Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; On Becoming A Leader (Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Ili Kuwa Kiongozi Bora Kwa Zama Hizi).

$
0
0
Dunia ya sasa inabadilika kwa kasi sana, mambo mengi ambayo yalikuwa yamezoeleka sasa hivi hayana tena nafasi.


Mabadiliko haya ya kasi yanaleta changamoto kubwa kwa viongozi wa zama hizi. Wengi wameendelea kufanya mambo kwa mazoea na hivyo kushindwa au kukosa kabisa maarifa sahihi ya kuwa viongozi bora.

Mshauri wa mambo ya uongozi, Warreb Bennis, mwaka 1987 aliandika kitabu ON BECOMING A LEADER, akiangalia sifa za viongozi ambao wameweza kuwa na mafanikio makubwa. Miaka zaidi ya 20 baadaye, alitoa toleo jingine la kitabu hichi, kuonesha mabadiliko yanayoendelea duniani na namna viongozi bora wanavyokuwa viongozi bora.

Kupitia kitabu hichi, ametushirikisha misingi ambayo viongozi wenye mafanikio makubwa wamekuwa wanaiishi na imekuwa na msaada kwao.

Kwa sababu kila mmoja wetu anapaswa kuwa kiongozi kwa namba moja au nyingine, ni muhimu kila mmoja wetu akaijua misingi hii na kuitumia kwenye maisha yake ili kuweza kufanikiwa.

Karibu kwenye uchambuzi hii wa kitabu cha ON BECOMING A LEADER, nikushirikishe yale muhimu ambayo nimejifunza kwenye kitabu hichi. Mwisho kabisa nitakupa utaratibu wa kupata kitabu hichi ili uweze kukisoma zaidi.

1. Uongozi wa zama hizi ni ushirikiano.

Zamani ilizoeleka kwamba kiongozi ndiyo mwenye majibu yote sahihi na watu walipaswa kumfuata pekee. Lakini zama hizi uongozi ni ushirikiano baina ya kiongozi na wafuasi. 

Dunia ya sasa ina changamoto nyingi na ngumu, hakuna mtu mmoja anayeweza kuzitatua yeye peke yake, ushirikiano ni muhimu mno.

Ili kuwa kiongozi bora, tengeneza ushirikiano baina yako na wale ambao unawaongoza, wajione sehemu ya timu na siyo tu watu wa kufuata amri. Kwa njia hii utapata ushirikiano mzuri na mawazo mazuri kutoka kwa wengine.

2. Uhodari wa aina nne ambao viongozi bora wanao.
Kila kiongozi bora, ambaye ameweza kuwa na mafanikio makubwa, amekuwa na uhodari wa aina nne.

Moja; uwezo wa kuwashawishi wengine kupitia kile wanachofanya. Viongozi hawa wanakuwa na maono makubwa ambayo wengine wanahamasika kujiunga nao na kuweza kuyafikia kwa pamoja.

Mbili; wana sauti yao ya kipekee, ambayo wafuasi wanaikubali na kuifuata. Sauti hapa inahusisha vitu vingi, kusudi, kujiamini na ukomavu wa kihisia.

Tatu; uadilifu, viongozi wote wenye mafanikio wana uadilifu wa hali ya juu, wanayo misingi ambayo wanaiishi na kuisimamia. Maneno yao na matendo yao ni kitu kimoja.

Nne; utayari wa kubadilika, huu ndiyo uhodari wa tofauti zaidi kwa zama hizi za mabadiliko makubwa. Wale ambao wapo tayari kubadilika hata kama hawajawa tayari, wamekuwa viongozi bora.

Jijengee uhodari huu wa aina nne ili kuwa kiongozi bora.

3. Kujifunza uongozi siyo kitu rahisi.

Watu wengi wamekuwa wanabishana iwapo viongozi wanazaliwa au wanatengenezwa (kufundishwa). Na mara nyingi imekuwa inaishia kwamba viongozi wanatengenezwa. 

Lakini unapoangalia kwa undani zaidi, unagundua siyo sahihi kwamba viongozi wanatengenezwa kwa kufundishwa, bali viongozi wanajitengeneza wenyewe.

Uongozi ni mgumu sana kiasi cha mtu kuweza kufundishwa. Hii ni kwa sababu uongozi unahusisha mambo mengi, na zaidi watu. Sasa unaweza kutabiri na kupangilia kila kitu, lakini siyo watu. Watu hawatabiriki.

Ili kuwa kiongozi bora, kuwa tayari kujitengeneza wewe mwenyewe kuwa kiongozi, na hatua ya kwanza kufanya hivyo ni kujijua wewe mwenyewe kwanza.

