Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

USHAURI; Jinsi Ya Kupata Elimu Bora Ya Kufanikiwa Kwenye Biashara Hata Kama Una Elimu Ndogo Ya Darasani.

$
0
0
Rafiki,

Karibu kwenye kipengele chetu cha ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia maisha ya mafanikio. Changamoto zipo na zitaendelea kuwepo, hatua bora kwetu kuchukua siyo kuzikwepa, bali kuzitatua. Unapotatua changamoto unakuwa mtu wa tofauti kabisa, kwa sababu changamoto ya aina ile haiwezi kukusumbua tena. Ni sawa na kufaulu kidato kimoja kwenda kingine.

Ni matumaini yangu kwamba wewe rafiki yangu upo vizuri na unaendelea kupambana ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi. Ni kukumbushe tu ya kwamba hakuna mbadala wa mapambano, kwa sababu hakuna chochote utakachokipata kwa mteremko.

Leo tunakwenda kuangalia changamoto ya elimu ndogo kama kikwazo cha kuingia kwenye biashara. Wapo watu ambao wanajizuia kuingia kwenye biashara kwa sababu ya elimu yao ndogo. Na pia wanashindwa kuzitumia fursa nyingi za kujifunza zinazopatikana ili kuweza kupiga hatua. Karibu kwenye makala hii kujua hatua za kuchukua ili uweze kuanzisha na kukuza biashara hata kama elimu yako ni ndogo.

Kabla hatujaangalia hatua zipi unaweza kuchukua, tusome maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu changamoto hii.

Changamoto kwangu naona ni kiwango cha elimu cha kawaida ambacho ni kidato cha nne ambapo kwa sasa hivi ni ngumu kuingia katika ushindani wa ajira, lakini pia unaweza kusema ujiajiri bado kwani elimu za ujasiriamali bado ni ngumu kufika huku kijijini, hivyo waweza kukwama kutokana na udogo wa elimu uliyonayo. Rajabu M.M

Ni kweli kwamba elimu ndogo inaweza kuwa kikwazo kwa mtu kuajiriwa, kwa sababu ajira nyingi zinahitaji watu ambao wana utaalamu fulani ili kuweza kuzifanya. Kwa mfano haijalishi unapenda kiasi gani kufundisha, kama hujasomea ualimu hakuna anayeweza kukuajiri ufundishe.

Lakini biashara ni tofauti, hakuna kikwazo chochote kwa mtu kuanza biashara kwa sababu ya elimu ndogo, au kukosa kabisa elimu ya darasani. Bali mtu anaweza kuanza biashara kwa kujifunza yeye mwenyewe na kuendelea kujifunza kadiri anavyokwenda.

Hivyo mtu yeyote anayesema kwamba ameshindwa kuenza biashara kwa sababu elimu yake ni ndogo, kuna kitu anaficha, hiyo siyo sababu halisi. Kuanza biashara yako mwenyewe, hasa ambayo ni ndogo kabisa huhitaji kupeleka vyeti vyako popote, wala huhitaji kumwomba mtu chochote. Unachohitaji wewe ni kuona hitaji la watu ambalo unaweza kulitimiza na kisha kuanza kulifanyia kazi.

Kuhusu kukosa elimu ya ujasiriamali au biashara.

Kitu kingine ambacho watu wamekuwa wanakitumia kujikwamisha ni kuamini bado hawajapata elimu ya kutosha ya biashara na ujasiriamali. Na hivyo kuendelea kusubiri, kama vile kuna siku watu watawaita na kuanza kuwafundisha.

Elimu ya biashara na ujasiriamali, hasa wa kufanya kwa vitendo, ni tofauti kabisa na elimu ya darasani. Hakuna siku ya kujiandikisha na masomo kuanza, bali hii ni elimu endelevu na elimu ya kujituma wewe mwenyewe. Siyo elimu ya kusoma ili ujibu mtihani, au ili upate cheti, bali ni elimu ya kusoma ili utoke na kitu cha kufanya.

Hivyo basi, usisubiri mtu aje kukupa elimu ya ujasiriamali, bali hii ni elimu ambayo unapaswa kuitafuta wewe mwenyewe. Wewe mwenyewe lazima uchukue hatua za makusudi na uwe na njaa ya kweli ya kupata elimu hii. Na hapo utaona kila fursa ya kupata elimu hiyo. Na hii haijalishi kama upo mjini au kijijini, dunia ya sasa ni ya tofauti kabisa, haitofautishi mjini na kijijini katika upatikanaji wa elimu, maarifa na taarifa.

Hatua unazoweza kuchukua kujifunza biashara na ujasiriamali;

Kwanza; nunua vitabu na majarida yanayofundisha kuhusu biashara na ujasiriamali, hapa utapata elimu ya msingi kabisa kwenye biashara na ujasiriamali. Vitu kama namna ya kuboresha wazo lako la biashara, kuwafikia wateja zaidi, kudhibiti matumizi yako ya kifedha utajifunza kwa njia hiyo.

Pata na usome kitabu cha BIASHARA NDANI YA AJIRA, utajifunza misingi muhimu ya biashara. Kupata kitabu hichi, tuma ujumbe kwenye simu namba 0717396253.

Pili; tembelea mitandao inayoandika kuhusu biashara na ujasiriamali, hapa huhitaji hata gharama kubwa. Kupitia mitandao hiyo utajifunza mambo mengi na mapya kwenye biashara na ujasiriamali.

Tembelea www.amkamtanzania.com na www.kisimachamaarifa.co.tz kila siku na utajifunza mengi kuhusu biashara na mafanikio.

Tatu; tembelea watu ambao tayari wanafanya kile unachotaka kufanya, na jifunze kutoka kwao. Jifunze kwa kuangalia namna wanafanya, na pia jifunze kwa kuwauliza na kupata majibu ya mambo mbalimbali yanayohusu wanachofanya. Hapa utajua changamoto mbalimbali wanazopitia na namna wanavyozitatua.

Nne; anza biashara yako mwenyewe na hilo ndiyo darasa la maisha yako yote. Ukishakuwa kwenye biashara, kila siku kwako ni nafasi ya kujifunza. Kila siku vipo vitu vingi vya kujifunza kupitia changamoto unazokutana nazo na pia ili kukua zaidi. Unapokuwa kwenye biashara unajifunza vitu vingi zaidi na kwa uhalisia kuliko unavyojifunza kabla hujaingia kwenye biashara.

Hivyo haijalishi elimu yako ni ndogo kiasi gani, zipo fursa nyingi sana za kujifunza biashara. Tumia njia hizo nne nilizokushirikisha hapo juu na utaweza kuanzisha na kukuza biashara yako mwenyewe.

Elimu kamwe haipaswi kuwa kigezo cha wewe kutokuingia kwenye biashara, hasa kwa karne hii tunayoishi sasa. Tumia kila fursa inayokuzunguka kuhakikisha unaanza biashara yako na kuweza kuikuza.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,



TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kama ungependa kupata ushauri wa moja kwa moja kutoka kwangu kuhusiana na changamoto yako bonyeza maandishi haya na utapata utaratibu wa kupata ushauri kutoka kwangu. Karibu sana rafiki tufanye kazi kwa pamoja.

Kupata vitabu vya mafanikio kwenye Kazi, Biashara Na Maisha kwa ujumla tembelea MOBILE UNIVERSITY, bonyeza hayo maandishi.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>