Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

ONGEA NA KOCHA; Waepuke Watu Hawa Kwa Nguvu Zako Zote, Wanakurudisha Nyuma.

$
0
0
Habari za leo rafiki yangu?

Karibu kwenye mazungumzo yetu ya leo ambapo wewe na mimi kocha wako tunapata nafasi ya kushirikishana mambo muhimu kuhusu maisha na mafanikio. Ni muhimu tukumbushane mambo haya mara kwa mara kwa sababu tukikaa muda mrefu bila ya kukumbushana tunasahau na kurudi kule kule.
 

Watu wengi wamekuwa wanafikiri maarifa ni kitu unachopata mara moja na kisha ukawa vizuri. 

Kama ambavyo wengi wakishahitimu masomo yao basi wanatupa kabisa vitabu na kuona wapo huru na wameondoka kwenye kifungo cha kusoma.

Kama una mawazo ya aina hiyo kwanza nikupe pole, halafu nikuambie AMKA kutoka kwenye huo usingizi. Kama umechagua maisha ya mafanikio, kama umechagua kuingia kwenye biashara na kufanikiwa, kama unataka kufanya kazi yako kwa ubora wa hali ya juu na kuweza kugusa maisha ya wengi, basi kuna kitu kimoja ambacho LAZIMA ukifanye mpaka siku utakapoingia kaburini, kitu hicho ni KUJIFUNZA KILA SIKU.

SOMA; Wajue Watu Hawa na Waepuke Kwenye Maisha Yako.
Nimeanza na hili la kujifunza kwa sababu kuna watu wanajidanganya kwamba wanajua kila kitu. 

Kuna watu hawanunui vitabu kwa kuona wanajua zaidi, kuna watu hawahudhurii mafunzo hata yanayotolewa bure kwa kuamini wanajua kila kitu. Hawa ni watu ambao wamechagua kufa kabla ya wakati wao, hawa ni watu ambao hawana tena wanakotaka kwenda.

Nakusihi sana wewe rafiki yangu, usiwe mmoja wa watu hawa, maana unakuwa umechagua maisha magumu wewe mwenyewe kwa hiari yako.

Baada ya hayo machache kuhusu kujifunza kila siku, leo nataka nikushirikishe kuhusu watu hatari sana unaopaswa kuwaepuka kwenye maisha yako.

Unakumbuka wakati ukiwa mdogo wazazi wako walikuambia usicheze na watoto fulani? Kwa sababu watoto hao walikuwa na tabia mbaya na ukaambiwa ukicheza nao na wewe utakuwa na tabia mbaya? Huenda uliona wazazi kama wanakuonea, hasa kama watoto wale ni marafiki zako au mlisoma pamoja. Huenda pia hili unalifanya kwa watoto wako, kuwatahadharisha wasicheze na watoto fulani ambao tabia zao siyo nzuri.

Sasa leo na mimi nachukua jukumu hilo la kukutahadharisha watu wa kuepuka kuwa nao kwenye maisha. Watu ambao ni sumu na ukiwachekea wanakumaliza kabisa.

Je kuna mtu yeyote amewahi kukuambia ndoto zako ni kubwa mno, mipango unayoweka unajidanganya, huwezi kuifikia? Je kuna mtu amewahi kukuambia unapenda pesa sana, kwamba siyo vizuri kupenda sana pesa? Kuna mtu amewahi kukuambia kwamba unapenda sana kufanya kazi, kwamba upunguze kidogo? Sasa leo nataka kukuambia, watu wa aina hiyo ni hatari mno.

SOMA; Mambo Muhimu Ya Kujifunza Kutoka Kwa Watu Wenye Mafanikio.

Watu hawa ni hatari kwa sababu wanachofanya ni kutafuta watu ambao watawadhibitishia kwamba wapo sahihi.

Si umewahi kusikia usemi kwamba kifo cha wengi ni harusi? Sasa hivyo ndivyo tabia na saikolojia ya binadamu ilivyo. Kwamba mtu akiwa peke yake anajiona kama hayupo sahihi au anakosea, na akiwa katikati ya wengi anaona yupo sahihi kwa sababu siyo yeye mwenyewe ambaye yupo vile alivyo.

