Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; How To Negotiate Better Deals (Mwongozo Wa Majadiliano Ya Kukuwezesha Kupata Mipango Bora).

$
0
0
Maisha ni majadiliano, kupata kile ambacho unakitaka, kwa namna unavyotaka wewe, utahitaji kujadiliana na wale wanaopaswa kukupa kile unachotaka. Na mara nyingi, hasa inapokuja kwenye biashara, mpango ambao watu wanakuambia kwa mara ya kwanza, siyo mpango bora kwako, unahitaji majadiliano ili kuweza kupata mpango bora, iwe ni bei au makubaliano mengine.


Mwandishi Jeremy Thorn, anatushirikisha mbinu muhimu za kutumia kwenye majadiliano ili tuweze kushinda na kupata kile ambacho tunakitaka. Hizi ni mbinu ambazo zinafanya kazi, na unapoweza kuzitumia vizuri, mara zote utanufaika.

Karibu tujifunze mbinu hizi, ili tuweze kujadiliana vizuri, tuweze kupata tunachotaka na pia kuepuka kuwanufaisha wengine bila ya sisi kunufaika.

1. Kwenye kila hatua ya maisha yako, utahitaji makubaliano ili kuweza kupata mpango mzuri wa kile unachotaka. Inawezekana kuwa ni kazi unatafuta, au biashara unauza, au vitu unataka kununua. 

Wakati mwingine ni kumshawishi mwenza wako, au wazazi wako, au watoto wako. Unapaswa kuwa na misingi sahihi ya kufanya hivyo ili uweze kupata mpango bora.

2. Fursa za majadiliano zipo kila eneo la maisha yako, popote unapofika, jua ya kwamba unaweza kujadiliana na kupata kilicho bora zaidi. Hata kama ni kazi mtu anakuajiri, mtahitaji kujadiliana ili aweze kukupa mshahara mzuri kwako. Hata kuwashawishi watu kukubaliana na mawazo yako, unahitaji kuwa na mbinu bora za majadiliano, ambazo zitawapa watu hao sababu ya kufanya kile unachotaka wafanye, bila ya kuona umewalazimisha au kuwashinikiza.

3. Majadiliano, hasa yale ya kibiashara, ni neno ambalo lina taswira hasi, wengi huona kama ni kuwaonea na kudhulumu wengine, hasa wale ambao hawana uwezo mzuri wa majadiliano. Lakini huo siyo ukweli, makubaliano yanawafikisha watu wote wawili kwenye hatua nzuri kwenye lolote wanalofanyia kazi.

4. Watu wengi wamekuwa wanaogopa kuanzisha majadiliano, wakihofia watu watawachukuliaje. 

Kwa mfano pale unapotaka mtu akupunguzie kitu kama unataka kununua, au kutaka mtu akulipe zaidi kama unauza. Ukweli ni kwamba anayeuza, au anayenunua kwako, tayari anategemea uwe unataka kupata zaidi, hivyo ana kiwango chake cha kukuruhusu wewe upate zaidi. Huwezi kukijua kiwango hicho, kama wewe mwenyewe hutakuwa tayari kutaka zaidi. Hivyo mara zote uliza kupata mpango bora zaidi, iwe ni kwenye bei au makubaliano mengine.

5. Kuwa na akili au ujanja sana hakusaidii kwenye majadiliano, hii ni kwa sababu majadiliano ni uzoefu na ujuzi zaidi kuliko ujanja na akili. Ndiyo maana unahitaji kujifunza na kufanyia kazi mbinu za majadiliano, ili kuweza kuwa bora zaidi.

6. Majadiliano ni asili yetu sisi binadamu, ukitaka kujua hilo, waangalie watoto wadogo. Mtoto anapotaka kitu, atang’ang’ana mpaka ahakikishe amekipata. Wewe kama mzazi unaweza kumkatalia na kumkatisha tamaa, lakini yeye ataendelea kung’ang’ania mpaka utafika hatua ya kumpa ili asikusumbue. Japokuwa huhitaji kuwa msumbufu kama mtoto, lakini unapaswa kujua unataka nini, na kuhakikisha unakipata.


7. Kabla hujaingia kwenye majadiliano ya kupata mpango bora, lazima kwanza wewe mwenyewe uwe na nguvu ya maafikiano, yaani uwe na kitu ambacho mwingine anakitaka, hivyo kuwa tayari kujadiliana na wewe. Kwenye biashara maana yake uwe na bidhaa au huduma bora sana ambayo mteja anaihitaji, au uwe na fedha za kuweza kulipa kama ni mteja. Kwenye kazi maana yake uwe na kitu ambacho yule anayetaka umfanyie kazi anakihitaji. Kama huna nguvu hiyo, usijisumbue kuingia kwenye majadiliano, hakuna atakayepoteza muda na wewe.