4. Mkishakuwa watu watatu, uongozi ni lazima.

Mtu mmoja akiwa mwenyewe jangwani, hahitaji sana uongozi, anaweza kuendesha maisha yake namna anavyoweza. Mkiwa watu wawili, na kama mmeshibana sana, mnaelewana kwa kila jambo, mnaweza kwenda vizuri bila ya uongozi. Lakini mkishakuwa watatu, lazima mmoja awe kiongozi la sivyo hamtaweza kufanya chochote.

Kwa kuwa maeneo mengi ya maisha yako unakuwa na watu wengine, kuanzia kwenye familia mpaka kwenye kazi zako, ni muhimu sana uwe kiongozi bora.

5. Sababu tatu kwa nini viongozi ni muhimu sana.

Moja; viongozi ndiyo wenye jukumu la ufanisi wa taasisi wanayoongoza. Kushinda au kushindwa kwa taasisi kunatokana na maamuzi ambayo kiongozi wa taasisi hiyo anayafanya.

Mbili; mabadiliko yanayoendelea kwa kasi yanahitaji kuwa na mtu wa kuweza kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajaleta madhara makubwa. Kwa sehemu kubwa kiongozi anapaswa kuliona hilo mapema.

Tatu; kila taasisi kwa zama hizi inapimwa kwa uadilifu wake, kiongozi wa taasisi ndiye anayewajibika kwa uadilifu wa taasisi yake, kulingana na namna anavyoiendesha, watu anaowapa nafasi na kazi zinavyofanyika.

6. Maisha siyo njia iliyonyooka.

Kitu kikubwa kinacholeta changamoto kwenye uongozi ni kwamba maisha siyo njia iliyonyooka. Hakuna mipango ambayo inatokea kama ilivyopangwa. Hakuna hatua ambazo ukitoka moja unaenda nyingine. Mambo yanaweza kutokea kwa mpangilio ambao hata haueleweki. Bila ya kuwa na uongozi imara, taasisi inaweza kukosa uelekeo kwa mambo yanavyoenda zama hizi.

7. Hatua nne za kiongozi kuweza kufanikiwa kwenye dunia isiyoeleweka.

Kwa kuwa dunia tunayoishi sasa haieleweki, mipango haiendi kama tulivyopanga, viongozi wanaofanikiwa wanapitia hatua hizi nne;

Moja; wanajijua wao wenyewe, kwa kujua wanaweza kufanya nini na hawawezi kufanya nini.

Mbili; wanasikiliza sauti iliyopo ndani yako, kila mtu ana sauti ya ndani, ila wengi wamekuwa hawaisikilizi.

Tatu; kujifunza kutoka kwa mamenta sahihi, viongozi wanaofanikiwa wana watu ambao wanajifunza kutoka kwao.

Nne; kuongozwa na maono makubwa, bila ya maono makubwa, kelele zilizopo zinawapoteza viongozi.

8. Misingi mikuu ya viongozi wenye mafanikio.
Viongozi wapo wa kila aina na kila rangi, warefu, wafupi, weupe na weusi, vijana na 
wazee. Lakini wote wana misingi ambayo wanaifuata, misingi hiyo ni kama ifuatavyo;

Moja; wanaongozwa na maono makubwa, wanajua kabisa nini wanataka na kwa nini wanakitaka.

Mbili; mapenzi juu ya kile wanachofanya, haya ndiyo yanawasukuma kufanya.

Tatu; uadilifu ambao unahisisha maeneo matatu; kujitambua, uvumilivu na ukomavu.

Nne; uaminifu, ambalo ni zao la uadilifu.

Tano; udadisi na uthubutu, hii inawawezesha kugundua vitu vipya na kuchukua hatua kabla mabadiliko hayajawasumbua.

9. Viongozi siyo mameneja.

Kumekuwepo na tofauti nyingi kati ya viongozi na mameneja, lakini tofauti kubwa kabisa ni kwamba viongozi wanawawezesha watu kuwa bora zaidi huku mameneja wakiwasimamia watu. Tofauti nyingine ni kama ifuatavyo;

Mameneja wanasimamia, viongozi wanahamasisha.

Mameneja ni kopi, viongozi ni halisi.

Mameneja wanatunza hali kama ilivyo, viongozi wanaboresha hali iliyopo.

Mameneja wanakazana na mifumo na michakato, viongozi wanakazana na watu.

Mameneja wana mtazamo wa karibu, viongozi wana mtazamo wa mbali.

Mameneja wanauliza VIPI na LINI, viongozi wanauliza NINI na KWA NINI.

Mameneja wanakubaliana na mfumo kama ulivyo, viongozi wanabadili mfumo ili kuwa bora zaidi.

