Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Mambo 29 Niliyojifunza Kwenye Miaka 29 Ya Maisha Yangu Hapa Duniani.

$
0
0
Habari za leo rafiki yangu,

Jana tarehe 28/05/2017 ilikuwa siku yangu ya kuzaliwa ambapo nilitimiza miaka 29 hapa duniani. Nilizaliwa tarehe kama hiyo mwaka 1988. Kwa wale ambao hatujuani zaidi labda hatujawahi kukutana au siyo mwanachama wa KISIMA CHA MAARIFA, basi huenda ukashangazwa na umri huo. Huenda ulitegemea umri wangu ni mkubwa zaidi, lakini ndiyo huo, na una haki ya kushangaa.
 

Nina mengi sana ya kushukuru kwenye maisha yangu, kuanzia kwa wazazi wangu, jamii inayonizunguka na kwa kila mtu ambaye nimewahi kukutana naye kwenye maisha yangu. 

Nina mengi zaidi ya kushukuru kwenye kila tukio ambalo limewahi kutokea kwenye maisha yangu, zuri au baya, yote yamenifikisha hapa nilipo sasa.

Katika siku yangu hiyo ya kuzaliwa, marafiki wengi wamenitumia salamu nyingi na zuri. 

Salamu hizi zimenifariji sana kwa sababu marafiki ni watu muhimu kwenye maisha ya mtu yeyote yule.

Huwa sina utaratibu wa kufanya sherehe kwenye siku za kuzaliwa, ila nachukua muda kutafakari maisha yangu, nilipotoka, nilipo na ninapokwenda. Na jana nimefanya zoezi hilo na kukuandalia mambo haya 29 niliyojifunza kwenye miaka 29 ya maisha yangu hapa duniani. Najua bado ni umri mdogo na nina mengi sana ya kujifunza miaka inayokuja, na hivyo nitakuwa nakushirikisha kila mara kadiri ninavyojifunza.

Mambo haya 29 ninayokushirikisha, ni yale ambayo yanagusa maisha yangu moja kwa moja, ambayo huenda sijawahi kukushirikisha kwenye kazi zangu nyingine.

Mipango yangu mikubwa miwili ya maisha yangu bado ni ile ile, KUWA BILIONEA KABLA YA MWAKA 2030, na KUWA RAISI WA TANZANIA MWAKA 2040. Naomba usianze kuleta ubishi kwenye hayo, maana wakati natangaza hayo mara ya kwanza mwaka 2014 wapo watu walipinga sana na kusema niachane na ndoto hizo, lakini sijui hata leo hii wako wapi, na mimi ndoto zangu zipo hai na kila siku nazipigania. Hivyo kama una wasiwasi wowote juu ya ndoto hizo, nakushauri usubiri muda ufike na uone kipi kitakuwa kimetokea, ila tu sina wasiwasi juu ya hayo mawili.

Baada ya hayo machache, basi moja kwa moja nikuletee mambo 29 muhimu niliyojifunza kwenye maisha mpaka sasa.

1. Hakuna anayejua anachofanya.

Kwa kifupi dunia ni ngumu kuielewa kuliko watu wanavyodhani wanaielewa. Nimekuwa najifunza kupitia watu, waliopita hapa duniani na waliopo hai, na ninachokiona ni kwamba hakuna anayejua anachofanya. Kila mtu anajaribu kuwa bora, kuwa wa msaada kwa wengine na kuacha jina hata atakapoondoka. Unaweza kuona watu kwa namna wanavyoonekana nje, au kwa ujuzi na uzoefu walionao na ukafikiri wana majibu ya kile unachotaka, kumbe hata wao wanakazana kupata majibu.

Hivyo kama kuna wakati kwenye maisha yako unajiona kama unapotea hivi, usiogope, ndivyo maisha yalivyo. Kumbuka misingi, kila siku kazana kuwa bora zaidi, kuwa wa msaada zaidi na kuacha jina, kupitia chochote unachofanya.

2. Unapokuwa huna pa kuanzia, anzia pale ulipo, kwa kile unachoweza kufanya.

Mwaka 2011 nilifukuzwa chuo kikuu, baada ya kushiriki kwenye maandamano ya kutetea haki zetu kama wanafunzi. Nilirudi mtaani sina popote pa kuanzia. Ulikuwa wakati mgumu sana kwenye maisha yangu. Lakini sikukata tamaa, bali niliangalia wapi naweza kuanzia. 

Nilikuwa naweza kufundisha masomo ya sayansi, hivyo nikaomba kufundisha kwenye shule za sekondari. Pia nilikuwa na kompyuta na uwezo wa kuingia intaneti, nikaanza kujifunza kila nilichokuwa nakutana nacho. Nikasoma na kuangalia masomo mengi mno, nikajifunza mwenyewe kutengeneza website, blog na program nyingine za kompyuta, bila ya kuelekezwa na mtu yeyote. Na mpaka sasa ni ujuzi unaoniwezesha kutengeneza kipato.

Hata kama upo chini kiasi gani, anzia hapo ulipo.

3. Amini kwenye kile unachotaka kufikia, kiishi na utakifikia.

Mwaka 2007 wakati nachaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano na sita shule ya sekondari kibaha, niliweka lengo moja, kupata ufaulu wa daraja la kwanza kwa alama tatu (division one ya point 3), yaani kupata alama A kwenye masomo matatu niliyosoma, Fizikia, Biolojia na Kemia. Watu walinipinga na kuniambia najisumbua, siwezi kupata matokeo hayo, na niache kujitesa. Mwaka 2009 matokeo yalipotoka, nilipata kile nilichopanga.

Kama kuna kitu unataka, amini na weka juhudi, hata kama kila mtu anakuambia huwezi, achana naye, wewe weka juhudi, utapata kile unachotaka.

4. Ukikataliwa usirudi nyuma, badala yake songa mbele.

Mwaka 2013 baada ya kuanza kuandika makala kwenye blog ya AMKA MTANZANIA, kuna watu waliniambia makala zako ni nzuri sana, peleka kwenye magazeti na zitachapwa. 

Nikaenda kwenye gazeti moja na kupeleka makala, mhariri akaniambia ni kweli makala zako nzuri, ila wewe ni nani? Una jina gani? Basi ikawa imeishia pale, hazikuchapwa. Hivyo nikarudi na kusema kama wamekataa kwa sababu sina jina, basi nitatengeneza jina kupitia blog yangu hii. Nikaendelea kuandika kila siku, mpaka baadaye magazeti ndiyo yakawa yananitafuta niwape makala zangu wachape.

Ukikataliwa usirudi nyume, endelea kuweka juhudi kubwa zaidi.

5. Msimamo unalipa sana.

Nilipoanza kuandika makala kuhusu maendeleo binafsi na mafanikio kupitia blog ya AMKA MTANZANIA, wasomaji walikuwa wachache sana. Unaandika na wala hakuna anayekutafuta wala kutoa mrejesho wa kazi zako. Na wakitokea wa mrejesho basi unakuwa mrejesho hasi kiasi kwamba unaweza kukata tamaa. Lakini mimi niliendelea, kwa sababu kuandika ni kitu ambacho nilikuwa napenda kufanya. Baadaye watu wengi walikuja kununua maarifa zaidi ninayotoa, niligundua ni watu waliokuwa wananifuatilia kwa muda mrefu, baada ya kuona nipo na siondoki, wakaniamini na sasa tupo pamoja.

Chochote unachofanya, kuwa na msimamo, fanya hata kama hakuna anayekuangalia, wapo watu wanakufuatilia bila ya wewe kujua, wakiona bado upo, wataungana na wewe, ila kama unajaribu na kuacha, hutakuja kupata mtu.

6. Kila kitu kina gharama kwenye maisha.

Niliposhiriki kwenye mgomo ulipelekea kufukuzwa chuo kikuu, sikuwa nimeelewa somo hili hapo kabla. Kwamba vipo vitu ambavyo vinakuwa sahihi kabisa mtu kufanya, lakini vinakuja na gharama. Hivyo unapofanya kitu, lazima ujue ipo gharama utalipa, hata kama ni kitu kuzuri kwa wengine.