Sasa kwenye jamii zetu, wapo watu ambao wamekata tamaa na maisha yao, wapo watu ambao ni wavivu na wazembe ambao hawawezi kufanya kazi zao kwa juhudi. Wapo watu ambao hawajiamini, na hivyo hawaamini kwenye ndoto zao. Na wapo watu ambao umasikini umewaburuza vya kutosha.

Watu hawa hawapendi kuwa peke yao, hivyo wanahakikisha wanapata wafuasi wa kutosha, ili wasionekane wao ndiyo wazembe peke yao. Hivyo wanachokifanya ni kuhakikisha kila mtu anayewazunguka naye anakuwa kama wao. Hivyo wakikuona wewe una ndoto kubwa, kwa sababu hawaamini kwenye ndoto zao, basi wanakukatisha na wewe tamaa, wanakuambia uachane na ndoto hizo, unajidanganya. Kwa sababu wao hawawezi kufanya kazi kwa kujituma, wakikuona wewe unajituma wanaanza kukuambia unapenda kazi sana, punguza kidogo, au unajipendekeza na maneno mengine ya hovyo kama hayo. Kwa sababu wao umasikini umeshawamaliza, wakikuona wewe una mipango mikubwa ya fedha wanaanza kukusema unapenda sana fedha, una tamaa ya fedha na mengine kama hayo.

SOMA; Hawa Ndiyo Watu Muhimu Sana Wanaoleta Mabadiliko Katika Jamii Yetu.

Wanafanya hivyo kwa sababu wanataka wapate wafuasi kwenye kundi lao la watu wazembe na waliokata tamaa. Sasa kama wewe utakubaliana nao, utakuwa umechagua kuingia kwenye kundi la wazembe na kuzika kabisa ndoto zako.

Ndiyo maana leo nimeona nikukumbushe hili rafiki yangu. Kaa mbali kabisa na mtu yeyote yule, ambaye anatoa kauli yoyote ya kukukatisha tamaa na kuzima ndoto zako. Yaani mtu anapoanza tu maneno hayo ya kukatisha tamaa, usiendelee kumsikiliza, achana naye mara moja.

Hatusemi kwamba mafanikio ni rahisi,

Wala hatusemi kwamba utajiri ni rahisi,

Hatujidanganyi kwamba ipo njia ya mkato ya kufanikiwa.

Tunaujua ukweli kwamba ili kufanikiwa tunahitaji kuweka juhudi kubwa, tunahitaji kujitoa na pia tutakutana na changamoto nyingi kadiri tunavyokwenda. Ambacho hatutaki ni mtu kutupigia kelele hizi kila siku, mtu kutukatisha tamaa hata kabla hatujaanza. Usiruhusu hilo rafiki yangu. 

Kaa mbali kabisa na watu wenye dalili na tabia za aina hiyo.

Muhimu; karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambapo utakutana na watu wenye sifa za tofauti na jamii inayokuzunguka. Ndani ya kisima unakutana na watu wanaopambana kufanikiwa, wanaojua wapi wanakwenda na wanaojua hakuna wa kuweza kuwazuia. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma ujumbe wenye neno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap kwenda namba 0755 953 887 (tumia wasap pekee)

Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,

Kama umejifunza kupitia makala hii karibu tujifunze zaidi kupitia KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utaingia kwenye kundi la wasap na kupata mafunzo kila siku. Bonyeza maandishi haya kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea MOBILE UNIVERSITY (bonyeza hayo maandishi.)

Pata kitabu BIASHARA NDANI YA AJIRA ujifunze jinsi unavyoweza kuanzisha na kukuza biashara yako, pia utajifunza mifereji nane(08) ya kipato unayopaswa kuwa nayo ili kufikia uhuru wa kifedha. Bonyeza maandishi haya kupata kitabu.

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>