Hongera rafiki yangu kwa nafasi hii nyingine ambayo tumepata fursa ya kujifunza pamoja hapa. Kitu ambacho nimekuwa nakuambia kila siku ni kwamba, kujifunza ni hitaji la msingi sana la maisha ya mafanikio. Na linapokuja swala la mafanikio najua unajua msimamo wangu ni upi, kwamba MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.
Leo nataka nikukumbushe kitu kimoja muhimu kuhusu mafanikio yetu kwenye maisha. Nataka kukukumbusha kwa sababu kila mtu amekuwa anakudanganya maisha yako yote. Wamekuwa wanakuambia vitu ambavyo siyo vya kweli na siyo kwa makusudi, ila ni kwa sababu hata wao wenyewe hawajui.
Kitu ambacho tumekuwa tunadanganywa ni kwamba unastahili kitu fulani, hivyo subiri tu na utapewa. Tunaambiwa kwa sababu tumesoma basi tunastahili kupewa ajira, yenye maslahi mazuri na hatimaye kuwa na maisha bora. Tunaambiwa kwa sababu tumeajiriwa, basi ni jukumu la mwajiri wetu kutupa kila tunachotaka na kuhakikisha maisha yetu yanakuwa mazuri. Tunaambiwa kwa sababu tumeanzisha biashara basi wateja lazima watakuja, tusubiri tu wataona na kuja wenyewe.
Haya na mengine mengi tumekuwa tunaambiwa kwenye maisha yetu na kuyachukua kama yalivyo, tunapojaribu kuyatumia kwenye maisha yetu ndiyo ukweli unakuja wazi, kwamba mambo siyo kama tulivyoambiwa.
Ukweli ni kwamba, kwenye hii dunia hakuna mtu atakayekupa chochote kile unachotaka. Hilo ni jukumu lako kupambana na kuhakikisha unapata kile ambacho unataka kwenye maisha yako. Lazima wewe mwenyewe uwe mstari wa mbele kuhakikisha unapata kile ambacho unataka kwenye maisha yako.
Kusoma siyo uhakika wa kupata ajira, na hata kuipata siyo uhakika wa kuwa na maisha bora. Kuna juhudi za ziada unahitaji kuweka ili kuweza kuwa na maisha bora kama unavyotaka wewe mwenyewe.
Na kama ilivyo wazi sasa, unaweza kusoma lakini usipate ajira, na pia hakuna njia isiyo ya uhakika ya kupata kipato sasa kama ajira. Hivyo unapokuwa ukiyafikiria hayo ya ajira na kipato, lazima ujue jitihada zako mwenyewe zinahitajika sana.
Usiyakabidhi maisha yako kwa mtu yeyote yule, hata kama anaonekana anaweza kukusaidia kiasi gani, kumbuka hakuna anayeweza kujua vizuri kuhusu wewe zaidi yako mwenyewe. Na unapoweka juhudi zako binafsi, inakuwa rahisi hata wengine nao kukusaidia wewe ili ufanikiwe zaidi.
Kitu kingine usiwakabidhi watu maisha yako ambao hawana mpango wowote wa kuhangaika na maisha yako. Kwa mfano, lengo la mwajiri wako siyo kufanya maisha yako kuwa bora, wala siyo kukufanya wewe kuwa tajiri, bali yeye anataka umkamilishie majukumu yako, na yeye akuwezeshe kupata fedha ya kusukuma maisha yako, ila uendelee kumtegemea yeye. Hayo mengine unayopanga wewe wala hayapo kwenye akili yake. Hivyo bila ya wewe mwenyewe kupambana, utaendelea kusubiri kitu ambacho hakipo.
Na hata kwenye biashara, wapo watu wengi mno wanaanzisha biashara wakiwa na mtazamo ambao unawafanya wazione biashara kuwa ngumu kwao. Wengi wanaanzisha biashara wakiamini wateja wakishaona biashara zao basi watakuja kwa wingi. Au kwa kuwa wamenunua mara moja basi watanunua tena. Huku ni kujidanganya ambapo kutafanya biashara iwe ngumu mno.
Unahitaji kuwatafuta wateja kwa nguvu popote pale walipo. Unahitaji kuwafikia na kuwashawishi wateja kwa nini waje kununua kwako na siyo kwa wafanyabiashara wengine kama wewe. Jua nini shida zao na unazitatuaje, kisha wajue wazi namna gani unatatua. Jua mahitaji yao na yatimize, kisha wafanye wajue kwamba unaweza kuwatimizia mahitaji yao.
Watu wengi hufikiri biashara ni kuwa na mtaji tu halafu ukaifungua, hiyo ni sehemu ndogo sana ya biashara. Sehemu kubwa ya biashara ni kuuza na ili uuze lazima uwe na wateja wa kutosha kwenye biashara yako. Hivyo masoko ni eneo muhimu la biashara yako ili uweze kupata wateja na baadaye uweze kuuza.
Hivyo nilichotaka kukukumbusha leo rafiki, hakuna mteremko, mapambano ni muhimu. Chochote unachotaka, jua hakuna atakayekuletea hapo ulipo, lazima upambane kukipata. Na kadiri unavyopambana mapema, ndivyo unavyotengeneza nafasi nzuri za kuweza kufanikiwa mapema.
Nikutakie mapambano mema rafiki yangu, usikate tamaa rafiki yangu, kama bado upo hai, mapambano lazima yaendelee.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.