huwezi kuzipata haraka.

Unaweza kuwekeza fedha yako kwenye maeneo ambayo siyo rahisi kuzitoa lakini pia haitakuchukua muda mrefu sana kuzitoa. Hivyo unaweza kuweka kwenye akaunti ya muda maalumu, yaani fixed deposit ambapo huwezi kutoa kwa kipindi fulani ambacho utaeleza, labda miezi mitatu, sita, tisa au mwaka. Pia unaweza kuwekeza kwa kununua hisa na vipande, ambapo uuzaji wake hauchukui muda mrefu sana kama uwekezaji wa maeneo kama ya majengo na ardhi.

Fedha unayopaswa kubaki nayo wewe ni ile ya matumizi yako, na ile ya dharura, iwapo lolote litatokea. Akiba nyingine, ziweke kwenye maeneo hayo.

Hatua ya nne; jilipe wewe kwanza, kabla hata hujaanza kutumia kipato chako.

Huenda hatua hiyo ya tatu ikakushinda kwa sababu labda hufanikiwi hata kufikisha kiasi cha kuweza kuwekeza, kutokana na matatizo yanayokuwa yanakuandama mara kwa mara. Sasa hapo cha kufanya ni hichi, kila unapopata kipato chako, ondoa sehemu fulani ya kipato hicho, labda asilimia 10, au hata chini ya hapo, na iweke mbali kabisa. Chukulia kama ulinunua kitu na hivyo huwezi kuipata tena. Tumia ile iliyobaki kwenye matumizi yako na wategemezi wako. Usikubali kabisa kipato chako chote kitumike kwenye matumizi, hata kama una matatizo kiasi gani, weka pembeni hata elfu kumi, haitakuwa sawa na bure.

Hatua ya tano; pambana zaidi, weka juhudi zaidi, teseka zaidi kwa muda mfupi kupunguza hayo ya sasa.

Pamoja na kufanya hayo hapo juu, kwa kuwa unajua matatizo yako ni yapi, unahitaji kuongeza kipato chako mara dufu. Kwa sababu hata kama utapunguza matumizi na yale ya wategemezi, itafika hatua huwezi kupunguza zaidi, watu lazima wale, na afya lazima zilindwe iwapo magonjwa yanatokea. Hivyo kilichobaki hapo ni wewe kutafuta njia zaidi za kuongeza kipato chako. Kama umeajiriwa anza biashara ya pembeni. Kama huwezi kuanza biashara kwa sababu yoyote, tafuta kitu unachoweza kufanya kwa muda wako wa ziada ili ulipwe zaidi.

Usiniambie una matatizo yote hayo halafu unaenda kazini asubuhi, unarudi jioni na kusubiri tena mpaka kesho, na jumamosi na jumapili na wewe unajiambia una weekend. Wewe unahitaji kupambana hasa, unahitaji ukitoka kazini upite sehemu nyingine ya kukuwezesha kuongeza kipato zaidi. Jumamosi na jumapili zinapaswa kuwa siku nzuri sana kwako. 

Pambana, fanya kile ambacho unaweza kufanya, halali lakini, ili uweze kuongeza kipato chako, hata kama ni kwa kiasi kidogo sana. Wewe huna anasa ya kupumzika na kustarehe kwa sasa, unahitaji kuweka juhudi ili kuweza kutoka hapo ulipo.

Hizo ni hatua tano ambazo namshauri Edger na wengine wanaopitia changamoto ya aina hiyo kuchukua ili waweze kutoka pale walipo sasa. Najua baadhi ya mambo niliyoshauri yanaweza kuonekana magumu au kujitesa, lakini ni bora uchukue hatua sasa, kabla maisha hayajaendelea kukutesa zaidi.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>