Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Barua Ya Wazi Kwa Waalimu Wa Sanaa Na Kada Nyingine Zilizokosa Kipaumbele Kwenye Ajira Za Serikali. ( Kama Umesoma Na Huna Ajira, Pia Soma Hapa.)

$
0
0
Habari za leo rafiki yangu,

Karibu kwenye barua ya leo ya wazi, ambapo kupitia barua hizi za wazi nakwenda kuzungumza na watu mbalimbali kuhusu hali wanazopitia na namna wanaweza kufanya maisha yao kuwa bora zaidi.
 

Leo nakwenda kuongea na walimu wa masomo ya sanaa na watu wa kada nyingine ambazo hazijapewa kipaumbele kwenye ajira za serikali. Kumekuwepo na malalamiko baada ya serikali kutangaza kwamba itaajiri walimu wa sayansi na hisabati pekee. Hii imepelekea walimu wa masomo ya sanaa kuuliza wao hatima yao vipi kwenye ajira? Hakuna anayewajibu moja kwa moja, ila mimi rafiki yenu, nachukua nafasi hii kuwapa njia mbadala za kuchukua ili kuhakikisha maisha yenu yanakuwa bora kabisa.

Karibu kwenye barua hii ya leo, jifunze na chukua hatua.

Kwako rafiki yangu ambaye umesoma na kuhitimu lakini bado hujapata ajira.

Wakati nipo kidato cha sita, nilijiambia hivi, nitasoma kwa bidii sana nipate daraja la kwanza, kwa sababu kipindi kile mikopo ya elimu ya chuo kikuu ilitolewa kwa wenye daraja la kwanza pekee. Na pia nilijiambia nitasoma sana nifaulu, na utakapofika wakati wa kuomba chuo kikuu nitajaza kozi mbili tu, ya kwanza ni udaktari kama matokeo yatakuwa mazuri kabisa. Na ya pili ni ualimu kama matokeo hayatatosha kusoma udaktari. Nilijiambia hivyo kwa sababu kwa enzi zile, udaktari na ualimu pekee ndiyo vilikuwa vimebaki kuwa na ajira za uhakika serikalini. Yaani ulikuwa unamaliza tu chuo ukiwa na uhakika wa ajira, na hata hivyo bado ungeweza kuamua kutokwenda kwenye ajira ya serikali kama ulipopangiwa hujapapenda na ukapata nafasi nzuri tu kwenye taasisi binafsi.

SOMA; Hizi Ndio Mbinu Anazutumia Mwajiri Wako Kuhakikisha Unaendelea Kuwa Mtumwa Wake.

Ni ndani ya miaka kumi tu mambo yamebadilika mno, huwezi hata kukumbuka kama kweli tulikuwa tukiambiwa udaktari na ualimu unakupa uhakika wa ajira. Sasa hivi serikali inatangaza wazi inaajiri baadhi ya walimu wa sayansi na hisabati, wale ambao ni wa sanaa na masomo mengine haiwahitaji kwa sasa. Sasa hivi serikali haiwezi kuajiri madaktari, wapo ambao wamehitimu kwa zaidi ya miaka miwili lakini bado hawajapata ajira, na hata serikali itakapoajiri, bado haina uwezo wa kuajiri wote ambao wanasubiri ajira.

Unanijua mimi rafiki yako, sikuambii haya ili ulalamike, na kuikasirikia serikali kwa nini isikuajiri, nakuandikia hayo kukuonesha ukweli ni upi ili niweze kukuonesha hatua zipi uchukue. Kama unachotaka ni kuendelea kuilalamikia na kuilaumu serikali, kama wengi wanavyofanya, unaweza kuishia hapa, maana hapo chini nitakwenda kuongea mambo tofauti kabisa ambayo yanaweza yasikufurahishe.

Baada ya kuona utangulizi huo, sasa hapa naomba nikuambie mambo muhimu unayopaswa kuyajua kuhusu hali hii inayoendelea;

1. Tulidanganywa.
Swala zima la kusoma kwa bidii, ili kufaulu na kupata ajira nzuri limekuwa linahubiriwa kwa muda mrefu. Lakini ukweli ni kwamba tumedanganywa kwa muda mrefu na hadithi hiyo. Kama ambavyo tunaona sasa, kusoma na kufaulu vizuri hakukuhakikishii kupata ajira. Unaweza kuendelea kusubiri mpaka upate ajira ndiyo maisha yako yaanze, huku ukipoteza muda, au unaweza kuamua kuanza maisha yako kwa vyovyote ulivyo.

SOMA; HESABU RAHISI ZA AJIRA AMBAZO HUTAKI KUZIKOKOTOA.

2. Hali hii ni endelevu.
Yaani pamoja na haya yanayoendelea, wapo wengi wenye matumaini kwamba siku moja kila kitu kitakwenda poa. Watu wanaamini ajira zitakuja tu, na watapata ajira. Ninachotaka kukuambia ni kwamba hali hii ni endelevu. Wale ambao wapo kwenye uhitaji sasa, hawataendelea kuwepo kwenye uhitaji miaka yote, labda watakuwa wengi sana kuliko uwezo wa kuajiri, au uwezo wa kuajiri utapungua. Hivyo unapoyafikiria maisha yako ya mbele, jua kwamba ajira zitaendelea kuwa changamoto.

Hakuna mtu aliwahi kufikiri kirahisi kwamba tutafika wakati daktari anaomba kazi na hapati, lakini yanatokea sasa, na siyo mwisho.

3. Hakuna anayekosa usingizi kwa sababu ya matatizo yako binafsi.

Siku moja, naibu waziri mmoja akiulizwa maswali na waandishi wa habari, alitoa takwimu ambazo siyo sahihi kuhusu hali ya ajira kwenye wizara yake, alisema watu ambao bado hawajaajiriwa ni wachache na akataja idadi ndogo kuliko uhalisia. Wengi walilipuka kwa malalamiko juu ya kitendo hicho lakini kilipita. Lakini bado naona watu hawakujifunza. Kupitia kitendo kile cha naibu waziri, somo lilikuwa kwamba matatizo yako ya ajira hayamnyimi mtu yeyote usingizi.

Iwe una ajira au huna, waziri, naibu waziri, makatibu na wengine wote wanaendelea kupokea mishahara yao ya mwisho wa mwezi. Hivyo hawakosi usingizi usiku wakifikiria kuna watu wengi wamesoma na hawana ajira, wao wanaendelea na yao. Sasa ukichagua kuweka matumaini kwao, unachagua kuyaacha maisha yako yatima.

Uchukue hatua gani kama umesoma tayari umesoma lakini huna ajira?

Mwaka 2011 nilifukuzwa chuo kikuu cha udaktari, kwa tangazo la muda mfupi sana, nilipewa dakika 45 za kuondoka kabisa kwenye eneo la chuo. Na barua ilisema nimesimamishwa kwa muda usiojulikana. Hapa ndipo nilipoanza kuona uhalisia wa maisha upoje, unajua huwezi kuuona uhalisia wa maisha kama bado unaendelea kuishi kwenye uongo.

SOMA; Changamoto Kuu Mbili (02) Za Ajira Na Jinsi Unavyoweza Kununua Uhuru Wako Kwenye Ajira.

Hapa ndipo nilipofanya maamuzi thabiti ya kwamba kamwe sitaruhusu maamuzi ya mtu mmoja yavuruge maisha yangu, hivyo niliamua kupambana kwa kila namna kuhakikisha ndoto za maisha yangu hazipotelei hewani. Hivyo nilianza kufanya kila ambacho niliweza kufanya kwa wakati ule, ili kwanza kupata kipato. Lakini mawazo hayakubali kwenye kipato tu, bali niliendelea kuangalia ndoto zangu za mbele, hivyo sikukubali kubaki kwenye hali ya chini au kazi za chini nilizoanza nazo. Nilitumia kila kitu kama ngazi ya kupanda na kufika juu zaidi. Na bado mpaka sasa naendelea na mapambano kila siku, na kuendelea kupanda ngazi kila siku.

Hivyo ninachotaka kukuambia rafiki yangu uliyesoma na kakosa ajira ni hichi, PAMBANA, angalia kila fursa iliyopo mbele yako na itumie. Hata kama ni fursa ya hadhi ya chini kuliko elimu yako, itumie kama daraja la kukuvusha. Nimeona watu wengi sana ambao wanakataa kazi kwa sababu haziendani na hadhi zao, au kipato ni kidogo kulingana na thamani zao.

Sikiliza rafiki yangu, unapokuwa huna ajira, huna hadhi, huna anasa ya kuchagua ni kazi gani ya hadhi yako na ipi siyo ya hadhi yako. Unapokuwa huna kipato, huna anasa ya kuchagua kazi ipi inakulipa na ipi haikulipi, unahitaji kufanya kila kitu.

Anza na kazi za hovyo, anza na kipato kidogo, lakini usikwame pale, kwa sababu nimekuwa naona wengi wanakwama, kwa kuridhika na hivyo vidogo mwishowe maisha yao yanabaki katika ngazi zile.

Wengi wamekuwa wanaimba kazi hakuna, halafu wanakaa nyumbani kuangalia tv, au wanashinda kwenye mitandao kufuatilia maisha ya wengine, ambao wana kazi zao. Nikuambie tena rafiki, kazi zipo ila hazitakufuata nyumbani, hazitakufuata huko unakoshinda, wewe ndiye unapaswa kuzifuata kazi kule zilipo. Nenda kwa watu wanaohitaji kusaidiwa au kutatuliwa changamoto zao, waambie kipi unaweza kuwasaidia na fanya hicho. Hakuna mtu ambaye atakukatalia iwapo utaweza kutatua tatizo ambalo linawasumbua, au kuwapa kitu ambacho wanahitaji.

Hivyo jitoe, fanya kazi, ongea na watu wanaohusika na yale unayofanya, wakati mwingine jitolee kufanya bure ili kuonesha kile ambacho unacho, kuwa tayari kuanzia chini kabisa, lakini jambo la muhimu kabisa, usiache ndoto zako ziyeyuke, popote ulipo, pambana kufikia ndoto zako.

Kitu kingine muhimu kufanya kwenye wakati kama huu ni kujifunza sana, jifunze kila kitu unachoweza kujifunza na kinachoweza kukusaidia. Chagua maeneo unayotaka kuyajua, soma kila unachoweza kusoma kwenye eneo hilo. Utapata mtazamo wa tofauti, utajifunza kitu kimoja hapa na kingine pale, na vyote hivi vitaendelea kukusukuma mbele zaidi. Tangu mwaka 2012 mpaka leo nimesoma vitabu vingi mno mpaka vingine sikumbuki majina yake, lakini kwenye kila kitabu nilichosoma, kuna kitu kimoja au viwili nimeondoka navyo, ambavyo vimekuwa na vinaendelea kuwa mchango bora kwangu kufikia ndoto zangu.

Nimalize barua hii kwa kukuambia wewe rafiki yangu kwamba, kama utachagua kusubiri mpaka upate ajira hayo ni maamuzi yako, na kama utaamua kuchukua hatua sasa ni maamuzi yako. 

Nilichotaka kukuambia ni kwamba hapo ulipo hata mimi nimeshakuwepo hapo, tena bila ya kutegemea, lakini sikukubali kubaki hapo, nilipambana na ninaendelea kupambana.

Maisha yako ni jukumu lako, chukua hatua sasa na jua kila hatua ina mzigo ambao utahitaji kuubeba.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
 
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>