8. Zipo aina tatu za majadiliano, kulingana na matokeo ya mwisho ambayo mtu unayataka;

Aina ya kwanza ni USHIRIKIANO, hapa kila mtu anapata kitu kwenye majadiliano hayo na hivyo kuimarisha ushirikiano zaidi. Hii inaitwa WIN - WIN DEGOTIATION. Kila upande unaondoka ukiwa umenufaika.

Aina ya pili ni USHINDANI, hapa upande mmoja unashinda na upande mwingine unashindwa. Hii inaitwa WIN – LOSE NEGOTIATION. Hii ni hali ya ushindani mkali, ambapo ili mmoja ashinde, lazima mwingine ashinde.

Aina ya tatu ni LOSE – LOSE negotiation, hapa kila mtu anapoteza. Hii inafikia pale kila upande unapotaka kushinda na hakuna anayetaka kupoteza, mwishowe wote wanapoteza.
Kila aina ni muhimu kulingana na aina ya majadiliano unayofanya.

9. Kwenye WIN – WIN, hapa ni majadiliano ambayo yanaimarisha ushirikiano, hasa kwenye biashara au makubaliano ya kikazi. Kupitia majadiliano haya, kila mtu anaridhika na mnakwenda pamoja. Haya ni majadiliano ya kuyapa kipaumbele kwa kila mtu, kwa sababu mwisho wa siku, ushirikiano ni bora zaidi.

Kwenye WIN – LOSE negotiation, inabidi wewe ukazane kushinda, kwa namna yoyote ile. Hapa ni yale majadiliano ambayo mtu mwingine anataka kunufaika zaidi, au huhitaji ushirikiano wowote baada ya makubaliano. Majadiliano haya huwa ni makali na yanahitaji uwe vizuri vinginevyo unaweza kupoteza.

10. Ipo aina nyingine ya majadiliano ambayo inaitwa DEADLOCK, hapa majadiliano yanakuwa yamegota na hayawezi kwenda mbele, kwa sababu kila upande unataka kushinda na hakuna anayetaka kushindwa. Hivyo majadiliano yanakwama na kuchukua muda mrefu. Unapojikuta kwenye majadiliano ya aina hii, unahitaji kutafuta nguvu kubwa zaidi ya kufanya upande wa pili kuchukua muda. Labda kuweka ukomo wa muda, kwamba kama mpaka kufikia wakati fulani makubaliano yatakuwa hayajafikiwa basi utajiondoa kwenye majadiliano hayo.

11. Unapoingia kwenye majadiliano, usiende na mtazamo hasi juu ya upande unaojadiliana nao. Kwa kufanya hivyo, utapata kile ambacho kipo kwenye mawazo yako. Kwa mfano kama unaenda kujadiliana kuhusu mshahara, na wewe ukajiambia naenda tu lakini najua hawawezi kukubali ninachotaka, huo ndiyo utakuwa ukweli. Kwa sababu hata namna unavyojadiliana, itawaonesha kama kweli unataka unachotaka. Nenda ukijiamini na ukiamini upande wa pili utakuwa tayari kukupa kile unataka, na mara nyingi inakuwa hivyo.

12. Inapotokea mabishano yameibuka katika majadiliano, unahitaji kuwa makini sana, maana mabishano usipoyafanya vizuri, yanaweza kuharibu kila kitu. Zifuatazo ni sheria za mabishano ambazo zitakuwezesha kushinda;

Moja; toa pointi chache kwa wakati, usiseme kila kitu, sema kiasi kisha nyingine utatoa wakati wengine wametoa pointi zao. Ukishasema kila kitu utabaki huna cha kusimamia.

Mbili; sikiliza kwa makini ili uweze kuelewa upande wa wengine ukoje, usiwakatishe watu wanapokuwa wanaongea. Unaposikiliza utaona sehemu nyingi za kuweza kuwashinda.

Tatu; tengeneza kesi yako vizuri, pangilia pointi zako kwa njia ambayo zitaleta ushawishi.

13. Katika majadiliano, unapaswa kutengeneza ushawishi, watu wakubaliane na kufanya kile unataka, kwa matakwa yao wenyewe badala ya kuona kama wanalazimishwa. Ili kujenga ushawishi, fuata sheria hizi tatu;

Moja; weka mkazo kwenye maeneo ambayo mnakubaliana, yale ambayo yana manufaa kwa kila mtu. 

Hakuna mtu ambaye hapendi kunufaika.

Mbili; uelewe upande wa pili, elewa kile anachotaka na onesha kujali. Usijiangalie tu wewe na kusisitiza kile unataka, bali onesha upande wa pili kwamba unaelewa wanachotaka na upo tayari kuwasaidia kwenye hilo. Siyo lazima kukubaliana nao kwa kila kitu, ila unapoonesha kujali, wanaona mpo upande mmoja.


Tatu; jua kwanza upande wa pili unaamini nini kwenye kile mnachojadiliana kabla hujatoa msimamo wako. Kwa njia hiyo utaweza kujua namna gani ya kuegemea upande wa wanachoamini na kusimamia, ili wewe uweze kupata unachotaka.

14. Katika majadiliano, ipo dhana inaitwa GAME THEORY SOLUTION. Kwa dhana hii, unapoingia kwenye majadiliano, ingia kwa mpango wa WIN – WIN, ukiangalia namna gani kila mtu anaweza kunufaika. Lakini kama upande wa pili utakuja na mpango wa WIN – LOSE, basi na wewe badilika na uingie kwenye WIN – LOSE. Na unapoingia kwenye WIN – LOSE, hakikisha unapambana hasa ili kupata kile unachotaka, kwa kuwa na mpango mzuri wa kuwashawishi watu kuchukua hatua.

15. Unapoamua kwenda na win – lose negotiation, zingatia yafuatayo;

Eleza wazi ni nini hasa unachotaka wewe.

Usikubali upande wa pili uoneshe unasimamia nini.

Upe upande wa pili njia rahisi ya kuondoka kwenye majadiliano hayo.

Kuwa tayari kutoa kitu kidogo cha kuridhisha upande wa pili, kwa sababu win – lose haimaanishi wewe ushinde halafu upande wa pili ukose kila kitu, hiyo itakuwa ni vita. Kwenye lose inamaanisha upande wa pili haupati kama ulivyokuwa unataka, ila wanapata kidogo.

16. Unapoamua kwenda na win – win, zingatia yafuatayo;

Eleza upande wa pili wazi kabisa kwamba msimamo wako ni kila mtu ashinde.

Anza na tatizo badala ya suluhisho, tatizo ambalo linaathiri pande zote.

Tengeneza mazingira ya kuheshimiana kwa pande zote mbili.

Shirikisha taarifa sahihi kwa upande wa pili, ili wajenge kukuamini.

Epuka kujitetea na kutoa lawama kwa upande wa pili, kufanya hivyo na wao wataingia kwenye kujitetea.

17. Ili kuweza kunufaika na majadiliano yoyote yale, unapaswa kuuelewa upande wa pili vizuri sana. 

Elewa wanachosimamia, elewa mahitaji yao, elewa madhaifu yao, na elewa kipi kinaweza kuwasukuma kuchukua hatua. Wakati huo tengeneza msimamo wako vizuri, hakikisha kuna kitu wanatoa kabla wewe hujakubali kutoa kitu.

18. Ili kuwa mtu ambaye anafanikiwa kwenye majadiliano, kuna hizi P nne ambazo unapaswa kuzizingatia;

POSITIVE, lazima wakati wowote wa majadiliano uwe kwenye mtazamo chanya kwako na kwa upande wa pili.

PATIENT, lazima uwe mvumilivu, mambo mazuri hayataki haraka.

PLACID, unahitaji kuwa mtulivu na usiyumbishwe, pia jaribu kuuyumbisha upande wa pili, maana watu wakishakosa utulivu, hufanya maamuzi ambayo siyo bora.

PREPARE, maandalizi ni muhimu sana, usiende kwenye majadiliano hujajiandaa vya kutosha, na kujua kwa kina kila kinachohusika. Jua upande wa pili watajaribu kukulaghai kwa njia zipi, na zipatie majibu.

19. Chagua wakati wako wa majadiliano vizuri sana. fanya majadiliano yako wakati wewe thamani yako iko juu kuliko upande wa pili, na isiwe kinyume na hapo. Kwa mfano huwezi kwenda kuomba ongezeko la mshahara, siku moja baada ya kupewa barua ya onyo kwa makosa uliyofanya kazini. 

Kadhalika usitake mteja alipe zaidi wakati umeshindwa kutimiza kitu ulichomwahidi. Taka zaidi pale ambapo upande wa pili unakutegemea zaidi.

20. Uliza mara mbili ya kile unachotaka, au toa nusu ya kile ambacho upande wa pili unataka. Kwa mfano, iwapo mtu amekuambia anataka kukulipa elfu 10 kwa kile unachotoa, mwambie unahitaji elfu 

21. Kwa njia hii mkijadiliana, utaishia kupata elfu 15. Kadhalika kama mtu anataka umlipe elfu 10, mwambie utamlipa elfu 5, na mkijadiliana utaishia kulipa elfu 7 na mia 5.

Usione aibu kutoa kiwango cha juu kwa unachotaka kupata au cha chini kwa unachotegemea kutoa. 
Ila inabidi uwe na mpango na uwe tayari kukubali mnapofikia kile kiwango rafiki kwako. Tofauti na hapo watu watakuona ni msumbufu na usiyejali. Onesha wazi nia yako ya kutaka kufikia makubaliano na mtayafikia.

Haya ni mambo muhimu ya kuzingatia kwenye majadiliano ili uweze kupata mpango bora kabisa kwako kwenye jambo lolote unalotaka kwenye maisha yako. Yazingatie ili uweze kupata unachotaka, huku ukiimarisha mahusiano na ushirikiano wako na wengine.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>