Mameneja wanafanya vitu kwa usahihi, viongozi wanafanya vitu sahihi.
Kuwa kiongozi, usiwe maneja.

10. Udhaifu ndiyo unaamua uongozi.

Lipo jambo moja la kushangaza sana kwenye uongozi na tabia. Viongozi bora kabisa huwa wanafanikiwa licha ya kuwa na madhaifu fulani kwenye maisha yao. Lakini pia, viongozi wabaya huwa wanafanikiwa kwa kutumia madhaifu yao.

Hivyo kama usipoyajua madhaifu yako vizuri, yanaweza kukupelekea ukafanikiwa kama kiongozi mbaya kuwahi kutokea. Lakini kama utayajua vizuri, unaweza kufanikiwa kuwa kiongozi mzuri.

11. Kazi kubwa ya kiongozi ni kujitengeneza yeye mwenyewe na kuiepuka jamii.

Jamii zetu huwa zinafanya kazi moja kubwa sana, kuhakikisha watu wote wanakuwa sawa. Kila mtu afanye kile ambacho kila mtu anafanya. Sasa ukienda na maisha hayo, kwa kufanya yale ambayo kila mtu anataka ufanye, huwezi kuwa kiongozi bora.

Ili uwe kiongozi bora lazima ujue ule utofauti uliopo ndani yako, lazima ujijue wewe mwenyewe vizuri. Lazima ujue maeneo gani uko vizuri na maeneo yapi una udhaifu, kisha kuchukua hatua ya kuwa bora zaidi.

12. Kujitabua na kujitengeneza hakuna mwisho.

Tunapokuwa watoto, tunatengenezwa na jamii, tunapelekwa shule, tunafundishwa majumbani na hata kwenye jamii. Tunapokuwa watu wazima, ndipo kazi ya kujitengeneza sisi wenyewe inapoanza. Kwanza tunahitaji kuanza kujitambua, maana jamii haikutupa fursa hiyo. Baada ya kujitambua ndiyo tunajitengeneza kuwa bora zaidi.

Sasa hili la kujitambua na kujitengeneza halina umri maalumu kama yale malezi mengine ya kwenye jamii. Wengine hupata fursa ya kujitambua na kujitengeneza wakiwa na miaka 

20, wengine mpaka wanafika miaka 50 wanakuwa bado hawajapata fursa hiyo. Na hata baada ya kujitambua, bado kujitengeneza kunaendelea, hakuna mwisho mpaka mtu anakufa.

13. Masomo manne muhimu kwenye kujitambua.

Kwenye kujitambua, yapo masomo manne muhimu unayopaswa kuyajua na kuyafanyia kazi.

Moja; wewe ndiye mwalimu bora zaidi kwako. Hakuna mwalimu anayeweza kukufundisha zaidi ya unavyoweza wewe mwenyewe.

Mbili; kubali majukumu yako, usimlaumu mtu yeyote. Ukianza kuwalaumu na kuwalalamikia wengine kuhusu maisha yako, bado hujajitambua.

Tatu; unaweza kujifunza chochote unachotaka kujifunza. Kama bado unasema huwezi kwa sababu hujui kitu fulani, kwa nini usijifunze? Dunia ya sasa unaweza kujifunza mwenyewe kila kitu.

Nne; uelewa wa kweli unatokana na kutafakari uzoefu wako. Kila kitu ambacho umewahi kupitia kwenye maisha yako, kina maana na mchango kwa hapo ulipo sasa. Unahitaji kupata muda wa kutafakari maana ya kila kitu na namna kimekufikisha hapo ulipo sasa.

Fanyia kazi masomo haya manne, ili uweze kujitambua na kuwa kiongozi bora.

14. Usichokielewa, siyo chako.

Kitu chochote ambacho hukielewi au hujakijua kwa undani, siyo chako. Hata wewe mwenyewe, kama bado hujajitambua, utaishia kutumiwa na watu wengine badala ya kujitumia wewe mwenyewe.

Unapaswa kuelewa kwa undani kila kinachohusiana na wewe, hapo ndipo unaweza kukitumia vizuri kwa mafanikio yako.

15. Katika kujifunza, unapaswa pia kufuta uliyojifunza.

Mambo mengi uliyofundishwa shuleni na hata kufundishwa na wazazi, yanaweza kuwa kikwazo kwako katika kufanikiwa kwenye uongozi. Kwa mfano huenda umeaminishwa njia pekee ya kufanikiwa kwenye maisha ni kupata ajira ya aina fulani. Hili unaweza kuwa unaliamini kabisa, lakini wewe unapenda vitu tofauti na kazi unayofanya.

