Yapo mambo ambayo yanatakiwa kujulikana mapema sana karibu kwa kila mtu katika maisha yake. Lakini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo pamoja na mazingira mambo hayo huchelewa sana kujulikana.
Kwa kuchelewa huko, ni chanzo kimojawapo cha watu hao kuweza kuishi maisha ya majuto na kujilaumu na kushindwa kwingi. Pengine kama watu wangeyajua mambo hayo mapema wasingeweza kuishi maisha ya namna hiyo.
Leo katika makala haya, nataka nikushirikishe mambo ya msingi kabisa ambayo wengi huchelewa kuyajua kwenye maisha yao. Lakini wewe kupitia makala haya nataka uyajue mapema na kuyafanyia kazi na kuleta mabadiliko ya maisha yako..
Jambo la kwanza, Kujitambua mapema.
Kati ya kitu ambacho wengi huchelewa kukijua ni kule kujitambua mapema. Wengi hushindwa sana kuelewa nini wafanye kwenye maisha yao, au ni nini ambacho wanatakiwa kuwajibika nacho kwa wakati husika.
Matokeo yake, wengi hushtuka umri umekwanda na kuanza kupiga kelele 'alaa kumbe maisha yalitakiwa yaende hivi au vile'. Na wanapokuja kugundua hilo pia huanza kuona tena kama wamechelewa mambo mengi sana ya kimaisha.
![]() |
Kujitambua mapema ni chanzo cha kufanikiwa mapema pia. |
Kujitambua mapema ni moja ya elimu ya msingi sana ambayo unatakiwa uipandikize kwa watoto wako haraka iwezekanavyo ili kuwajengea msingi bora wa mafanikio. Kukosa kujitambua mapema ni chanzo cha kutengeneza anguko la maisha yako.
Jambo la pili, umuhimu wa kuishi sasa.
Kitaalamu, msongo mkubwa wa mawazo unasababishwa sana na kuishi jana na wasiwasi mwingi wa maisha unasababishwa na mtu kuishi kesho zaidi. Ili kuepuka yote hayo, jifunze kuishi maisha yako kwa KUISHI SASA.
Usiendelee kufanya kosa la kujitesa maisha yako yote kwa kutokuishi sasa. Wengi pia huchelewa kulijua hili kwamba wanatakiwa kuishi sasa na matokeo yake utashangaa ni watu walioishi kwa mateso na kwa muda mrefu sana.
Jambo la tatu, kila kitu kipo kwa muda.
Wapo watu ambao hufanya mambo yao kama vile wataishi milele duniani na ni Kitu ambacho kipo wazi na kinasahaulika na wengi pia. Unatakiwa kukumbuka kila kitu kipo kwa muda tu na wala hakuna kitu cha kudumu.
Kwa hiyo, unapofanya mambo yako usijasahau katika hili, fanya kwa uhakika mkubwa sana kama vile hutakuja kufanya tena. Hiyo iko hivyo kwa sababu kila kitu kipo kwa muda. Jikumbushe hili kila siku na litakusaidia katika safari yako ya mafanikio.
Jambo la nne, kufanya kile unachokipenda.
Chanzo kingine kikubwa cha uvivu kinatokana na watu wengi kufanya yale mambo wasiyoyapenda na matokeo yake kushindwa kabisa kupata matokeo chanya. Wengi pia huchelewa kujua hili na kujikuta wamefanya mambo ya hovyo wasiyoyataka.
Kutokana na kufanya mambo ambayo wanaona hayakuwa sio yao hivyo hujikuta ni watu wa kujuta sana na kuumia kwa nini hawakujua mwanzo na kujiingiza katika mambo ambayo ni kama yamewaangusha au kuwapotezea muda.
Hayo kwa kifupi ndio mambo manne ambayo watu huchelewa sana kuyajua katika maisha yao na ambayo baadae husababsha majuto sana kwa kujilaumu kwa nini hawakujua siri au mambo hayo mapema.
Fanyia kazi haya ili upige hatua mbele ya kuelekea mafanikio ya maisha yako na kila la kheri katika kufikia mafanikio yako makubwa.
Kwa makala nyingine nzuri za maisha na mafanikio tembelea dirayamafanikio.blogspot.
com kila siku kwa ajili ya kujifunza na kuhamasika.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani Ngwangwalu,
Mshauri wa mafanikio, mwandishi na mjasiriamali,
Website, www.amkamtanzania.com
Mawasiliano; +255 767 048 035, +255 713 048 035,
Email; dirayamafanikio@gmail.com