Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; WHY WE WORK (Nadharia Ya Nini Kinawasukuma Watu Kufanya Kazi).

$
0
0


Nadharia ambayo imekuwa inatawala ulimwengu wa kazi na biashara ni kwamba watu wanafanya kazi ili walipwe. Kwamba kitu pekee kinachowasukuma watu kufanya kazi ni fedha. 


Nadharia hii imekuwa inatumika kuwalaghai watu wafanye kazi zaidi kwa kuwaongezea fedha, au kuwaadhibu wape wanaposhindwa kufanya kazi kwa kuwakata fedha.

Lakini tafiti nyingi zinaonesha kwamba kinachowasukuma watu kufanya kazi siyo fedha pekee. Japo fedha ni muhimu, lakini siyo kitu pekee kinachowasukuma watu kufanya kazi. Bali watu wanasukumwa zaidi na maana ambayo kazi wanayoifanya inawapa. Kwamba ni mchango gani wanatoa kupitia kazi hizo wanazofanya.

Mwanzilishi mkubwa wa nadharia kwamba watu wanafanya kazi kwa ajili ya fedha pekee ni mwandishi Adam Smith aliyeandika moja ya vitabu vilivyojenga misingi ya ubepari. Katika kitabu chake cha THE WEALTH OF NATIONS, Adam aliandika kwamba kwa asili watu ni wavivu na hawapendi kufanya kazi, hivyo ili kiwanda kiweze kuzalisha kwa wingi na kupata faida, lazima kigawe majukumu yake katika vipande vidogo vidogo sana ambavyo vinaweza kufanywa na yeyote bila hata ya ujuzi mkubwa, kisha kutafuta watu unaoweza kuwalipa kiasi kidogo na wakafanya kazi hiyo. Wakikataa tafuta wengine, maana huhitaji utaalamu mkubwa. Na alitumia mfano wa kiwanda cha kutengeneza pini, ambapo aligawa jukumu la kutengeneza pini katika hatua tano, ambapo kila hatua inahitaji mtu mmoja, hatua ya kwanza ni kukata waya, hatua ya pili kuunyoosha, hatua ya tatu kuweka ncha mbele, hatua ya nne kuweka kichwa cha pini na hatua ya tano kutoa pini iliyokamilika. Hapo unaweza kumwajiri mtu yeyote na akafanya kazi.

SOMA; Sababu Tatu(3) Zinazokuzui Kufanikiwa Kwenye Kazi Unayofanya.

Tatizo la nadharia ya Smith ni kuwachukulia watu kama mashine ambazo zinaweza kufanyishwa kazi muda wowote na kupata kile mtu anachotaka. Na hii imeondoa kabisa maana ya kazi kwa watu, kuwafanya watu kupata msongo wa mawazo kwa kufanya kazi ambazo hazina maana kwao.

Mwanasaikolojia na mwandishi Barry Schwartz kupitia kitabu chake hichi cha WHY WE WORK anatukumbusha msingi mkuu wa kazi kwetu, ambao ni kutengeneza maana kwetu sisi. Anatuonesha kupitia tafiti jinsi ambavyo kazi yenye maana kwa mtu ina faida kwake na kwa jamii kwa ujumla. Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi wa kitabu hiki.

1. Watu wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kinachowasukuma kufanya kazi ni kupata fedha. Unaweza kufikiri hivi wakati una shida sana ya fedha, lakini unapozipata fedha ndipo unapoona bado kuna ombwe ndani yako. Kazi inahitaji kuwa na maana kwako zaidi ya fedha unazozipata. 

Kazi inahitaji kukuridhisha wewe kwanza, kuliko hata inavyokuingizia fedha.

2. Watu ambao wanaridhishwa na kazi zao, wanapoulizwa nini kinawaridhisha kwenye kazi zao, hawataji fedha. Kitu cha kwanza kwao ni ile maana ambayo kazi wanayofanya inaleta kwenye maisha yao, ule mchango ambao wanautoa kwa wengine.

SOMA; Mambo Saba(7) Yanayowafanya Wafanyakazi Wengi Kuwa Na Ufanisi Mdogo Kwenye Kazi Zao.

3. Watu ambao wanaridhishwa na kazi zao, wanajihusisha sana na kazi zao. Wanapokuwa wanafanya kazi zao, akili yao yote na moyo wao wote unakuwa kwenye kazi hiyo. Hakuna kingine kinakuwa muhimu kwao kama kazi yao wakati wanaifanya.

4. Kitu kingine kinachowasukuma watu kufanya kazi zao, na kuwafanya wazipende ni ile hali ya kuwa na maamuzi kwenye kazi zao. Pale wanapojua kwamba wao ndiyo wenye maamuzi kwenye kazi hizo, wanapojua wao ndiyo wanajisimamia wenyewe na wanaweza kufanya kile ambacho ni sahihi kwa namna wanavyotaka wao, wanavutiwa na kazi hizo.

