Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Zawadi Ya Vitabu Kumi(10) Nilivyosoma Kwenye Siku Saba(07) Za Likizo Yangu Binafsi.

$
0
0


Habari za leo rafiki yangu?

Sikukuu za mwisho wa mwaka zinakwendaje kwa upande wako?

Kama ambavyo nilikujulisha wiki moja iliyopita, nilikuwa likizo yangu binafsi ya siku saba. Likizo hii ilianza ijumaa tarehe 23/12/2016 mpaka jana alhamisi tarehe 29/12/2016. Huu ni utaratibu ambao nimejiwekea kila mwaka ambapo napata wiki moja ya kukaa mbali na dunia na kufanya mambo muhimu kwangu na kwa kazi zangu.

Likizo ya mwaka huu nilidhamiria kupata muda wa kutafakari kuhusu maisha yangu na kazi zangu na kuweka mikakati ya mwaka unaokuja 2017. Pia nilidhamiria kupata muda mwingi zaidi wa kufanya meditation na kuzama zaidi kwenye meditation. Na kingine kikubwa ambacho nilipanga kufanya ilikuwa kusoma angalau kurasa 500 za vitabu kila siku, huu ukiwa ni wastani wa vitabu viwili kila siku.

Nashukuru nimemaliza likizo yangu ya wiki moja, imekuwa na manufaa makubwa kwangu binafsi na pia itakuwa na manufaa kwako kwa kadiri tunavyoendelea kuwa pamoja kupitia kazi zangu. 

Nimefanikiwa kufanya mengi niliyopanga kufanya, na zaidi nimejifunza mambo makubwa sana ambayo sikuwa nimejifunza mpaka sasa. Nazidi kuielewa ile kauli ya mwanafalsafa Socrates kwamba kadiri unavyojifunza, ndipo unagundua kwamba kuna vitu vingi hujui.

Zoezi la kusoma kurasa 500 kila siku lilishindikana.

Pamoja na kufanikisha mengi niliyopanga kwenye likizo hii ya siku saba, zoezi la kusoma kurasa 500 za vitabu kila siku lilishindikana. Sikuweza kusoma kurasa 500 hata siku moja. Siku ambayo nilijitahidi sana nilifika kurasa 400, na siku nyingine nimekuwa nasoma kati ya kurasa 200 mpaka 300.

Pamoja na kushindwa huku kusoma kurasa 500 kama nilivyopanga, nimejifunza mambo mengi sana na ambayo yatakuwa na msaada kwangu, hasa kuhusu usomaji.

Niligundua kwamba ili niweze kusoma kurasa 500 kwa siku, kwanza nilihitaji kutenga angalau masaa 10 kwa siku kwa ajili ya kusoma pekee, na hili halikuwa shida kwangu, kwa sababu kwa siku hizi saba za likizo, nimekuwa natumia wastani wa masaa 10 kila siku kwa ajili ya kusoma.
Changamoto kubwa na ambapo nimejifunza ni kwenye kasi ya usomaji. Ili niweze kusoma kurasa 500 kila siku, ilinipasa nisome kwa kasi (speed reading). Hii ni njia ambayo kwa dakika moja unaweza kusoma kurasa mbili mpaka tatu za kitabu. Ni njia nzuri kupata maarifa ya jumla kutoka kwenye kitabu, kwani hapa husomi kila neno na husomi mstari kwa mstari.

Sasa hivi sivyo ninavyopenda kusoma mimi, mimi napenda kusoma mstari kwa mstari, nikiruka hata mstari mmoja nahisi kuna kitu nakosa, nina udadisi wa hali ya juu kitu ambacho kinanifanya nisipende kusoma kwa kasi.
Hivi ndivyo ninavyosoma kitabu;

Kwanza kabisa nasoma kila ukurasa, kuanzia yaliyomo, dibaji, utangulizi na kama kuna sifa zimetolewa kuhusu kitabu basi nasoma zote. Mimi kama mwandishi najifunza mengi sana kwenye kila kinachoandikwa kwenye kitabu.

Kwenye usomaji huwa napenda kuchukua point ninazojifunza kwenye kitabu husika. Hivyo kila kitabu ambacho nimewahi kusoma, nina notes zake na nimezihifadhi kwenye mtandao. Hii ina maana siku yoyote nikitaka kufanya marejeo ya kitabu fulani nilichosoma basi nafungua nilipohifadhi zile point nilizoandika.
Yote haya yananizuia nisiweze kusoma kwa kasi.

Kitu kikubwa nilichojifunza wakati nasoma, ni kutokusoma kwa ajili ya kumaliza kurasa fulani, badala yake nasoma kwa ajili ya kujifunza. Hivyo kama nimesoma kurasa 10 na nimejifunza kitu ambacho naweza kukifanyia kazi hii ni bora kuliko kusoma kurasa 100 halafu nisitoke na kitu ninachoweza kufanyia kazi.

Hivyo baada ya likizo hii ya siku saba, nitarudi kwenye utaratibu wangu wa kawaida wa kusoma vitabu viwili kila wiki, ili pia niweze kufanya mambo mengine, ikiwepo kukuandalia makala nzuri zaidi, zitakazokupa maarifa sahihi ya kukuwezesha kufanya maamuzi sahihi kwenye maisha yako.

Vitabu 10 nilivyosoma wakati huu wa likizo.

Hivi hapa ni vitabu 10 nilivyofanikiwa kusoma ndani ya siku saba za likizo. Nitakupa utaratibu wa wewe kuweza kupata vitabu vyote hivi bure kabisa ili uweze kujifunza pia. Hapa nitakushirikisha kwa uchache kile ambacho nimejifunza kwenye kila kitabu, nitaendelea kukushirikisha mengi zaidi kadiri tunavyokwenda.

1. TRIBES; We need you to lead us – Seth Godin.

Seth Godin ni mmoja wa waandishi ambao wamenivutia sana katika uandishi, amekuwa akienda kinyume kabisa na mambo yote ambayo watu wamekuwa wanafanya kwa mazoea. Ni yeye alinihamasisha kuandika kila siku, kupitia blog yake ambapo amekuwa anaandika kila siku tangu mwaka 2003. Mimi nimeanza kuandika kila siku tangu mwaka 2014, na sina mpango wa kuacha kuandika kila siku, mpaka siku ambayo nitaondoka hapa duniani.

Katika kitabu hiki cha TRIBES, Seth anatuonesha namna bora kabisa ya kuwa kiongozi kwenye kile ambacho mtu unachagua kufanya. Seth anasema kwamba yapo makundi ya watu ambayo yapo tayari kuongozwa, unachohitaji ni wewe kuwafikia watu hao na kuwaongoza. Seth ametoa mifano namna ambavyo biashara, wasanii na hata harakati zilivyoweza kupata wafuasi wengi. 

Anasema wafuasi wapo tayari kwa jambo lolote unalotaka kufanya, ni wewe kujitokeza na kuwaongoza wafuasi hao.

Kuna mengi sana ya kujifunza kwenye kitabu hiki kuhusu biashara, uongozi na maisha kwa ujumla.

Kama wewe ni mfanyabiashara, kiongozi kazini, mwandishi au msanii, usiache kusoma kitabu hiki. Seth atakufundisha jinsi gani ya kupata wafuasi kwenye jambo lolote unalofanya. Na kama unavyojua kwenye dunia ya sasa, unahitaji watu wanaokubaliana na wewe kwenye lile unalofanya ili uweze kufika kule unakotaka kufika.

2. TRUMP UNIVERSITY WEALTH BUILDING 101; Your first 90 days on the path to prosperity.

Nafikiri ukishasikia tu neno Trump unapata picha ya utajiri kwenye mawazo yako. Ndiyo Donald Trump ni mfanyabiashara bilionea ambaye mwaka 2016 ameishangaza dunia kwa kuweza kuwa raisi wa Marekani kinyume na matarajio ya wengi. Pamoja na utajiri wake, amekuwa anapenda sana kuandika vitabu, na niliwahi kukushirikisha vitabu vyake vingine vitano, unaweza kubonyeza hapa kama hukupata vitabu vile vitano.
Kwenye kitabu hiki Trump, pamoja na waandishi wengine, anatushirikisha maarifa ya kufikia utajiri kwenye maisha yetu. Kwenye kitabu hiki Trump ameanza kwa kutufungua akili zetu kuhusu utajiri, kwa kutushirikisha mambo 12 muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo ili kufanikiwa.

Kupitia kitabu hiki tunajifunza njia za kuongeza kipato, kujilipa wewe mwenyewe kwanza, kuwekeza kwenye hisa, majengo na pia kulinda utajiri wako. Najua unapenda kuwa tajiri kama bado hujawa, na hata kama tayari umeshakuwa tajiri, basi yapo mambo ya kuwezesha utajiri wako udumu. Kwenye kitabu hiki, utajifunza yote hayo.

3. MEDITATION; Meditation techniques, spiritual growth and stress management. – Jasmine Bell.

Kama ambavyo nilikuambia, kwenye likizo hii nilipanga kuzama zaidi kwenye meditation, na hivyo nilichukua kitabu rahisi cha kuanza nacho, na hiki kilikuwa kizuri. Kimeelezea mbinu mbalimbali za kufanya meditation, namna ya kutumia meditation kuondokana na msongo wa mawazo na hata kuweza kukua kiroho kupitia meditation.

Kupitia kitabu hiki, hata kama hujawahi kufanya meditation kabisa, utapata mwongozo mzuri sana. Ni kitabu kifupi kusoma na unaweza kuanza kufanyia kazi mara moja. Utajifunza mambo ya kuzingatia kabla na baada ya meditation, na mbinu bora za meditation kulingana na mahitaji yako.

4. SUPERCOACH; 10 secrets to transform anyone’s life. – Michael Neill.

Kama ambavyo maneno ya kitabu yanasema, hapa unakutana na supa kocha Michael ambaye atakushirikisha siri 10 za kuyabadili kabisa maisha yako.
Wakati nachagua kusoma kitabu hiki nilikuwa nahitaji kupata maarifa zaidi kwa ajili ya ukocha wangu, namna ya kuwasaidia watu kufikia mipango ya maisha yao. Lakini nimejikuta najifunza mengi mno kuhusu maisha yangu mwenyewe, ambayo yataniwezesha kuyafanya maisha yangu kuwa bora zaidi.

Kwa kitabu hiki pekee, nimeandika point 72 ambazo nimeondokana nazo kwenye kitabu hiki. Ni kitabu ambacho nimeandika notes nyingi kuliko vitabu 10 nilivyosoma.
Kwenye kitabu hiki unajifunza kila kitu, kuanzia mtazamo wako juu ya maisha, maamuzi unayofanya, namna ya kuwashawishi watu wakubaliane na wewe, namna ya kufikia uhuru wa kifedha na kujenga matumaini ya mafanikio.
Kwa maneno mafupi niseme tu; SOMA HIKI KITABU.

5. THE PROPHET – Khalil Gibran.

Hiki ni kitabu ambacho sikuwa nimepanga kukisoma, lakini nilikuta kimenukuliwa kwenye kitabu cha Meditation, nikaamua kukiangalia, nikakuta ni kitabu kifupi, na hivyo kuweza kukisoma mara moja.

Kitabu hiki ni nabii ambaye alikaa na watu kwa muda mrefu, ukafika wakati wa yeye kuondoka, lakini wakati anaondoka watu wakawa wamejawa na simanzi, basi wakajikusanya na wakamwomba awafundishe kwa mara ya mwisho. Hivyo wakawa wanamwuliza maswali kuhusu maeneo mbalimbali ya maisha, na yeye akawa anawashirikisha busara zake. Walimwuliza maswali kuhusu upendo, ndoa, watoto, kutoa, kula na kunywa, kazi, furaha na huzuni, nyumba, mavazi, biashara, uongozi, uhalifu na mengine mengi. Kwa kifupi kila eneo la maisha yetu ya kila siku limeulizwa na kuna busara nzuri sana za namna ya kupeleka maisha yako ya kila siku.
Ni kitabu kifupi sana, kisome.

6. THE ART OF POWER – Thich Nhat Hanh.

Hakuna kitu kimeleta maafa kwenye dunia hii kama tamaa ya madaraka. Mtawa wa kibudha Thich Nhat Hanh ameyazungumzia madaraka kwa upande wa kiroho. Ametufundisha namna ambavyo tunaweza kuyapata madaraka na kuyatumia kwa manufaa yetu na ya wengine pia. 

Thich anatufundisha nguvu tano za kiroho ambazo kila mmoja wetu anaweza kuzitumia kufanya mambo makubwa kwenye maisha yake. Pia anatufundisha namna ya kutuliza akili zetu (MINDFULLNESS) na kuweza kufanya maamuzi bora. Anatukumbusha kuhusu tamaa ambazo zimewaharibu watu wengi.

Hiki pia ni kitabu cha kusoma, kwa kila kiongozi na mtu mwingine yeyote ambaye anapenda kuwa na mchango chanya kwa wengine.

7. HOW THE MIGHTY FALL; And why some companies never give in. – Jim Collins.

Jim Collins amewahi kuandika vitabu viwili maarufu sana; BUILT TO LAST na GOOD TO GREAT. Katika vitabu hivi viwili alionesha jinsi gani makampuni makubwa yaliweza kufika pale yalipo na kwa nini yanaendelea kukaa kileleni. Baadaye kilichotokea ni kwamba mengi ya makampuni aliyoyasifia kwa kukua na kukaa kileleni, mengi yalianza kuporomoka na kupotea kabisa. Likamsukuma kuangalia kwa nini makampuni makubwa yanafikia hatua ya kufa, na kwa nini mengine yanaepuka kufa.

