Habari za leo rafiki?
Linapokuja swala la fedha, kila mtu huwa anakuwa na hisia zake, lakini ukweli unabaki kwamba kila mtu anahitaji fedha ili maisha yaweze kwenda. Hata wale ambao wanasema kwamba fedha siyo kila kitu, usiku hawalali wakifikiria wanapata wapi fedha. Hivyo tukiweka unafiki pembeni, fedha ni muhimu sana.
Pamoja na umuhimu huu wa fedha, watu wengi hawana elimu sahihi ya fedha, wengi huwa wanafanya mambo kwa kuiga au mazoea, na hilo limekuwa linawaumiza sana.
Moja ya maeneo ambayo yanawaumiza sana watu kifedha ni matumizi, na kwenye matumizi yapo muhimu na ambayo siyo muhimu. Haya ambayo siyo muhimu ndiyo hatari kabisa kwa sababu wengi huwa hawayaoni haraka na kuishia kuwa mzigo kwao kwa sababu wanaendelea na maisha yao kwa mazoea.
Hapa nakwenda kukuonesha gharama ambazo zimekuwa zinakuzuia wewe kufikia utajiri, bila ya wewe mwenyewe kujua. Soma na uweze kuchukua hatua sahihi. Hii ni sehemu ya masomo ya semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA, niliyoendesha wiki mbili zilizopita, na nairudia tena kesho kwa wale walioikosa. Soma kipande hichi na kama utaona lipo la kujifunza, karibu kwenye semina.
Kwenye sehemu ya somo la leo tunaangalia gharama ambazo tunaingia kwenye maisha yetu, ambazo nazo pia zimekuwa zinachangia kwenye matumizi yetu na hivyo kupunguza nguvu yetu ya kufikia uhuru wa kifedha.
Zipo gharama nyingi ndogo ndogo, ambazo huwezi kuona madhara yake wakati unaingia, ila unapokaa chini na kupiga mahesabu ya gharama hizo, ndiyo unagundua ni kwa jinsi gani umekuwa unapoteza fedha, ambazo kama ungejipanga vizuri ungeweza kuziokoa na kuendelea kupata kiasi kizuri cha kujilipa wewe mwenyewe na hata kuwekeza zaidi. Gharama tunazokwenda kujadili leo ni ndogo ndogo sana kiasi kwamba unaweza kuzidharau lakini utakapopiga mahesabu yake kwa muda mrefu, utaona namna gani unapoteza fedha. Wahenga walisema tundu dogo linaloingiza maji kwenye boti, linaweza kuzamisha boti kabisa, hivi pia ndivyo ilivyo kwenye gharama, unaweza kuzidharau gharama ndogo, lakini madhara yake yakawa makubwa.
Ili kuzielewa vizuri, nitazigawa gharama hizi kwenye makundi Manne muhimu kulingana na ufanano wa gharama hizi.
Kundi la kwanza; gharama za miamala ya kifedha.
Maisha sasa hivi yamerahisishwa sana, kutuma na kupokea fedha imekuwa rahisi kupitia mabenki na hata mitandao ya simu. Huduma za kifedha za mitandao ya simu zinatuwezesha kutuma na kupokea fedha popote pale tulipo, iwe tupo eneo lenye benki au la. Tunapenda kutumia huduma hizi kutokana na urahisi wake, lakini tunasahau kwamba zina gharama. Hivyo kadiri tunavyotumia bila ya mipango, ndivyo tunavyoingia gharama kubwa zaidi.
