Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

USHAURI; Umuhimu Na Jinsi Ya Kutofautisha Biashara Na Maisha Ya Kawaida.

$
0
0

Mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA tumekutana tena leo kwenye kipengele hiki cha USHAURI WA CHANGAMOTO mbalimbali ambazo zinatuzuia kufikia malengo yetu na hatimaye mafanikio makubwa kwenye maisha. Maisha yana changamoto nyingi sana na wakati mwingine unaweza usione kipi sahihi cha kufanya hasa unapokuwa katikati ya changamoto hizi. Ni kupitia kipengele hiki ambapo tunaweza kusaidiana mawazo na hatimaye ukaweza kutatua changamoto yako.

Leo tutaangalia changamoto ya kutofautisha biashara na maisha ya kawaida. Hii ni changamoto kubwa sana na ambayo imewafanya wengi washindwe kufikia mafanikio kupitia biashara zao.

SOMA; Kitu Kimoja Unachohitaji Ili Kufanikiwa Kama Unaanzia Chini Kabisa.

 

Mara nyingi watu wanapopata matatizo kwenye maisha, huona biashara zao ni sehemu rahisi kwao kutatua matatizo yao. Tatizo kubwa linakuja kwamba mtu anapotumia biashara yake kutatua matatizo ya maisha, matatizo hayaishi na biashara inaathirika sana na hata kufa kabisa.

Hata watu wanaosema kwamba kuna chuma ulete kwenye biashara zao, wao wenyewe ndio chuma ulete kwa sababu wanashindwa kutenganisha biashara na maisha yao ya kawaida. Unapochanganya biashara na maisha ya kawaida huwezi kuona maendeleo makubwa kwenye biashara yako.

Je ufanye nini ili uweze kutofautisha maisha ya kawaida na biashara ili uweze kuona mafanikio kwenye biashara yako?

biashara-1

Kabla hatujaona nini cha kufanya, tuone maoni ya msomaji mwenzetu kuhusu swala hili.

Changamoto yangu ni kwamba: najihusisha na biashara ya nafaka(mahindi na mpunga). Nikiweka stoo kwa ajili ya kuuza baadae ili nipate faida,hali ya hewa inakuwa mbaya kama vile ukame na njaa hali inayopelekea kuwagawia tena ndugu zangu kiasi fulani cha hiyo stoo maana wananitegemea sana. Nikiuza kilichobaki hakinipi faida zaidi ya gharama za kununulia tu. Je nifanyeje?

Tumeona maoni ya msomaji mwenzetu juu ya muingiliano wa biashara yake na maisha ya kawaida. Inawezekana hata wewe kuna jinsi ambavyo biashara yako inaingiliana na maisha, kwa mfano matumizi yako yanatoka moja kw amoja kwenye biashara na vingine vingi.

Vifuatavyo ni baadhi ya vitu unavyoweza kufanya ili kutatua changamoto hii.

Kwanza kabisa ni muhimu utambue kwamba tatizo la njaa linalotokea halitokei kwa sababu wewe una akiba ya chakula. Na hata linapotokea na kama usingekuwa na akiba ya chakula, bado watu wangepata njia ya kutatua tatizo hilo. Ila kwa sasa hawafikirii sana njia nyingine kwa sababu wana uhakika kwamba wewe utakuwa na chakula wakati huo wa njaa na utawasaidia. Hii ni hali ya kawaida kwa binadamu, hatupendi kujichosha sana ahasa tunapokuwa na uhakika na kitu. Kikubwa cha kufanya hapa ni wewe kuwahamasisha hao ndugu zako watunze mazao ya kutosha wakati wa msimu wa mavuno, na uwaambie wazi kabisa kwamba mazao unayonunua wewe na kutunza sio kwa ajili ya chakula, bali ni kwa ajili ya biashara. Kwa hali hii utawafanya waanze kuchukua majukumu ya maisha yao na kuacha kuwa tegemezi. Najua unaweza kufikiria kwamba kufanya hivyo utaonekana una roho mbaya, ila ukweli ni kwamba unahitaji kuchagua kitu kimoja, kuonekana una roho nzuri, huku biashara yako inakufa na unaendelea kulalamika moyoni au kuonekana una roho mbaya, huku ukiwasaidia watu kuchukua majukumu ya maisha yao na wewe biashara yako kukua.

Hii pia unaweza kuitumia kwenye biashara ya kawaida, unapopata matatizo, mawazo yako ya kwanza yasiwe kwenye biashara yako, fikiria njia nyingine kwanza za kutatua tatizo hilo. Lazima kuna njia nyingi tu, hasa pale unapofikiria kama nisingekuwa na biashara hii ningefanya nini?

SOMA; Matumizi Mawili Ya Mbegu Za Mahindi.

Pili, badili mipango na muundo wako wa biashara. Kama unaona kufanya hiko nilichoshauri hapo juu ni kigumu kwako, basi unaweza kubadili muundo na mipango ya biashara yako. Kwa mfano badala ya kusubiri mpaka kipindi ambacho hakuna kabisa mazao ndio uuze, uza mapema kabla njaa haijaanza. Hata kama hutouza kwa bei kubwa sana, fanya hivyo ili kuepuka kukosa kabisa faida. Kumbuka hufanyi hivi ili kuwanyima ndugu zako chakula, ila unafanya hivi ili kuokoa biashara yako, ambayo kama ikikua, utaweza kuwasaidia hao ndugu zako zaidi. Angalia jinsi utakavyoweza kuuza mazao yako mapema kabla ya njaa kuingia na kulazimika kuwagawia ndugu zako na wewe kushindwa kupata faida.

Tatu, nunua mazao ya ziada wakati wa mavuno. Kitu kingine muhimu unachoweza kufanya, ni kununua mazao ya ziada wakati wa msimu wa mavuno. Fanya hivi ukilenga kuweka sehemu ya mazao hayo kama chakula pale njaa itakapotokea. Na njaa itakapotokea hakikisha unagawa kiasi kile cha ziada ulichonunua tu, kikiisha unawaambia ukweli kwmaba kimekwisha na waangalie njia nyingine za kuokoa maisha yao.

SOMA; UKURASA WA 11; Watu Hawa Wanakurudisha Nyuma.

Nne badilisha biashara kabisa. Kama hayo yote tuliyojadili hapo juu hayatawezekana kwenye hali yako, unachiweza kufanya ni kubadili biashara kabisa. Angalia ni biashara gani utakayoweza kufanya kwa maeneo uliyopo ambayo haitakuw ana muingiliano mkubwa sana na watu kiasi cha wao kukutegemea sana wewe. Ukifikiria vizuri hutakosa biashara ya tofauti. Kuliko kufanya biashara moja ambayo haikupeleki mbele miaka yote ni bora kubadili na kuangalia biashara nyingine ambayo inaweza kukupa nafasi nzuri ya kuendelea.

SOMA; Maswali Matatu Muhimu Ya Kujiuliza Kwenye Wazo Lako La Biashara.

Kikubwa nachoweza kukushauri kwa ujumla ni kwamba unahitaji kuwa makini sana na biashara yako. Watu wakishajua sehemu fulani kunapatikana suluhisho la matatizo yao, hawafikirii tena kitu kingine. Ni bora uamue kufanya maamuzi magumu ya kukuza biashara yako kwa njia tulizojadili hapo juu hata kama hao ndugu zako watakuona mbaya, ila biashara yako itakapokuwa utaweza kuwasaidia vizuri zaidi ikiwepo hata kuwapatia kazi mbalimbali. Lakini ukiendekeza hili la njaa, mtazidi kurudishana nyuma na hutawez akuwasaidia vizuri.

Kumbuka njia nzuri ya kumsaidia masikini ni wewe kutokuwa masikini, ukikubali kuendelea kuunganisha biashara yako na maisha, utaendelea kuwa masikini na hutaweza kuwasaidia hao ndugu zako.

Nakutakia kila la kheri kwenye kutenganisha biashara yako na maisha ya kawaida.

TUPO PAMOJA.

Makirita Amani 

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.

Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.

kitabu-kava-tangazo4322


Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>