Kwenye kitabu hiki ameeleza hatua tano ambazo makampuni yanayokufa yanapitia, na kwa kila hatua ametoa mfano wa kampuni ambazo zilikuwa zinafanya yale yaliyopelekea kufa kwa makampuni hayo.

Japokuwa kitabu hiki kimeandikwa kutokana na tafiti za makampuni makubwa, ila hatua hizi tano zinapotiwa na mtu yeyote ambaye amewahi kupata mafanikio makubwa halafu akaporomoka. 

Umewahi kuona mtu alikuwa tairi halafu ghafla akaporomoka na kuwa masikini? Au msanii alikuwa maarufu lakini anaishia kupoteza umaarufu na maisha yanakuwa magumu? Vijana wanasema kafulia, waswahili wanasema utajiri ulikuwa wa dawa. Sasa ukisoma kitabu hiki, utaona wazi wazi namna mtu anavyochagua yeye mwenyewe kuporomoka kwa kupita kwenye hatua hizo tano.

Yaani baada ya kusoma hatua hizo tano za kuporomoka, nimeona namna watu wengi waliopata mafanikio na kupotea walipokuwa wanaanza kuharibu. Na pia naona makosa ambayo watu wanayafanya sasa ambayo yanawapelekea kushindwa baadaye.

Hiki ni kitabu ambacho kila mtu inabidi akisome, kwa sababu najua utafanikiwa, lakini kukaa kwenye mafanikio hayo kwa muda mrefu ni kitu ambacho sina uhakika nacho, kwa sababu sijui maamuzi gani utafanya ukishafanikiwa. Soma kitabu hiki ili uepuke kuchukua hatua ambazo zitaharibu mafanikio yako.

8. JUST RUN IT; Running an exceptional business is easier than you think – Dick Cross.

Biashara ndogo na za kati ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa mataifa mengi duniani. Lakini biashara hizi ndogo ndiyo zinaongoza kwa changamoto kwa sababu kuu moja; watu hawajui ni namna gani ya kuendesha biashara zao. Mwandishi Dick Cross, ambaye amebobea kwenye biashara ndogo na za kati, anasema ukiwauliza watu wanaendeshaje biashara zao, hutapata jibu la moja kwa moja.

Hii ni kwa sababu watu hawajawahi kufundishwa namna ya kuendesha biashara zao. Sijui unaelewa vizuri. Anachosema na ambacho ni ukweli ni kwamba watu huwa wanafundishwa vipande vya biashara, labda masoko, mauzo, uongozi, mzunguko wa fedha, lakini hawafundishi biashara kama biashara yenyewe. Yaani namna ya kufanya maamuzi ya kila siku kwenye biashara zao.

Kupitia kitabu hiki anatufundisha namna ya kuendesha biashara kwa ujumla. Siyo vipande vya biashara, bali biashara kama biashara. Kisome kitabu hiki, najua unahitaji kuwa kwenye biashara kama mpaka sasa bado hujaanza biashara.
9. MONEY; Master the game – Tonny Robbins.

Hiki ni kitabu kikubwa, kurasa 600 na bado sijamaliza kukisoma chote. Kitabu hiki kimeijadili fedha, pesa, chapaa au vyovyote unavyopenda kuuita wewe.
Tonny anakuambia hivi, UNAWEZA KUITAWALA FEDHA, AU FEDHA INAWEZA KUKUTAWALA. Na anachokufundisha kwenye kitabu hiki ni NAMNA YA KUITAWALA FEDHA.

Anaichukulia fedha kama mchezo ambao kama unataka kushinda, yaani kuwa na uhuru wa kifedha, basi lazima uujue mchezo na uweze kuutawala. Ipo misingi saba ambayo Tonny anatufundisha kwenye kitabu hiki; 1. Kuiweka akili yako sawa kuhusu fedha, hapa anatukumbusha kuhusu kujilipa wenyewe. 2. Kujua sheria za mchezo wa fedha, aisee kuna mengi sana unapaswa kujua kama unataka kuwa tajiri, wapo watu ambao wanachofanya ni kukutenganisha wewe na fedha zako. 3. Kuijua ndoto yako na gharama ya ndoto hiyo. 4. 

Kufanya maamuzi ya uwekezaji kwenye maisha yako. 5. Mpango bora wa uwekezaji ambao haukuletei hasara, hupotezi fedha hata kama uchumi unayumba. 6. Siri za uwekezaji za mabilionea ambazo watu wengine hawazijui 7. Kufurahia utajiri wako na kutoa kwa wengine.
Kitabu hiki kimeandikwa sana kwa mazingira ya marekani, kwa mfano uwekezaji kwenye masoko ya hisa ya marekani. Lakini yapo mengi ya kujifunza ambayo unaweza kuyafanyia kazi. Kisome kitabu hiki, ila jipe muda wa kutosha, ni shule ya kutosha kuhusu fedha.

10. MINDFUL WORK; How meditation is changing business from the inside out. – 

David Gelles.

Hiki ni kitabu ambacho rafiki yangu Dr Bukaza Chachage aliniachia muda kidogo alipopita ofisini kwangu. Sikuwa nimepata muda wa kukisoma na hivyo nilikiweka kwenye orodha ya vitabu vya kusoma kwenye likizo yangu.

Mwandishi wa kitabu hiki amechimba kwa undani kabisa namna ambavyo meditation inawasaidia watu kwenye ulimwengu wa biashara. Ametushirikisha tafiti mbalimbali za kisayansi na kitabibu ambazo zinaonesha faida za meditation.

Faida zipo nyingi mno, kupunguza msongo, kuongeza uzalishaji, kupunguza makosa, kuepuka kuchoka (burnout) na nyingine nyingi.

Kama unataka kupata sababu kwa nini kila siku ufanye meditation, hata kama ni kwa dakika tano tu, basi soma kitabu hiki. Ni kitabu ambacho kimeitenganisha meditation na dini yoyote ile, ameeleza namna meditation ilivyo demokrasia, kwamba huhitaji kuamini dini fulani ndiyo ufanye meditation, ni wewe kuamua kuituliza akili yako na kuvuna faida za kutosha.

Hivi ndiyo vitabu kumi ambavyo nimefanikiwa kuvisoma. Nakushauri sana na wewe uvisome, lakini usivisome ndani ya siku saba kama nilivyofanya mimi, bali visome kwa kadiri unavyoweza wewe, hata kama itakuchukua mwaka mzima, ni sawa kuliko kutokusoma kabisa.

Niseme kwamba kama ulikuwa hujui vitabu gani usome mwaka 2017, basi hivyo hapo, anza navyo.

Jinsi ya kupata vitabu hivyo bure kabisa.

Kwa kuwa wewe ni rafiki yangu, nakupa vitabu hivyo bure kabisa. vitabu 9 kati ya hivyo kumi ni softcopy hivyo utaweza kuvipakua popote ulipo, hicho cha kumi ni hardcopy, unaweza kukipata kwenye maduka ya vitabu.

Vitabu hivyo 9 nitaviweka kwenye kundi la TELEGRAM LA AMKA MTANZANIA, unachohitaji ni wewe kuingia kwenye kundi hilo na kuvipakua. Kujiunga na kundi hilo ni bure kabisa. unachohitaji ni kuwa na simu yenye telegram (telegram ni sawa na wasap) kisha bonyeza maandishi haya kujiunga. Kama utashindwa kujiunga kwa kubonyeza maandishi hayo, basi ingia kwenye telegram yako na tuma ujumbe kwa njia ya telegram wenye neno AMKA MTANZANIA kwenda namba 0755 953 887 kisha utaunganishwa kwenye kundi. Muhimu sana tuma ujumbe kwenye telegram, usitume kwa njia ya kawaida.
KUHUSU SEMINA YA 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO.

Rafiki, zimebaki siku chache sana kufika mwisho wa kulipia semina ya 2017 MAFANIKIO MAKUBWA BILA YA MALENGO. Semina hii inafanyika kwa njia ya mtandao wa wasap, kupitia kundi la KISIMA CHA MAARIFA. Kwa kulipia ada, unapata nafasi ya kushiriki semina hii ya kuuanza mwaka 2017 kivingine, unapata nafasi ya kushiriki semina nyingine ya katikati ya mwaka, na kila siku unapata mafunzo na hamasa ya kufikia mafanikio. Ada ni tsh 50,000/= na ni ada ya mwaka mzima ya kuwa kwenye kundi. Ili kujiunga tuma fedha kwenye namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenye namba 0717 396 253 na utaunganishwa kwenye kundi.

Karibu sana tuuanze mwaka 2017 pamoja na tusafiri wote pamoja mwaka mzima 2017 kwa mafanikio zaidi. Mwisho wa kulipia ada ni tarehe 02/01/2017. Wahi kulipa ada yako ili usikose nafasi hii. Kwa maelezo zaidi unaweza kunipigia simu kwenye namba 0717 396 253 na tukazungumza. Kujua utakayojifunza kwenye semina hii na faida zaidi za kujiunga, bonyeza maandishi haya. Karibu sana.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>