Tuchukue mfano wa mfanyakazi, ambaye analipwa mshahara kupitia akaunti ya benki. Kwa kuwa labda yupo mbali na benki, anaona atoe fedha ile kwa njia ya simu, hivyo anahamisha fedha ile kutoka benki kwenda mtandao wa simu, hapo anakatwa fedha. Akishakuwa nayo kwenye mtandao wa simu, anakwenda kuitoa kwa wakala, huko nako anakatwa fedha ya kutoa. Sasa miamala hiyo miwili pekee, kama ni zaidi ya shilingi laki mbili, imeshamgharimu mtu karibu shilingi elfu 10. Kwa sababu kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu unakatwa karibu shilingi elfu 5, na unapokwenda kutoa kwa wakala tena unakatwa karibu elfu tano kutokana na kiwango unachotoa. Sasa hapo bado hujaenda kwa wakala wa kwanza akakuambia ana fedha kidogo, ukaenda wa pili naye akakuambia ana fedha kidogo, unapata akili, utoe kidogo kidogo kwa mawakala wote wawili, ili upate fedha ya kutosha. Na hapo unaweka gharama za kutoa mara mbili.
Ni imani yangu mabenki na mitandao ya simu yanatengeneza fedha sana kwenye huduma hizi bila hata ya watu kugundua hili.
Kila akaunti ya akiba uliyonayo benki, kila mwezi inakatwa fedha za matunzo. Kila unapoenda kuchukua fedha benki unakatwa gharama ya kutoa. Kila unapotumia ATM kutoa fedha unakatwa. Tena kila unapoingiza kadi unakatwa, kwa mfano kama unataka kutoa milioni moja, na kiwango cha juu ni kutoa laki nne, itakubidi uweke kadi mara tatu, mara ya kwanza laki nne, mara ya pili laki nne, mara ya tatu laki mbili, na hapo utakuwa umelipia siyo chini ya elfu 4 kwa kutoa hiyo milioni moja.
Watu wengine wamekuwa wanaacha fedha zao benki au kwenye mitandao ya simu ili kujizuia kuzitumia kwa urahisi, ila wanapopata shida, wanaenda kutoa kidogo kidogo, hapo wanazidisha gharama kwenye kupata fedha hizo.
Gharama hizi za miamala ya kifedha, ni gharama ambazo zinamwathiri kila mmoja wetu, kwa sababu kwa namna moja au nyingine tunatumia huduma hizi, na wakati mwingine ni muhimu sana. Hivyo tunachopaswa kufanya ni kuzitumia tukiwa tunapiga mahesabu vizuri na tukiwa tumeshahakikisha kwamba hakuna namna nyingine ya kufanya.
Mimi binafsi nilikuja kustuka siku moja namna ambavyo nilikuwa napoteza fedha nyingi bila hata ya kujua. Kwa kuwa kazi zangu zinahusisha mtandao wa intaneti, nimekuwa natumia mtandao wa halotel, ambao mtandao wake kwenye intaneti uko vizuri. Sasa siku za nyuma maeneo mengi walikuwa hawana vocha, na pia huduma ya halopesa ilikuwa haijasambaa vya kutosha. Wakawa wanatoa taarifa kwamba unaweza kuhamisha fedha kutoka benki kwenda halopesa, nikafurahi sana, nikijua tatizo langu la kupata vocha limeisha, kwa sababu nitatoa fedha benki, kupeleka halopesa, halafu nanunua vocha na kulipia intaneti. Sasa sikufikiria gharama ni kiasi gani, na kwa kuwa nalipia kwa huduma ya simu, sikuwa naletewa gharama za kutuma. Hivyo kila wiki nilikuwa natoa elfu kumi benki, kwenda halo pesa, halafu nanunua vocha kwa ajili ya kulipia intaneti. Siku moja nilienda kuomba statement ya benki benki ndipo nilipigwa butwaa, kumbe kila ninapohamisha elfu kumi, wananikata elfu mbili na mia tano. Niliona jinsi gani nimekuwa mzembe kwenye hilo na tangu wakati huo sijarudia tena zoezi hilo, nimejifunza kuweka fedha kupitia wakala hata kabla sijamaliza salio, na hiyo inapunguza gharama.
Kama unataka kuona ni kiasi gani cha fedha umekuwa unapoteza kwa kuhamisha hamisha fedha, nenda kaombe statement kwenye benki yako, na pitia kila muamala. Omba kwa mwezi mmoja au mitatu iliyopita, hilo pia lina gharama, lakini itakufungua macho.
Hatua za kuchukua ili kupunguza gharama za miamala ya kifedha.
1. Kumbuka kila unapotoa fedha kwa kutumia ATM au mitandao ya simu kuna gharama unalipa, hivyo usifurahie tu kutumia, piga mahesabu yako vizuri.
2. Toa fedha kwa wakati mmoja na jijengee nidhamu ya kukaa na fedha bila ya kuzitumia. Ukishapanga bajeti yako ya mwezi, nakushauri utoe kiasi hicho cha fedha benki na ukae nacho, au unaweza kutoa nusu na kutumia kisha kwenda kutoa tena nusu iliyobaki. kutoa kidogo kidogo kila unapohitaji unaingia gharama kubwa kuliko unayojaribu kuokoa.
3. Kama upo mbali na huduma za kibenki, na inakulazimu kutumia mitandao ya simu kutoa fedha, toa kiasi kikubwa kwa wakati mmoja, badala ya kutoa kidogo kidogo. Kutoa fedha kupitia mitandao ya simu kuna gharama kubwa uliko unavyotoa kupitia benki.
4. Kama unafanya biashara ambayo unalipwa kwa njia ya mitandao ya simu, usiende kutoa fedha kila unapolipwa, badala yake acha mpaka kifike kiasi kikubwa ndiyo utoe au kuhamishia benki. Kutoa kidogo kidogo kunakuongezea gharama.
5. Kabla hujatumia huduma ya ATM au mitandao ya simu kwenye miamala, jiulize kama kuna uwezekano wa kutumia njia nyingine, kama benki moja kwa moja au kulipana fedha taslimu.
Eneo hili la gharama za miamala ni la kuwa makini nalo, kwa sababu wengi wanapoteza elfu moja hapa, elfu mbili pale na kadhalika, ukihesabu kwa mwezi mtu anapoteza siyo chini ya elfu 10, ambayo hii angeiwekeza kwenye uwekezaji mdogo mdogo, angeanza kupiga hatua.
Kundi la pili; gharama za mawasiliano.
Rafiki, hilo ni eneo moja kati ya manne ambayo yanapoteza fedha zako kila wakati, bila hata ya wewe kujua. Fanyia kazi hilo moja, na nina hakika, kila mwezi utaokoa siyo chini ya shilingi elfu kumi.
Kama utapenda kujifunza zaidi kuhusu fedha, na mna ya kuongeza kipato, namna ya kudhibiti matumizi, kuwekeza, biashara na hata kuwajengea watoto msingi mzuri wa kifedha, karibu kwenye semina ya ELIMU YA MSINGI YA FEDHA.
Hii ni semina ambayo inafanyika kwa njia ya mtandao wa wasap, hivyo unaweza kushiriki ukiwa popote. Inafanyika kuanzia kesho jumapili mpaka jumapili inayokuja, kwa wiki moja. Masomo kumi kuhusu fedha yatafundishwa, utakuwa na nafasi ya kuuliza swali lolote kuhusu fedha.
Ada ya kushiriki semina hii ni tsh 10,000/= badala ya tsh 50,000/= ya mwanzo ambayo ndiyo mtu alipaswa kulipa ili kushiriki semina hii.
Kupata nafasi ya kushiriki, tume fedha tsh elfu 10 kwa namba 0717 396 253 au 0755 953 887 ukishatuma fedha, tuma ujumbe kwenye wasap namba 0717 396 253 wenye majina yako na utawekwa kwenye kundi la semina.
Mwisho wa kujiunga na semina hii ni leo na nafasi zipo chache. Chukua hatua sasa hivi rafiki yangu ili usikose nafasi hii ya kipekee.
Nina imani, kwa sehemu ya somo nililokushirikisha hapa pekee, unaweza kuokoa elfu kumi, ambayo utaitumia kupata masomo yote kuhusu fedha. Hivyo utakuwa hujapoteza chochote.
Karibu sana rafiki tupate elimu ya kujenga msingi imara wa kifedha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,