7. Wapo watu watakupinga bila sababu ya msingi.

Kupitia kazi ya uandishi na kufundisha wengine mbinu bora za kuwa na maisha bora, nimekutana na watu wengi wanaonipinga bila hata sababu ya msingi. Yaani mtu hakujui unatoka wapi na unaenda wapi, lakini anakupinga tu na kukuambia maneno ya kukatisha tamaa. Mwanzo nilikuwa naumia sana kwa watu wa aina hii, lakini sasa hivi wala hawanisumbui, najua wapo na huwa najiambia hivi; KILA MTU NA AFANYE KAZI ALIYOCHAGUA KUFANYA. MIMI NIMECHAGUA KUWASHIRIKISHA WATU MAARIFA SAHIHI, NITAFANYA HIVI, WAPO WATU WALICHAGUA KUPINGA, NA WAO WATAFANYA HIVYO. Muda ndiyo utakaoamua nani atakayeshinda kwenye kile anafanya.

8. Huwezi kuwaridhisha watu wote hata ufanye nini.

Yapo mengi nimejifunza mpaka wakati mwingine huwa nacheka nikikumbuka, au nikikutana na hali ya namna hii.

Nimekuwa naendesha semina mbalimbali kwa njia ya mtandao, kwa sababu ya watu wanaofuatilia masomo yangu kuwa sehemu mbalimbali. Wapo wanaosema semina za mtandao siyo nzuri, tunataka za kuhudhuria. Tukaandaa ya kuhudhuria, wengi wakasema zinafanyika dar, wengine tupo mikoani. Na hata waliopo dar wengine wakasema wamebanwa na kazi.

Kwenye vitabu pia, nimekuwa natoa vitabu kwa mfumo wa nakala tete na nakala za kawaida, watu watakuambia nakala tete hawaziwezi, ukiwapa za kawaida wanakuambia wapo mbali.

Kadhalika kwenye huduma za kulipia, nimekuwa na huduma kuu ya kulipia ya KISIMA CHA MAARIFA, ada ni elfu 50 kwa mwaka. Wapo wanasema ada ni kubwa na wangependa kulipa kidogo kidogo. Ukiwapa nafasi hiyo ya kulipa kidogo kidogo wanakuja na sababu nyingine. Wale ambao hawawezi kabisa nawaambia kuna makala zaidi ya elfu moja kwenye AMKA MTANZANIA, wanaweza kusoma bure kabisa, lakini bado watakuja na sababu.

Hivyo nilichojifunza ni kuangalia nawalenga watu gani na kuona njia ya kuwafikia hao. 

Wengine watakuja na malalamiko, lakini sitakuwa na la kuwasaidia.

9. Uaminifu unalipa, uaminifu ni mtaji.

Mwaka 2015 kupitia kundi la KISIMA CHA MAARIFA, lilitokea wazo la kuanzisha kampuni ya pamoja, kwa watu wote ambao tupo kwenye kundi na tunajifunza pamoja. Wachache tukakubaliana kwenda mbele na wazo hilo. Na kila mtu kuchagua kiasi ambacho anaweza kuchangia kwenye mtaji wa kampuni yetu hiyo mpya. Changamoto kubwa ilikuwa hatujawahi kukutana wote kwa pamoja, hivyo wengi wamekutana kwenye kundi kupitia mimi. Kwa sababu ya uaminifu ambao nimeweza kujenga kupitia kazi hizi, watu waliniamini na kuwa wanatuma michango yao kwenye akaunti yangu binafsi mpaka tuliposajili kampuni na kuwa na akaunti ya kampuni. Leo baada ya miaka miwili, tumeweza kuichanga mtaji za zaidi ya milioni 100, tuna mashamba mawili, hekari 30 mbozi ambazo tunalima maparachichi na hekari 20 mkuranga ambapo tunalima maembe, mananasi na kufuga kuku. Yote haya yamefanyika kwa uaminifu pekee, na siyo kitu kingine.

Uaminifu ni muhimu sana kwenye maisha, fanya kila jambo kwa uaminifu wa hali ya juu. 

Itakusaidia sana.

10. Huhitaji ‘connection’, unahitaji kazi.

Watu wengi, hasa vijana wamekuwa wakiamini sana kwenye ‘connection’, yaani kuwa na watu wa kuwaunganisha na watu ambao wanataka kukutana nao, hasa kama wapo juu. 

Kwenye maisha yangu mpaka hapa nimefika, siamini kwenye connection, badala yake naamini kwenye kazi. Kama kuna mtu nataka kumfikia, ninachofanya ni kufanya kazi ambayo anaihitaji sana kwenye kile anachofanya. Hivyo ninapoenda kwake na kitu kitakachomsaidia, hiyo inakuwa connection nzuri zaidi.

Weka kazi, tena siyo kazi ndogo, toa thamani kubwa kwa wengine, na thamani yako itakufikisha popote unapotaka.

11. Huhitaji ufadhili, unahitaji kazi.

Kitu kingine ambacho nimekuwa naona kwa watu ni hichi cha kulalamika kwamba hawajapiga hatua kwa sababu wamekosa ufadhili, labda serikali haijawawezesha. Mimi nimekuwa sielewi hii sababu watu wanaitoa wapi, kwa sababu kitu pekee ninachoamini kitanipa chochote ni kazi. Na pale ambapo sina pa kuanzia, naanzia popote pale nilipo. 

Nimefundisha shule za sekondari, nimefundisha kwenye vyuo vya kari, nimefundisha tuisheni za nyumba kwa nyuma. Nimefanya kila ninachoweza kufanya, kuongeza thamani kwa wengine, na mara zote kazi ninayofanya inazaa matunda.

12. Watu wakikupinga kwa kikubwa unachopanga kufanya, wewe fanya, usipige nao kelele.

Mwaka 2014 kwenye kujifunza kupitia kazi za watu mbalimbali, nilikutana na ushauri huu, kwamba ili uwe mtu bora na uliyebobea kwenye jambo lolote, unahitaji kusoma vitabu 500 kwenye jambo hilo. Ukisoma vitabu 100 unakuwa ndiyo umeanza kulijua jambo, ukisoma vitabu 200 utaanza kujua kama unaweza kutengeneza fedha au la, ukisoma vitabu 300, utaanza kutengeneza kipato cha kawaida. Ukisoma vitabu 400 unatengeneza kipato cha uhakika na cha juu zaidi, na ukisoma vitabu 500 unakuwa mtu uliyebobea, unakuwa ‘world class’. Sasa vitabu 500 unavimalizaje? Ushauri ukawa, unavisoma ndani ya miaka mitano, na kila mwaka unasoma vitabu 100. Kwa kuwa mwaka una wiki 52, basi kila wiki ukisoma vitabu viwili tu, kwa mwaka unamaliza vitabu 100.

Nikaona ni wazo zuri, nikawashirikisha watu wote kupitia mitandao yote niliyopo. Wengi walisema haiwezekani kabisa, na sababu nyingi. Nashukuru nilipata watu wa kuanza nao, na tangu october 2014 mpaka leo tuna kikundi cha kusoma vitabu viwili kila wiki. Siyo kila wiki unakamilisha vitabu vyote viwili, lakini una uhakika wa kumaliza kitabu kimoja kila wiki. Nimeweza kufika hatua ya kusoma kitabu kizima kwa siku moja. Mpaka sasa nimesoma vitabu zaidi ya 300, na hili litakwenda kwa maisha yangu yote.

13. Una muda wa kutosha kufanya kila unachotaka kufanya.

Tangu mwaka 2014, nimerudi kwenye masomo ya udaktari, masomo magumu na yanayohitaji muda. Nimekuwa nafanya masomo haya ya udaktari, naandika kila siku, naendesha biashara, nasimamia kazi za kampuni na nina familia, mke na watoto wawili. 

Nawezaje yote hayo, kwa sababu nimejifunza upo muda wa kutosha kufanya kila ambacho mtu anataka kufanya. Muhimu ni kuupangilia vizuri na kuweka vipaumbele, baada ya hapo unakuwa na nidhamu kwenye vipaumbele vyako.

Masaa 24 uliyonayo kwenye siku ni mengi sana, hasa ukipunguza muda wa kulala na unaopoteza kwenye mambo yasiyo ya msingi.

14. Habari ni uchafu kwenye akili ya mtu.

Katika kujifunza ili kuboresha maisha yangu, nilikuwa nakutana na ushauri wa kuachana na habari. Sikuwa nauelewa, maana nilikuwa nimekunywa sumu ya kuamini lazima ujue kila kinachoendelea bwana! Hivyo asubuhi nilikuwa naanza na uchambuzi wa magazeti, habari nyingine, jioni nahakikisha naangalia taarifa za habari zote, nijue mambo yanaendaje. Basi nikajaribu hilo la kuacha habari, kitu kinachoitwa kama NEWS FAST. Nikaenda kwa wiki moja bila ya habari yoyote. Na baada ya wiki kuisha, sikuwa nimekosa chochote cha maana, na nikawa nimeweza kusoma vitabu zaidi na kupata muda wa kufanya zaidi.

Habari ni uchafu kwenye akili, na ni upotevu mkubwa wa muda kwa mambo ambayo hayana umuhimu wowote. Ikiwepo habari muhimu kabisa, utaisikia kwa kila mtu, na siyo mpaka wewe upoteze muda kuipata.

15. Hakuna sehemu nzuri ya kujifunza kama kwenye foleni au kusubiri kitu.

Ninaishi dar es salaam, mji ambao foleni siyo kitu cha kushangaza, ni sehemu ya maisha. 

Nilijifunza kwamba foleni siyo muda wa kulalamika wala kupoteza, hivyo nikaona njia nzuri za kujifunza ukiwa kwenye foleni. Njia hizo ni kusoma vitabu au kusikiliza vitabu. Siku za nyuma nilikuwa natumia daladala, sasa daladala za dar kukaa kwenye siti ni bahati, na hivyo mara nyingi unasimama. Huwezi kusoma kitabu ukiwa umesimama na kubanwa na watu. 

Hivyo nilichofanya ni kununua simu ndogo inayoingia memory card na spika za masikioni, kisha nikawa nasikiliza vitabu muda wote niwapo kwenye foleni. Yaani naweza kuwa nimesimama kwenye gari nikasikiliza kitabu mwanzo mpaka mwisho. Baadaye nikawa natumia gari yangu binafsi, na mpaka sasa sheria yangu ni moja, nikiwasha gari, basi lazima kuwe na kitabu kinaendelea. Nina flash yenye vitabu zaidi ya 100 vilivyosomwa (AUDIO BOOKS) kila siku natumia siyo masaa mawili kwenye foleni, na hayo yote najifunza.

16. Changamoto ndiyo mafanikio yenyewe.

Kila jambo ambalo nakutana nalo kama changamoto, mara zote nimekuwa naligeuza kama fursa kwangu ya kukua zaidi. Tangu kufukuzwa chuoni, kurudi chuoni, kuanzisha blog, kujifunza kutengeneza blog na website, kote nimekuwa nasukumwa na changamoto ninazokutana nazo mimi mwenyewe.

17. Hakuna wa kukuzia kufanikiwa, wala hakuna wa kukulazimisha kufanikiwa.

Na hii ndiyo imekuwa motto yangu siku zote; MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA. Nimekuwa naona wazi, namna ambavyo nikipambana, napata chochote ninachopigania. Na naona namna watu wengine ambao wana kila kitu wanavyoshindwa kuwa na maisha wanayoyataka, kwa sababu hawapambani. Wakifikiri watapelekewa mafanikio pale walipo.

18. Madeni ni sumu.

Nimekuwa naona namna watu wanavyoteseka na madeni. Sehemu ambazo nilibahatika kufanya kazi kwa muda, nilikuwa naona namna watu wanakosa uhuru kwa kuwa na madeni. Nimekuwa naona watu wa karibu wakiteseka na madeni. Na sasa nina bahati ya kuwashauri watu na naona namna madeni yanawashikilia nyuma.

Hivyo nilijiwekea sheria, ya kwamba ni marufuku kukopa kitu ambacho hakinizalishii. Yaani kama nitakopa halafu nilipe mimi, hairuhusiwi. Labda kama nitakopa na walipe wengine, ikiwa na maana nikope kwa ajili ya kuzalisha zaidi. Lakini kukopa ili kupata fedha ya kula, nimejiwekea mwiko kwenye hilo. Na ni bora nishinde njaa au nifanye kazi usiku na mchana, na kazi ya aina yoyote ile halali, ili kupata fedha ya kuendesha maisha, na siyo kukopa. Na ninashukuru mpaka umri huu sina madeni yoyote ambayo ni mzigo kwangu, labda deni la elimu ya juu ambalo ninapanga kulilipa mara moja.

19. Ukiona kitu kinakubalika na wengi, ni vyema ukakaa nacho mbali, siyo kitu bora kwako.

Nilichojifunza ni kwamba, kitu kinachokubalika na wengi, ni kitu rahisi, kisicho na ugumu na thamani yake ni ndogo. Vitu vigumu, ambacho siyo rahisi kufanya na thamani yake ni kubwa, vimekuwa havina umaarufu kwa wengi. Na hivyo ndivyo navipenda mimi, maana ndiyo vinakutenga na wengi na kukuinua zaidi.

20. Kazi, kazi, kazi, kazi.....

Naweza kuandika hilo hata mara ishirini, na bado nitaendelea kuliamini zaidi. NI KAZI. 

Nimeshaandika pia hapo juu, lakini kazi inasimama yenyewe. Ninaamini kabisa kutoka ndani ya moyo wangu na hili halitakuja kutetereka maisha yangu yote, ya kwamba fedha na maendeleo ni zao la KAZI. Naamini hakuna kabisa njia rahisi ya kupata fedha na mafanikio bila ya kufanya kazi. Na hivyo mtu yeyote akija kwangu na kuniambia kuna njia ya kupata hela bila kufanya kazi, namwambia aishie hapo hapo, na aache ujinga. Katika kujifunza kwangu, nimeenda mbali kabisa kwenye historia, tangu utawala wa roma, kilichowainua watu na hata kuwaangusha ni kazi.

21. Usipokuwa na misingi, utaangushwa.

Mwaka 2014, ilikuja fursa moja ya kibiashara hapa Tanzania. Sasa fursa hizi zikija, watu wengi huwa wananitafuta kwa sababu wanajua nina mtandao mkubwa. Wakaniambia fursa hiyo, nikaingia kwenye misingi yangu, nikaona haiendani na misingi ile. Yaani ilikuwa unaweza kupata fedha, bila ya kazi yoyote, wewe ni kuwaunganisha watu wengi tu. 

Nikaikataa. Mtu mmoja tuliyeheshimiana sana aliniambia Amani unaikosa hii fursa, utakuja kujuta, wewe ulivyo na mtandao mkubwa utanufaika zaidi. Nikamwambia ni bora niikose lakini siyo kuharibu kile ninachojenga. Haikuchukua muda biashara ile ilifungwa na wale waliojihusisha nayo kupoteza fedha, muda na heshima zao.

Nisingekuwa na misingi niliyojijengea, ningeingia haraka kwa tamaa ya fedha za haraka, na leo nisingekuwa nakuandikia haya hapa.

22. Dunia itakupa unachopigania.

Hili nimekuwa naliona kila mahali. Yaani dunia inampimia kila mtu kadiri ya anavyopigana na kupambana. Wanaoweka juhudi kidogo wanapata kidogo, wanaoweka juhudi kubwa wanapata zaidi. Na hii haijalishi unaanzia wapi, kinachopimwa ni juhudi za kazi unayofanya, inayoongeza thamani kwa wengine.

23. Umasikini ni mbaya, umasikini ni sumu.

Kumekuwa na dhana fulani kwenye jamii zetu kwamba kuongelea utajiri ni kitu kibaya. Siku za mwanzo nilikuwa nikiandika makala yoyote kuhusu utajiri watu wananiandikia maisha siyo utajiri tu, au fedha siyo kila kitu, au fedha haileti furaha. Kuna wakati, wakati bado naanza kuandika, mpaka nikawa naogopa kuandika chochote kuhusu utajiri, mpaka nilipojiuliza mimi nataka utajiri au umasikini. Na nikaandika kitabu KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, nikieleza sababu zote zinazowafanya watu wanase kwenye umasikini. Na sasa nasema kila mtu anapaswa kuwa tajiri, utajiri siyo kitu kibaya, na umasikini siyo kitu kizuri, na tukiacha kupunguza ukali wa maneno, umasikini ni mbaya, umasikini ni sumu. Nimekuwa hospitali kwa muda mrefu wa masomo yangu ya udaktari, na nikuambie tu, watu masikini wanakufa kwa sababu za umasikini zaidi ya kitu kingine chochote. Kila siku nasema umasikini ni mbaya.

24. Tafuta kitu ambacho unaweza kufanya kila siku.

Kila siku, ninapoamka asubuhi, kitu cha kwanza ni kuandika. Nimekuwa naandika kila siku, bila kuruka hata siku moja tangu mwaka 2014. Kwa tabia hii ya kuandika kila siku, naianza siku yangu kwa ushindi. Hata kama kila nilichopanga siku hiyo hakitaenda sawa, mwisho wa siku najua leo niliandika, na unakuwa ushindi mkubwa zaidi.

Pata kitu cha aina hii kwako, inaweza kuwa ni kutandika kitanda chako kila siku, au kusoma kitu asubuhi, au kuandika, au kufanya mazoezi, chochote kitakachoianzisha siku yako vizuri.

25. Amka asubuhi na mapema, ushindi upo asubuhi.

Katika maisha yangu ya elimu, sijawahi kuwa mtu w akukesha kusoma. Sasa nilipochaguliwa kujiunga na sekondari ya kibaha, ile ni shule ya wanafunzi wenye vipaji maalumu kiakili, nilipofika nilikuta watu wanaweza kusoma mpaka asubuhi, wanakesha usiku kucha. Na mimi nikajaribu siku moja kukesha, nikasoma kuanzia saa tatu usiku mpaka saa moja asubuhi, nililala siku tatu mfululizo, na siku weza kusoma chochote kwa siku hizo tatu. Basi nikaona hii hainifai, nikaanza kujaribu njia nyingine, nikawa naamka asubuhi na mapema, nikaona muda huu ni mzuri zaidi. Basi tangu kipindi hicho, mwaka 2007 mpaka leo, huwa naamka asubuhi sana na mapema, kati ya saa kumi mpaka saa kumi na moja asubuhi. Na nimekuwa napata masaa mawili ya kufanya mambo makubwa kila siku.

Ushindi upo asubuhi, ukiweza kuitengeneza vizuri asubuhi yako, utaweza kuimiliki siku yako.

26. Chagua sana marafiki zako.

Baada ya kuanza kuyaboresha maisha yangu, niligundua sehemu kubwa ya marafiki niliokuwa nao nisingeweza kwenda nao tena. Kwa sababu unagundua maono yenu yanatofautiana. Wakati wewe unapanga kuweka akiba uwekeze, wao wanawaza ‘bata’ nzuri zinaliwa wapi. Ili kuondoa mzozano, nilipunguza sana marafiki, na cha kushangaza nimepata marafiki wengi zaidi wenye mtizamo wa kule ninakokwenda.

Kama watu wanaokuzunguka unaona hawaendani na ndoto zako, usiwalee wala kuwaonea haya, kaa nao mbali, maisha ni yako, unastahili kilicho bora.

27. Uwekezaji ndiyo msingi wa utajiri.

Kama nilivyosema, utajiri ni muhimu kwenye maisha ya kila mtu, kama bado huna sumu ya jamii kwamba matajiri ni watu wabaya. Sasa watu wengi wamekuwa wanafikiria utajiri unaweza kuja mara moja, labda kushinda bahati nasibu au kurithi mali. Lakini njia ambayo mimi naifanyia kazi kila siku ni uwekezaji. Na upo uwekezaji wa kila aina, ambao unaweza kuanza kidogo kabisa na kujenga utajiri wako.

Kama huwekezi, sijui unafanya nini, kwa sababu kipato chochote ulichonacho sasa, iwe ni ajira au biashara, huna uhakika wa kuendelea kuwa nacho milele. Mambo yanabadilika, na nguvu zako zinapungua, unahitaji kufika wakati ambapo uwekezaji wako unakuzalishia hata kama hufanyi kazi.

28. Usisubiri uwe tayari, unapopata wazo zuri, au unapoona fursa inayokufaa, iendee.

Mambo yote ninayofanya kwenye maisha yangu, sijawahi kusubiri mpaka nikawa tayari. Nimekuwa napata wazo na kuanza, naona fursa na kuichukua. Ninapoanza kufanya ndiyo nakutana na changamoto zaidi ambazo zinanifanya nijifunze zaidi. Ninachojifunza kinakukwa kikubwa kuliko kama ningesubiri mpaka niwe tayari.

Nimekuwa najaribu vitu vingi mno, vingine vinakubali na nakwenda navyo, vingine vinakataa na ninaachana navyo.

29. Wewe pekee ndiye unayeweza kujielewa. Wengine watakuelewa nusu nusu tu.

Hili nimekuwa naliona kila wakati, nawaambia watu kitu ambacho labda napanga kufanya, au nafanya, na watakataa kwamba haiwezekani. Huenda hata wewe kwenye orodha hii ya vitu 29, kuna baadhi ya vitu utakuwa na wasiwasi navyo, na kusema haiwezekani akawa ameweza kufanya hivyo. Sikushangai, kwa sababu ni vigumu sana mtu kumwelewa mtu mwingine kwa uhakika. Kile mtu anajielewa yeye mwenyewe zaidi.

Kwa mfano sasa hivi kuna tatizo la ukosefu wa ajira kila kwa kila sekta, hata kwa fani kama za udaktari, tunaona wahitimu ni wengi na ajira hakuna. Sasa watu wananiuliza wewe umesomea udaktari, unafikiriaje swala la ajira? Nawajibu sina mpango wa kuajiriwa, wanashangaa, sasa umesomea udaktari ili nini? Hapo na mimi inabidi niwashangae, kwa sababu dhana kwamba unasoma ili uajiriwe, ni uongo ambao umepoteza wengi. Ndiyo nimeweka juhudi kubwa kusomea udaktari, lakini sitaajiriwa, na zipo njia nyingi ninaziona za kutumia udaktari wangu kuwasaidia wengi zaidi.

Hayo ndiyo mambo 29 muhimu niliyoweza kukushirikisha rafiki yangu, leo hii nikiwa na miaka 29. Yote hapo ni kutokana na uzoefu wangu mdogo nilionao mpaka sasa. Najua bado nina miaka mingi, na yote nitaiendea na msingi imara ninayoendelea kujijengea.

Wapo wengi wamekuwa wananiandikia kila siku, nataka kuwa kama wewe nifanyeje? Na sehemu ya kwanza ninayowaambia wawe ni kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambapo tunakuwa karibu kupitia kundi la wasap. Kujiunga unalipa ada ya shilingi elfu 50 ambayo ni ada ya mwaka kupitia namba 0755953887 au 0717396253 kisha unatuma ujumbe kwenye wasap namba 0717396253 na ninakuweka kwenye kundi.

Pia nimekuwa naandika vitabu, na vyote nimekuwa nashirikisha uzoefu wangu binafsi kwenye mambo mbalimbali. Yaani kwenye vitabu hivi nakupa maarifa ambayo mimi mwenyewe nayatumia kwenye maisha yangu. Vitabu kaka; KWA NINI MPAKA SASA WEWE SIYO TAJIRI, JINSI YA KUTENGENEZA KIPATO KWA KUTUMIA BLOG, BIASHARA NDANI YA AJIRA na PATA MASAA MAWILI YA ZIADA, kote nimeshirikisha yale ninayofanya mimi mwenyewe. Hivyo unaweza kusoma vitabu hivi na kuweza kuchukua hatua zaidi. Kupata vitabu tuma ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717396253 na nitakupa utaratibu wa kupata vitabu hivyo.

Nina mengi ya kukushirikisha rafiki, haya hapa ni chembe tu. Nimekuwa najifunza kila siku na nitaendelea kujifunza maisha yangu yote. Kuandika ni kitu ambacho nitakifanya kila siku ya maisha yangu, hivyo kuwa karibu na AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu, unayoweza kuitumia kutengeneza kipato, BONYEZA maandishi haya.

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>