5. Watu hawapendi kazi kwa sababu tu ni rahisi, tafiti zinaonesha wengi wanapenda kazi ambazo zinawapa changamoto, kazi ambazo zinawasukuma zaidi kila siku, kazi ambazo zinawafanya wajifunze zaidi na kazi ambazo zinawafanya kuwafikia watu wengi zaidi kila siku.

6. Pamoja na kwamba kinachowasukuma watu kufanya kazi siyo fedha, bado sehemu kubwa ya watu kwenye jamii wanafanya kazi ili walipwe. Watu wengi wanakwenda kazini kwa sababu wasipoenda watakosa fedha ya kuendesha maisha yao. Na hii inatokana na kufanikiwa kwa jamii kutuuzia nadharia ya uongo kwamba lengo kuu la kazi ni kupata fedha, hakuna zaidi ya hapo.

7. Utafiti uliofanya na shirika la Gallup unaonesha kwamba asilimia 63 ya watu hawaridhishwi na kazi zao, na ni asilimia 13 pekee ambao wanakiri kuridhishwa na kazi wanazozifanya. Hii inaonesha kwamba sehemu kubwa ya watu wanafanya kazi ambazo hawazipendi na haziwaridhishi. Lakini wanaendelea kuzifanya kwa sababu jamii imewauzia nadharia ya uongo kwamba unafanya kazi ili ulipwe. Wanafanya na kulipwa kweli, lakini hawaridhiki na kazi zao.

SOMA; Kitu Kimoja Kinachowatofautisha Waliofanikiwa Na Walioshindwa, Na Jinsi Unavyoweza Kukitumia Kufikia Mafanikio Makubwa.

8. Watu wengi wamekuwa wanafikiri ya kwamba kuna baadhi ya kazi zinakuwa na maana na kuwaridhisha watu na nyingine haziwezi kuwa na maana. Na hapa kazi kama udaktari, uanasheria, ualimu na nyingine kama hizo zinaonekana kuwa na maana kwa wale wanaozifanya. Kazi nyingine kama za kufanya usafi au usaidizi mwingine zinaonekana ni sehemu tu ya kujipatia fedha, au ya kupita ili kupata kazi nzuri. Ukweli ni kwamba kila kazi inaweza kuwa na maana kwa mtu anayeifanya, maana haianzi na kazi yenyewe, badala yake maana inaanza na mtu mwenyewe.

9. Unaweza kutengeneza maana kwenye kazi unayofanya kwa kuangalia namna ambavyo watu wengine wananufaika na kazi unayoifanya. Kwa mfano kama kazi yako ni kufanya usafi ofisini, angalia namna ambavyo huduma yako ya usafi inaiwezesha ofisi kutoa huduma kwa watu wengine. Hebu fikiria kama ofisi ingekuwa chafu, watu wangekuja kupata huduma ambazo wanazipata pale? Kwa kuangalia eneo hili la kazi yako, utaona maana kubwa ya kazi hiyo kwako.

10. Kitu kingine kinachowatofautisha wanaoridhishwa na kazi zao na wale wasioridhishwa ni namna watu wanavyochukulia kazi hizo. Wale wasioridhishwa na kazi zao wanazichukulia kazi kama kazi tu, kitu ambacho wanafanya ili walipwe. Hakuna kingine wanachoona kwenye kazi hizo. Ila wale wanaoridhishwa na kazi zao wanazichukulia kazi zao kama WITO. Wanachokulia kama deni ambalo wanapaswa kulilipa hapa duniani, kwa njia hii wanatoa huduma bora na kupata matokeo bora pia.

11. Kuna faida nyingi pale mtu anapofanya kazi ambayo inamridhisha. Kwanza kabisa anaifanya kwa moyo mmoja na hivyo kutoa mchango mkubwa kwa wengine. Pili inamridhisha yeye mwenyewe na hivyo kutokuwa na msongo wa mawazo unaosababishwa na changamoto za kazi. Tatu inamfanya mtu kupata kipato kikubwa zaidi. Yaani hapa ni kama kinyume, kinachomsukuma mtu kufanya kazi siyo fedha, lakini anajikuta anapata fedha zaidi kwa sababu anatoa huduma zaidi.

12. Wale wanaochukulia fedha kama sababu pekee ya watu kufanya kazi, pia wamekuwa wanatumia fedha kama zawadi au adhabu kwenye kazi. Pale mtu anapofanya vizuri anaongezewa fedha na akifanya vibaya anapunguziwa fedha. Kwa mawazo ya haraka haraka unaweza kuona zawadi ya fedha inawasukuma watu kufanya kazi zaidi, lakini tafiti zinaonesha zawadi ya fedha inapunguza morali ya watu kufanya kazi. Kama watu walifanya vizuri kwa sababu kazi inawaridhisha na wewe ukawapa fedha, wanaanza kuangalia kile walichofanya kama kitu cha kununuliwa na kusahau msukumo wao wa awali. Kidogo kidogo watu wanasahau msukumo halisi na kuangalia fedha pekee.

13. Hasara nyingine ya kutumia ongezeko la fedha kama zawadi kwa wale wanaofanya kazi vizuri, kunawafanya watu kutafuta njia zisizo sahihi za kuonekana wamefanya kazi ili walipwe zaidi. Inaacha kuwa kufanya kazi halisi na inakuwa kutafuta njia itakayoonesha kwamba mtu amefanya kazi. Na hapa ndipo uongo unapotawala sehemu za kazi.

14. Kuwepo kwa miongozo mingi ya namna mtu anavyopaswa kufanya kazi yake imekuwa chanzo cha wengi pia kutokuridhishwa na kazi zao. Pale ambapo mtu anasimamiwa sana, anakosa uhuru wa kufanya kazi yake kwa uwezo wake na anaishia kufanya kwa hofu.

15. Mawazo na mifumo ya kijamii ina nguvu kubwa ya kuwabadili watu. Hata kitu cha uongo, kinapokelewa kama ukweli pale ambapo watu wengi wanakikubali katika jamii. Na hivi ndivyo maeneo ya kazi yamekuwa yanawabadili wafanyakazi. Pale ambapo utamaduni wa kazi ni kuwaangalia wafanyakazi kama watu wako pale kwa ajili ya kupata fedha, na watu wanafanya kwa ajili ya kupata fedha pekee.

16. Mara nyingi watu wanatoa kile ambacho wanategemewa kutoa, wanafanya kile ambacho wanategemewa kufanywa. Na ndiyo maana watu wakitegemewa kufanya kazi zao kwa kujituma wanafanya hivyo, wakitegemewa kufanya ili wapate fedha, wanafanya hivyo pia.

17. Kile ambacho watu wanafanya kwenye kazi zao za kila siku, kinatokana na namna watu wengine wanavyofanya kwenye kazi zao hizo pia. Hii ndiyo maana wazo lolote ambalo linachukuliwa na wengi, linaonekana kama wazo zuri hata kama siyo wazo sahihi.

18. Wachumi wanafikiria ufanisi kwa kipimo cha fedha, kwamba kiasi kilichowekezwa kimezalisha kiasi gani. Na katika hesabu hizi, mfanyakazi anaonekana kama uwekezaji na siyo mchango muhimu kwenye uzalishaji. Kipimo sahihi ambacho kinaweza kuwajumuisha wafanyakazi pia ni kuangalia mtu amepata ubora kiasi gani, kwa kuangalia pia mchango wa wafanyakazi kwenye kile kilichofanyika.

19. Watu wengi ambao wanafanya kazi zao kwa sababu tu ya fedha, wanaweka juhudi sana mwanzoni na huenda wakafanikiwa kuzipata hizo fedha. Lakini baada ya kupata fedha, ndipo wanapoona kazi zao kama mzigo kwao, wanaanza kufanya mambo ambayo wengine wanashindwa kuwaelewa. Ni vyema kutengeneza maana ya kazi yako kwako kabla hujafika hatua ya kuichoka na kujikuta unaharibu kila ambacho ulishatengeneza.

20. Mengi ambayo umejifunza hapa yanaweza kuwa yanakushangaza, kwa sababu tangu unakua mpaka sasa, tangu unasoma mpaka unatafuta kazi au biashara ya kufanya, mawazo yako yote yalikuwa ni kuhusu kupata fedha. Lakini sasa unajifunza kitu cha tofauti, ambacho unaweza usijue ni namna gani ya kukitumia, sasa naomba nimalize kwa kukupa hatua muhimu za kuchukua;

1. Kwa kazi au biashara ambayo unafanya sasa, anza kutafuta maana yake kwako licha tu ya kupata fedha. Angalia ni watu gani wananufaika na kile unachofanya, angalia ni mchango gani unaotoa kwa wengine, utaanza kuona umuhimu wako kwa wengine.

2. Kazi au biashara yoyote unayoifanya, imiliki kama yako, hata kama umeajiriwa. Ona kila unachofanya kama kina nembo yako, hivyo kifanye kwa ubora wa hali ya juu sana.

3. Acha kuangalia fedha pekee kwenye kila unachofanya, acha kuhesabu fedha pekee kwenye kila unachogusa, angalia pia namna unavyogusa maisha ya wengine.

4. Unapoajiri watu, ajiri kwa uwezo wao na hamasa yao ya kufanya kazi. Na usiajiri tu kwa sababu wanataka fedha. Ajiri watu ambao wana mchango kwenye kile unachotaka wafanye.

5. Unapoajiri watu ambao wana uwezo na hamasa ya kufanya kazi, wape uhuru wa kufanya kazi zao kwa ubora wa hali ya juu. Pia usiwajengee utaratibu wa kupongezwa kwa fedha pale wanapofanya kazi nzuri. Angalia njia nyingine za kuwaonesha wana mchango na wanajaliwa kuliko tu fedha.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>