Habari mpendwa rafiki na msomaji wa mtandao wa Amka Mtanzania? Ni matumaini yangu unaendelea vizuri na maisha yako lakini pia unaendelea kugusa maisha ya watu wengine na siyo kuishi maisha ya kibinafsi ya kujifikiria wewe mwenyewe na familia yako. Leo ni zawadi ya kipekee sana katika maisha yetu hivyo ni vema na haki kuitumia zawadi hii vizuri kwa kuzalisha mambo chanya katika maisha yetu.
Mpendwa msomaji, kila siku unatakiwa kujitahidi kuanza siku yako katika hali ya mtazamo chanya. Hakikisha asubuhi yako umeianza kwa kuingiza kitu chanya na siyo kuanza kusikiliza habari ambazo zinakuletea mtazamo hasi wa siku. Kwa mfano, unafungulia habari katika radio asubuhi unasikia watu kumi wameuawa na bokoharamu je habari hiyo itakusaidia nini katika maisha yako? Kwa hiyo habari nyingi zimeandaliwa kimasilahi hususani katika magazeti zinawakosesha matumaini watu wengi na kuwaaminisha kuwa duniani si sehemu salama.
SOMA; Mambo Mawili (2) Ya Msingi Ya Kuzingatia Katika Msamaha Wa Kweli.
Rafiki, napenda kukushauri usianze siku yako kwa kusikiliza habari kwani hazitokupa utulivu wa akili na utashindwa kuanza siku yako kwa furaha na hamasa kubwa ya kwenda kufanya kazi.
Basi, ndugu msomaji, nikualike tena katika makala yetu ya leo ambapo leo tutakwenda kujifunza wote kwa pamoja dayari unayopaswa kwenda kuichoma moto leo katika maisha yako.
Mpendwa msomaji, huenda unajiuliza katika akili yako ni dayari gani basi unayopaswa kwenda kuichoma katika maisha yako? Ili kuweza kufahamu ni dayari gani unayopaswa kwenda kuchoma moto leo basi nakualika uweze kusafiri pamoja nami mpaka mwisho wa somo letu la leo ili uweze kuyafahamu yale mazuri niliyoweza kukuandalia siku hii ya leo. Karibu sana rafiki tuweze kujifunza wote kwa pamoja.
Mtu mmoja aliyejulikana kwa jina la ndugu alichaguliwa kuongoza kikundi cha watu kumi na tano. Ndugu huyo alipochaguliwa kuongoza kikundi cha watu hao kumi na tano alikuja na sera zake juu ya kuliongoza kundi lake. Ndugu huyo baada ya kuwasilisha sera zake katika kikundi hicho wale wenzake kumi na nne walimpinga pamoja na kumcheka na kumkebehi kulingana na aina ya uongozi wa ndugu huyo.
Kila siku ndugu alikuwa akijaribu kuwasilisha mambo kwa wanakikundi wake lakini wanakikundi wenzake waliendelea kumpinga na kuchemka na kumpa kila aina ya kebehi unayoijua. Ndugu huyo baada ya kuona kila anapofanya jambo hakubaliki kwa wenzake aliamua kuchukua dayari au kijitabu kidogo ili aweze kuandika orodha ya machungu na maumizo ya moyo.
SOMA; Hivi Ndivyo Utakoweza Kuishi Na Mtu Wa Aina Yoyote Ile Kwa Furaha Na Amani - 2
Ndugu aliendelea kuwaongoza hivyo hivyo kwa muda mrefu sasa huku akiendelea kuwaongoza wenzake aliendelea kuandika kila siku yale mambo mabaya anayotendewa na wenzake. Aliamua kuandika machukizo yote anayofanyiwa katika maisha. Hivyo dayari ya kuorodhesha maumizo iliendelea kujaa. Alikuwa anaandika na kuyasoma yale maumizo anayopatiwa na mwenzake kila siku.
Ndugu msomaji, yale maumivu aliyokuwa anayaandika na kuyasoma kila siku yaliendelea kugeuka kuwa mwiba na kumuumiza moyo wake. Majeraha ya nafsi yaliendelea kumtafuna kila siku huku akijua njia bora ya kumaliza matatizo ni kuendelea kuandika na kuyasoma kila siku.
Mpendwa msomaji, tunajifunza nini kupitia ndugu huyu? Tunajifunza kuwa katika maisha yetu hatupaswi kuandika orodha ya maumivu tunayofanyiwa na wengine katika maisha yetu. Ndugu huyu alisahau kabisa kuwa dawa ya kuondoa maumivu katika moyo ni kumfutia mtu deni kwa kumsamehe tu. Ndugu alishindwa kufikiria njia nzuri ya kuondokana na mateso moyoni ni kusamehe badala ya kuendelea kuorodhesha maumivu.
Siku moja ndugu alichukua dayari yake aliyokuwa akiandikia majeraha ya moyo wake akaanza kusoma mwanzo hadi mwisho. Baada ya kusoma aliweza kupata na maumivu na majeraha makubwa katika maisha yake aliamua kulia kwa uchungu na hatimaye alifanya maamuzi ya kuchoma daftari la kuandika kumbukumbu ya orodha ya maumivu.
SOMA; Hizi Ndizo Lugha Tano (5) Muhimu Za Kuonesha Upendo Kwenye Mahusiano Yetu.
Baada ya kulichoma daftari hilo alijihisi mtu mpya katika maisha yake na kujiona mtu wa furaha na amani katika maisha yake.
Kweli msamaha huleta uhuru wa ndani na kutambua amani ya ndani na kuonja huruma ya Mungu ndani ya maisha yetu. Ni watu wangapi katika maisha yetu wanaendelea kuteseka katika maisha yako kuandika maumivu katika mioyo yao na kushindwa kusamehe? Ni vema kuamua kuchoma dayari ya maumivu katika maisha yako na kuwa mtu mpya.
Hatua ya kuchukua leo, nenda leo kachome daftari la kumbukumbu ya orodha ya maumivu katika maisha yako. Kachome daftari na kuanza maisha mapya ya uhuru na amani ya moyo na siyo kuandika maumivu kama mfano wa ndugu hapo juu.
Kwa hiyo, msamaha ni dawa ya kufuta maumivu uliyoandika katika dayari ya moyo wako.
Unaposamehe unakuwa unamfutia mtu deni na hivyo kubaki huru. Kumbuka upendo haukasiriki pale unapomsamehe mwenzako bali upendo huvumilia yote na wala hauandiki orodha ya maumivu moyoni. Kuendelea kuandika orodha ya maumizo katika dayari ni kujichagulia kuishi dunia ya kifungoni na siyo dunia ya uhuru.
Makala hii imeandikwa na Deogratius Kessy ambaye ni mwandishi, mhamasishaji na mjasiriamali, unaweza kuwasiliana naye kupitia namba 0717101505/0767101504 au kwa barua pepe deokessy.dk@gmail.com, kessydeo@mtaalamu.net au unaweza kutembelea tovuti yake, www.mtaalamu.net/kessydeo ,www.actualizeyourdream.blogspot.com