Hapa unahitaji kujifunza upya kwa kuanza kufuta yale ambayo umejifunza kwa muda mrefu. Kwa njia hii utaanza kuona ukweli kwamba maisha ni kile unachotengeneza wewe, na watu wote hatufanani.

16. Wewe ni zao la kila kitu umewahi kukutana nacho kwenye maisha.

Kumekuwa na mabishano mengi, iwapo tabia za watu zinatokana na mazingira wanayoishi au ni za kurithi, tafiti zinaonesha kwamba, kila kitu tunachokutana nacho kwenye maisha yetu, kinachangia tabia zetu. Kuanzia jene tulizorithi, mazingira tunayoishi, familia, marafiki, biashara, matetemeko ya ardhi, shule, ajali, tv na redio, magazeti na chochote unachoweza kufikiria, kina mchango kwa hapo ulipo.

Hivyo unapotaka kujenga tabia nzuri za uongozi, angalia kwa umakini kila unachojihusisha nacho.

17. Hakuna mtu anayeweza kukufundisha wewe kuwa wewe.

Wazazi wako wamekazana sana kukulea, jamii nayo imekazana kukufikisha hapo ulipo, lakini wote walifanya kazi moja, kujaribu kukufanya wewe uwe kama wengine. Ndiyo maana shuleni ulifundishwa vitu sawa na wengine, nyumbani ulikuwa unalinganishwa na wengine.

Ili kuwa kiongozi bora, lazima kwanza wewe uwe wewe, kitu ambacho hakuna mtu yeyote hapa duniani anaweza kukufundisha ila wewe. Wazazi wako hata kama wanakupenda kiasi gani, hawawezi kukufundisha wewe kuwa wewe, kwa sababu hata wao hawakujui wewe halisi ni yupi.

Hili ni jukumu kubwa ambalo wachache huweza kulikamilisha na kuweza kuwa viongozi bora.

18. Viongozi bora wanaijua dunia inayowazunguka.

Ili kuwa kiongozi bora, lazima uweze kuijua dunia inayokuzunguka kama unavyojijua wewe mwenyewe. Lazima uwajue watu na mazingira tofauti na yale uliyozoea wewe. 

Katika kuijua dunia inayokuzunguka, unahitaji elimu pana na endelevu, kusafiri maeneo mbalimbali, kuwa na marafiki wa aina mbalimbali.

Ijue dunia zaidi ya hapo ulipo, hii itakuwezesha kuwa bora zaidi kwenye kile unachofanya.

19. Aina tatu za kujifunza kwenye uongozi.

Katika kujifunza zipo aina tatu;

Aina ya kwanza ni kujifunza kuendelea na kile ambacho watu wamezoea kufanya, hapa mambo yanakuwa yale yale.

Aina ya pili ni kujifunza kutokana na mabadiliko yanayotokea. Hapa mabadiliko yanatokea na kuvuruga mambo, watu wanachukua hatua ili kuokoa hali isiwe mbaya.

Aina ya tatu ni kujifunza kwa ubunifu, hapa watu wanajifunza ili kuwa bora zaidi kila siku.

Katika aina hizi tatu, aina ya tatu ndiyo wanaitumia viongozi bora na inawawezesha kuwa mbele ya mabadiliko.

20. Kusafiri kunakufanya ujijue na kuijua dunia vizuri.

Unaposafiri unavuruga yale mazoea ambayo umeshayajenga kwenye maisha yako ya kila siku. Hivyo kila unachofanya unapokuwa safarini, kinakuhitaji uwe makini sana ili usikosee au kupotea. Hali hii inakufanya utumie akili yako haswa badala ya kufanya kwa mazoea.

Kwa njia hii unajijua vizuri wewe mwenyewe na hata kuijua dunia pia, kwa kujua watu wa makabila na asili tofauti na namna wanavyoendesha maisha yao.

Mara zote nimekuwa nasema dunia ya sasa inatutaka sisi wote kuwa viongozi, kwa kuanzia kwenye familia yako, bila kuwa kiongozi, familia haiwezi kusimama, ukienda kwenye biashara, ili iwe na mafanikio, lazima uwe kiongozi mzuri.

Zingatia sana misingi hii tuliyojifunza kupitia uchambuzi huu wa kitabu, na pia nakusihi sana usome kitabu hichi, kwani yapo mengi mazuri.

Kupata kitabu hichi cha ON BECOMING A LEADER bure kabisa jiunge na kundi la telegram la AMKA MTANZANIA. Kujiunga bonyeza maandishi haya kisha join group. 

Hakikisha una program ya telegram kwenye kifaa chako.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles