Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Mambo Muhimu Ya Kufanyia Kazi, Ili Biashara Yako Iwe Na Mafanikio Makubwa.

$
0
0
Kufanikiwa katika biashara na kujenga mafanikio, sio jambo la muujiza bali ipo misingi ambayo kila mfanyabiashara awe mdogo au mkubwa akiifata misingi hiyo vyema, ni lazima biashara hiyo itakuwa ya mafanikio sana.
Tatizo la watu wengi hasa wanapoanza biashara, wanaanza pasi kujua misingi ya kuwasaidia kuweza kukuza biashara zao na kuwa kubwa na zenye mafanikio. Watu hawa hujikuta wakianzisha biashara kama kwa kubahatisha, matokeo yake huchukua muda mrefu sana mpaka kuweza kukuza biashara hiyo.
Kimsingi mafanikio,  yawe kwenye biashara au kitu chochote kile, kwa kawaida huwa hayaendi kwa kubahatisha, bali kwa kufuata misingi na kanuni husika. Hata biashara yako ili iweze kuwa kubwa inahitajika sana ujue mambo ya msingi yatakayofanikisha biashara yako.
Kwa kupitia nukuu kadhaa, ambazo zimeainishwa kwenye makala yetu hii ya leo, tunakwenda kujifunza mambo ya msingi ambayo ukiyazingatia, yatakusaidia sana kujenga biashara yenye mafanikio makubwa. Mambo hayo ni yapi, karibu tujifunze pamoja.

Fuata sheria za msingi ili kukuza biashara yako.
Kujenga uaminifu wa kibiashara.
Siri kubwa ya mafanikio ya biashara yoyote ipo kwenye uaminifu. Unatakiwa uijenge biashara yako kwenye misingi mikubwa sana ya uaminifu wa hali ya juu ili uweze kuikuza. Usipokuwa mwaminifu, elewa utabomoa kila kitu na hutafika mbali. Hakuna ambaye anapenda kufanya biashara na mtu ambaye sio mwaminifu.
Kujenga mahusiano na wateja wapya.
Pamoja na kwamba unawateja wako, lakini lazima uwe na mikakati ya kutafuta wateja wapya. Katika zoezi hili, sio lazima upate wateja wengi kwa pamoja, tafuta hata mteja mpya mmoja na jenga nae mahusiano mazuri, kisha wengine utazidi kuwapata taratibu. Hata uwe na wateja wengi vipi usiridhike, jenga mahusiano na wateja wengine, itakusaidia sana kukuza biashara yako.
Kutambua mahitaji ya wateja mapema.
Unapokuwa kwenye biashara yako, jenga utaratibu wa kuwasoma wateja wako mapema. Kama biashara yako ni ya kuuza vitu, usifanye biashara yako kwa kuridhika na kusahau mahitaji mapya wanayoyataka wateja wako. Ni vyema na muhimu sana ukajua vitu wanavyotaka watejwa wako na ukaviweka mapema.
Kutangaza bidhaa zako kwa ufanisi.
Siku zote tunaambiwa biashara ni matangazo, hilo ni ukweli na halina ubishi. Unataka biashara yako izidi kupaa na kukua, itangaze biashara yako. Unaweza kuanza kwa kuitangaza biashara yako kwenye mitandao ya kijamii na utashangaa biashara yako inapaa na kufikia ngazi kubwa ya mafanikio ambayo hukutegemea.
Kujibu maswali ya wateja vizuri.
Wakati upo kwenye biashara yako kuna maswali ambayo unakuwa unaulizwa sana na wateja wako. Sasa inapotokea unaulizwa maswali hayo, tafadhali usiwe na hasira, penda kujibu maswali hayo tena ikiwezekana uwaulize kama kunamaswali ya ziada. Jibu maswali hayo kwa biusara, maana kwa kujibu yatakusaidia sana kuweza kujua wateja wako wanataka nini kwenye biashara na itakufanya uwe mbobezi kwa ukifanyacho.
Kufanyia kazi mrejesho wa wateja.
Kile wanachokwambia wateja wako kuhusiana na huduma unayotoa au kile unachokiuza, ni busara na vyema sana kama utakuwa una utaratibu wa kukitolea mrejesho. Kama ni barua pepe jibu, kama ni simu jibu, kama kuna marekebisho yaliyopendelezwa yafanye, hiyo itakusaidia sana kukuza biashara yako kwa viwango.
Kwa kuzingatia mambo hayo na kuyachukulia hatua, hakuna ubishi utajikuta unakuza biashara yako na kufikia mafanikio makubwa sana ambayo hukuyategemea awali.
Ansante kwa kusoma makala haya na endelea kujifunza kupitia www.amkamtanzania.comkila siku kujifunza na kuboresha maisha yako.
Lakini kwa makala nyingine nzuri za mafanikio pia tembelea dirayamafanikio.blogspot.com kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuhamasika.
Nikutakie siku njema na mafanikio makubwa katika biashara yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,




Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles