Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Ushauri Kwa Wanaotegemea Kuanza Elimu Ya Vyuo Vikuu, Mambo Matatu Ya Kuzingatia Katika Kuchagua Kozi Ya Kusoma.

$
0
0
Habari rafiki?

Huu ni ule wakati wa mwaka ambao vijana waliomaliza kidato cha sita na hata watu wanaotaka kujiendeleza kielimu wanapochagua kozi za kusomea na hata vyuo gani. Najua mpaka sasa mengi yameshaandikwa kuhusiana na hili, lakini naomba na mimi nichomeke pua yangu kusema machache muhimu.


Sikuwa na mpango wowote wa kuandikia hili mwaka huu, kwa sababu karibu kila mwaka wakati kama huu nimekuwa naandika makala za aina hii, hivyo yeyote akitafuta makala za aina hiyo mtandaoni atakutana na zangu pia. Lakini simu za ndugu na jamaa zimekuwa nyingi wakitaka ushauri. Hivyo nimechukua nafasi na kuandika makala hii, nikiwa nina imani itamsaidia mtu kufanya uchaguzi sahihi kwake.

Kitu ambacho nimejifunza tangu mwaka 2008 nikiwa kidato cha sita mpaka sasa ni kwamba, ushauri wanaopewa vijana wengi wanaokwenda kujiunga na masomo ya vyuo vikuu siyo sahihi. Wengi wanashauriana wao kwa wao, na hivyo kukosa msingi mzuri au wanashauriwa na watu ambao wameshauriwa vibaya na hivyo kupata ushauri mbovu ambao unakuja kuwagharimu zaidi.

Kwa mfano, swali moja linaloulizwa sana kwa sasa ni; kozi gani nikisoma kuna uhakika wa ajira? Hili ni swali ambalo lilipaswa kuulizwa mwisho mwaka 2000, lakini kuuliza swali kama hilo kwa zama hizi, ni kutafuta kudanganywa au kuja kuwalaumu watu. Ukweli ni kwamba hakuna kitu chochote chenye uhakika kwa zama hizi. Siku za nyuma ilikuwa ukisoma ualimu au udaktari basi ajira ni uhakika. Sasa tuna walimu na madaktari wengi mtaani ambao hawajaajiriwa.

Hivyo kwenye makala hii, nimejikita kukupa wewe mtazamo tofauti kwenye kuangalia elimu hii ya juu, ambapo kama utautumia, utafanya maamuzi sahihi kwako.

Katika mtazamo huu wa tofauti ninaokwenda kukupa, nitakushirikisha mambo matatu mhimu ya kuzingatia ili kuchagua vizuri. Hapa sahau kuhusu ajira ya uhakika, angalia kwanza kupata elimu, halafu ujifunze namna ya kutumia elimu uliyopata kuboresha maisha yako na wengine.

Kigezo cha kwanza; MCHEPUO NA UFAULU WAKO.

Mchepuo uliosomea utaamua zaidi usomee nini katika ngazi ya chuo kikuu, hili kila mtu analielewa vizuri. Huwezi kusoma masomo ya sanaa sekondari na ukaomba kusomea udaktari chuo kikuu. Hivyo kwa masomo uliyochukua sekondari, yataamua aina za kozi unazoweza kusoma.

Kigezo kikubwa kipo kwenye ufaulu wako. Kama ufaulu wako ni mzuri, ina maana unaweza kuchagua kozi nyingi, zinazoendana na masomo uliyochukua ulipokuwa sekondari. Hivyo kama una ufaulu wa alama zinazohitajika katika kila kozi, una uhuru mkubwa wa kuchagua.

Kigezo cha pili; UWEZO WAKO WA KUJISOMESHA.

Zamani ilizoeleka baadhi ya kozi na kwa ufaulu wa juu, kupata mkopo wa kusoma elimu ya juu ilikuwa uhakika. Lakini sasa hivi mambo yamebadilika, upatikanaji wa mikopo umekuwa mgumu, hata kama mtu anasoma kozi zenye kipaumbele na ufaulu ni mkubwa.

Hivyo unapochagua kozi ya kusoma, angalia uwezo wako au wa wazazi/walezi wako kukusomesha kwenye kozi hiyo. Angalia kwenye kila chuo unachochagua, ada za kozi husika, mahitaji yote muhimu na gharama za maisha kwenye chuo husika.

Vyuo vyote vina mwongozo wa elimu kwenye chuo husika (prospectus), kabla ya kukimbilia kuomba, pata mwongozo huo na usome kwenye zile kozi ambazo unataka kusomea. Kama huna uhakika wa kupata mkopo kwa asilimia 100, na kama huna uwezo mkubwa wa kujisomesha, ni vyema kuchagua kozi na chuo ambacho hata kama hutapata mkopo unaweza kusoma kwa kujitegemea wewe mwenyewe.

Kigezo cha tatu; MAPENZI YAKO BINAFSI.

Baada ya kuangalia vigezo hivyo viwili hapo juu, sasa unaweza kuangalia wewe binafsi unapenda nini kwenye maisha yako. Na hili ni muhimu sana kwa sababu uhakika wa ajira haupo, hivyo ukisomea kitu ambacho unakipenda, utajituma sana na utafanya vizuri. Hata usipopata ajira, utaona njia za kutumia elimu yako kutengeneza kipato.

Pia kwa kupenda unachosoma, utajituma sana na kuwa tayari hata kujitolea, hilo litakuweka mbele zaidi na hata zikiwepo nafasi chache za ajira, wewe utakuwa na sifa bora zaidi. Ukisoma kitu ambacho unakipenda, utakuwa tayari kujituma sana, utaona fursa nyingi ambazo wengine wanaosoma ili tu kupata kazi hawawezi kuziona.

Mwisho kabisa; yote yakishindikana, soma chochote unachoweza kusoma.

Imani yangu huwa ni kwamba, hakuna elimu inayoenda bure. Hata kama hutafanyia kazi kile ambacho unasomea, yapo mambo mengi kuhusu maisha na mafanikio unayojifunza kwa kuwepo kwenye mfumo wa elimu. Kwa mfano nidhamu ya kuweza kufuatilia masomo, kufanya kazi unazopaswa kufanya mpaka kufaulu, itakuwezesha kufanya mambo mengi kwenye maisha yako.

Ushirikiano wako na wanafunzi wenzako utakufundisha namna ya kujenga mahusiano na ushirikiano bora na wengine. Pia kupitia elimu ya juu, unaweza kukutana na watu ambao mna mawazo yanayoendana, mkaungana na kuweza kufanya makubwa.

Muhimu hapa ni kuchukulia kila unachokutana nacho kama funzo. Umeonewa na wengine au hawa mwalimu, unajifunza kwamba maisha siyo wakati wote yako sawa. 

Umefaulu kwa juhudi unajua juhudi ni muhimu kwa mafanikio, umezembea ukafeli basi unajifunza ukiwa mzembe unashindwa.

Kwa vyovyote vile, kazana upate elimu, hata kama hakuna ajira, jifunze kwa sababu elimu itakufungua akili yako, na hiyo itakuwezesha kuziona fursa zaidi. Kwa kupata elimu ya chuo kikuu unajiweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kuchukua hatua zaidi. 

Lakini hilo linakupasa kuwa makini, na usiendeshe maisha yako kwa mazoea. Lazima uelewe kwamba elimu unayoipata ni mwanzo tu, unahitaji kuendelea kujifunza ziadi wewe mwenyewe ili kutengeneza yale maisha ambayo unayataka.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles