Habari za leo rafiki yangu,
Hongera kwa kuchukua nafasi hii nzuri ya kuwa pamoja na mimi hapa, tukijifunza kwa pamoja njia za kufanya biashara wetu kwa ubora zaidi. Falsafa yangu kuhusu biashara ni hii; kama hujawahi kufanya biashara basi bado hujayajua maisha. Biashara ina kila funzo la maisha ambalo kila mtu anapaswa kulijua.
Kila biashara huwa inapitia changamoto kwa kipindi fulani. Wakati mwingine changamoto huwa ni ndogo na ya muda mfupi. Lakini upo wakati ambapo changamoto ni kubwa na ya muda mrefu.
Changamoto zina hatari ya kuua biashara. Na changamoto kubwa kabisa inayopelekea kiashara nyingi kufa ni mzunguko wa fedha kwenye biashara unapokuwa na misukosuko. Mzunguko wa fedha ukishaleta shida, biashara inakufa haraka sana.
Huwa nasema mzunguko wa fedha kwenye biashara, ni sawa na mzunguko wa damu kwenye miili yetu binadamu. Damu ikiwa na shida, tunakufa haraka mno, kwa sababu damu ndiyo maisha yenyewe.
Leo tunakwenda kujifunza mambo matano muhimu ya kufanya pale ambapo biashara inakuwa na changamoto zinazopelekea biashara hiyo kufa.
Moja; jua pale ulipo kibiashara.
Upo usemi kwamba kulijua tatizo ni nusu ya kulitatua. Unaweza kuonekana ni usemi wa kawaida, lakini una maana kubwa sana, na wengi huwa hawauzingatii. Utaona watu wanakaza na tatizo, kumbe hata hawajui kama wana tatizo.
Unapoanza kuona biashara inakwenda tofauti na ilivyokuwa inakwenda, ni wakati wa kufanya tathmini. Kaa chini na itathmini biashara yako. Piga mahesabu muhimu ya kibiashara, iwapo unauza bidhaa basi fanya hesabu ya mali ulizonazo, mauzo na matumizi.
Ni muhimu sana ujue biashara ipo wapi kwa wakati wa changamoto. Je biashara inajiendesha kwa faida au kwa hasara. Je mzunguko wa fedha ni chanya au hasi. Yote hayo utayajua ukikaa chini na kupiga hesabu muhimu za kibiashara.
Mbili; punguza matumizi yasiyo muhimu na weka vipaumbele kwenye matumizi.
Baada ya kujua biashara yako ilipo kwa wakati wa changamoto, unahitaji kuanza kuchukua hatua mara moja. Na hatua ya kwanza kabisa kuchukua ni kudhibiti matumizi. Kwa sababu kwenye matumizi ndipo fedha zako za biashara zinapopotelea.
Wafanyabiashara wengi huanza biashara wakiwa na matumizi madogo, lakini kadiri biashara inakua, matumizi yanaongezeka. Biashara inakuwa na changamoto lakini matumizi yapo juu.
Angalia ni matumizi yapi siyo muhimu kabisa kwa biashara yako, yale ambayo unaweza kuyaondoa na biashara ikaendelea kwenda bila ya shida yoyote.
Kwa yale matumizi ambayo ni ya muhimu na huwezi kuyaondoa kabisa, weka vipaumbele katika kuyalipia. Kwa mfano kama kuna eneo unaweza kulipa kiasi badala ya kulipa kwa ukamili, fanya hivyo. Angalia kila fursa unayoweza kutumia kupunguza fedha kuondoka kwenye biashara yako.
Tatu; ongeza mauzo.
Kudhibiti matumizi ni hatua ya kwanza tu ya kuokoa biashara yako. Kudhibiti matumizi kuna ukomo, kuna matumizi ambayo huwezi kuyaondoa kabisa, hivyo utaendelea kuwa nayo.
Hivyo wakati unadhibiti matumizi, wakati huo huo unahitaji kuongeza kipato kwenye biashara yako. Na njia pekee ya wewe kufanya hivyo ni kuongeza mauzo kwenye biashara yako.
Zipo njia nyingi za kuongeza mauzo, hivyo nakushauri ufanyie kazi njia zaidi ya moja.
Kwa mfano unaweza kuongeza mauzo kwa;
1. Kuongeza bidhaa au huduma zaidi kwa wateja ulionao sasa.
2. Kuongeza wateja wapya kwenye bidhaa au huduma ulizonazo sasa.
3. Kuwauzia bidhaa au huduma zaidi wateja ulionao sasa.
Tumia kila fursa kuhakikisha hesabu unayofunga kwenye biashara inaongezeka kila siku. Na kwa kuwa umeshadhibiti matumizi yako, basi hili litawezesha mzunguko wa fedha kwenye biashara kuwa imara.
Nne; angalia ni wapi ulipoanguka.
Watu wasiojifunza kwenye makosa yao wenyewe, huwa wamelaaniwa kurudia makosa hayo tena na tena na tena. Usiwe mmoja wa watu hao. Kuna makosa umefanya mpaka biashara yako ikaingia kwenye matatizo. Labda ulijisahau na kuanza kuendesha biashara kwa mazoea, au uliondoa fedha kwenye biashara na kupeleka maeneo mengine. Yote hayo ni makosa.
Unahitaji kukaa chini na kuangalia kila ulilofanya likachangia biashara kuyumba.
Shida kwa wengi ni kwamba biashara inapopata changamoto, wanatafuta nani wa kumlaumu. Na huwa hawakosekani, hali mbaya ya uchumi, sheria mbovu, serikali, hali ya hewa na kila kitu kinachofaa kutaja.
Usiwe mtu wa aina hii, angalia umechangiaje kufika pale ulipofika, na jifunze ili usianguke tena.
Tano; epuka mambo haya kwenye biashara.
Kuna mambo ambayo inabidi uyaepuke kwenye biashara yako, kama unataka ikue vizuri na kuweza kukuletea mafanikio.
1. Epuka kukopesha kwenye biashara, iwapo biashara yako siyo ya mfumo wa kukopesha, basi jua kukopesha wateja ni kuwapoteza. Ndiyo, utaona unawasaidia, lakini wengi watakuumiza. Epuka hili kadiri ya uwezo wako.
2. Epuka kuingia kwenye biashara ambayo huna uzoefu nayo. Kwa sababu umefanikiwa kwenye biashara moja, haimaanishi wewe ndiyo bingwa wa kila biashara, unahitaji kujifunza mengi unapoingia kwenye biashara ambayo huna uzoefu nayo.
3. Epuka kuibebesha biashara mizigo ambayo haiwezi kuhimili. Usilazimishe kuishi maisha ambayo yapo nje ya uwezo wako kwa kutegemea biashara, utaua biashara yako na kupoteza maisha yako.
Fanyia kazi mambo haya matano ili kuweza kuokoa biashara yako ambayo ipo kwenye changamoto, hasa kifedha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.
Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.