Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; Sometimes You Win, Sometimes You Learn. (Somo Kubwa Unaloweza Kujifunza UCHAMBUZI Kupitia Makosa Yako).

$
0
0
Tunaishi kwenye dunia ambayo ni ya kushinda au kushindwa, kupata au kukosa, hali ambayo inayafanya maisha yetu labda yawe ya furaha sana kama tunashinda, au ya huzuni sana kama tunashindwa. Hivi sivyo maisha yanapaswa kwenda, kwa sababu jambo moja la uhakika ni kwamba, kila binadamu aliye hai, kuna namna atashindwa kwenye maisha. Yapo makosa ambayo atafanya na yatamkosesha kile ambacho anakitaka.
 

Hii ndiyo iliyopelekea mwandishi John Maxwell kuandika kitabu Sometimes You Win, Sometimes You Learn. Kauli ya kawaida iliyozoeleka na wengi ni kwamba sometimes you win, sometimes you lose, yaani mara nyingine unashinda, mara nyingine unashindwa. Lakini Maxwell anatuambia tuondoe neno kushindwa na tuweke neno KUJIFUNZA. Kwa sababu kama tunataka kunufaika na makosa tunayofanya, basi lazima tujifunze kupitia makosa hayo.

Karibu tujifunze kwa pamoja namna tunavyoweza kunufaika na makosa tunayofanya kwenye maisha yetu ya kila siku.

1. Mwisho wa kusoma siyo cheti au shahada (degree).

Umekuwa ni utamaduni wa wengi kufikiria kwamba kujifunza kunaisha pale wanapohitimu masomo yao ya shuleni. Ukweli ni kwamba unapohitimu ndiyo kujifunza kuhusu maisha kunaanza. Masomo ya shuleni yanakupa tu mwanga, lakini kujifunza halisi kupo kwenye maisha yako ya kila siku.

2. Kila mtu anashindwa, lazima na wewe utashindwa.

Ni kawaida yetu binadamu kufikiria kwamba maisha yanapaswa kuwa rahisi, sijui hata ni nani alitudanganya, kwa sababu ukiangalia mtiririko wa maisha yetu, kila kitu tumekuwa tunaanza kwa kushindwa. Angalia mtoto mdogo anapojifunza kutembea, anaanza kwa kuanguka. Lakini habaki pale alipoanguka, anaamka na kuendelea mbele.

Katika maisha yako ya kila siku, utashindwa na utafanya makosa. Hivyo usijisahaulishe wala usikubali kudanganywa kwamba maisha yako yatanyooka pekee, hata kama ungekuwa mtu gani.

3. Kushindwa ni darasa zuri mno kwako.

Unaweza kutumia kushindwa kama mwisho na kukata tamaa, au unaweza kutumia kushindwa kama hamasa ya wewe kusonga mbele zaidi. Kama unataka kufanikiwa kwenye maisha, basi unachopaswa kufanya ni kujifunza kupitia kushindwa kwako, jifunze kupitia makosa yako. Kipi ulichofanya kimepelekea matokeo uliyopata.

Kushindwa halafu usijifunze chochote kutokana na kushindwa huko hapo ni kushindwa mara mbili. Usikubali kushindwa mara mbili, jifunze kwa kila kosa na kila unaposhindwa.

4. Tofauti ya wanaofanikiwa na wanaoshindwa.

Inaanzia na namna wanavyoyachukulia makosa yao.
Mtu aliyefanikiwa anapokosea au anaposhindwa, anakubali mchango wake kwenye kushindwa kwake, anajifunza na kuchukua hatua. Wakati mwingine hawezi kurudia kosa kama lile au kushindwa kwa namna ile.

Ila sasa kwa wasiofanikiwa, hata mara moja hawezi kukubali amefanya makosa au ana mchango kwenye kushindwa kwake. Atakuja na kila sababu kwa nini ameshindwa, ila sababu hata moja haitamhusu yeye. Atakuambia kuhusu uchumi mbaya, kuhusu serikali mbovu, kuhusu wazazi waliomlea, kuhusu ndugu waliomtenga na hata kuhusu mke au mume ambaye amesababisha.

Usiwe mtu wa kutafuta sababu za kufunika kushindwa kwako, kubali mchango wako kwenye kushindwa, jifunze na songa mbele.

5. Kwa nini kushinda na kushindwa tunapokea tofauti?

Tunaposhinda tunachukulia kawaida, tunaona ni haki yetu kushinda, kwa sababu ndiyo tulichotegemea. Lakini tunaposhindwa tunaumia sana, hii ni kwa sababu tunakuwa na mategemeo makubwa ya kushinda. Tunakuwa tumewekeza hisia nyingi kwenye ushindi na tunapoukosa, tunaona kama hatustahili.

Anza kuchukulia ushindi kama ushindi, kama nafasi nzuri ambayo umeipata kwa kufanya mambo mazuri. Na pia chukulia kushindwa kama darasa la kujifunza namna bora kabisa ya kufanya mambo. Ukifanya hivi utanufaika kila mara, iwe umeshinda au umeshindwa.

6. Tengeneza mzunguko chanya kwenye maisha yako.

Tunaposhinda tunatengeneza mzunguko chanya, yaani unaposhinda kitu kimoja, unakuwa na hamasa ya kufanya kitu kingine na kingine na kingine tena. Yaani kama utaendelea kushinda basi unajikuta unafanya mengi.

Tatizo lipo kwenye kushindwa, maana hapa unatengeneza mzunguko hasi kwenye maisha yako. Unaposhindwa jambo moja, unaanza kujiona kama huwezi au hufai, hivyo unaogopa kuchukua hatua kwenye jambo jingine na hivyo kurudi nyuma zaidi.
Usikubali kushindwa kwenye jambo moja kulete mzunguko hasi kwenye maisha yako, jifunze kwa kila jambo na endelea kujaribu mengine zaidi.

7. Kujifunza kwenye kushindwa siyo kitu rahisi.

Ni kweli kujifunza kupitia kushindwa ni kitu chenye manufaa sana, lakini kwa nini wengi hawafanyi hivyo? Kwa sababu siyo rahisi. Siyo rahisi kujifunza wakati umeshindwa, kwa sababu kushindwa kunaumiza na kwa asili tunapoumizwa tunapenda kukaa na kupunguza yale machungu.
Kujifunza wakati wa kushindwa kunatutaka tuende tofauti na asili yetu. Kunatutaka tutabasamu wakati hatuna furaha, inahitaji nidhamu kuweza kufanya hivi. Jijengee nidhamu hii kwa kuanza na hatua ndogo ndogo na hatimaye utaweza kujifunza kwenye kila kushindwa unakopitia.
Mambo kumi na moja unayoweza kujifunza kupitia kushindwa;

8. UNYENYEKEVU; Hamasa ya kujifunza.

Huwezi kujifunza kupitia kushindwa kama huna unyenyekevu. Unyenyekevu ni hamasa kubwa ya kujifunza pale unaposhindwa. Kama unajiona wewe ni wa pekee sana, hustahili kushindwa, basi huwezi kujifunza kupitia kushindwa au makosa unayofanya.
Kuwa mnyenyekevu, jua unaweza kukosea, jua haupo juu ya wengine na jifunze kupitia makosa na kushindwa kwako.

9. UHALISIA; Msingi wa kujifunza.

Kitu kikubwa ambacho kushindwa kunatufundisha ni uhalisia. Kwa fikra za kawaida maisha ni marahisi sana. Watu watakudanganya mengi kuhusu maisha na mafanikio, fanya kazi hii utafanikiwa, fanya biashara hii utafanikiwa. Lakini unaposhindwa, ndiyo unakutana na uhalisia wa maisha ya kwamba kila mtu anaweza kushindwa. Na hapa ndipo kujifunza kunapoanzia.
Unaposhindwa, achana na zile hadithi za uongo ulizojazwa na uangalie uhalisia.

10. MAJUKUMU; Hatua ya kwanza ya kujifunza.

Watu wote ambao wanayachukua maisha yao kama jukumu lao, wanajifunza kupitia makosa wanayofanya na hata kushindwa wanakopitia. Tatizo lipo kwa wale ambao wanakimbia majukumu yao, wanaoona maisha yao yanatengenezwa au kubomolewa na watu wengine.
Kumbuka ya kwamba maisha yako ni jukumu lako, na hii ndiyo hatua ya kwanza kabisa ya kujifunza kupitia makosa yako.

11. UBORESHAJI; Lengo la kujifunza.

Hakuna mtu ambaye ni mkamilifu, na hivyo kitu cha kwanza unachopaswa kujifunza kwenye kushindwa ni kujiboresha zaidi kila siku. Watu wengi wamekuwa wakiwaangalia watu waliofanikiwa na kufikiri wamefika pale mara moja. Ukweli ni kwamba hawakujikuta pale, bali wamekuwa wakipiga hatua ndogo ndogo kila siku mpaka wamefika unapowaona sasa.
Unaposhindwa, kumbuka hizo ni hatua za wewe kuelekea kwenye mafanikio, unachohitaji ni kuangalia njia ya kuwa bora zaidi leo zaidi ya jana, na kuwa bora zaidi kesho zaidi ya leo.

12. MATUMAINI; Msukumo wa kujifunza.

Bila ya matumaini, maisha hayana maana. Kwa sababu kama tulivyojifunza, utashindwa mara nyingi kwenye maisha yako, huenda kuliko hata utakavyoshinda. Unahitaji kuwa na matumaini kwamba pamoja na kushindwa unakopitia, mambo yatakuwa mazuri baadaye. Pamoja na giza kubwa unalopita wakati wa kushindwa, mwisho kutakuwa na mwangaza.
Matumaini yanakusukuma kuweza kupita wakati mgumu wa kushindwa.

13. KUFUNDISHIKA; Njia ya kujifunza.

Kushindwa na kukosea ni jambo moja, kujifunza kupitia kushindwa na makosa yako ni jambo jingine tofauti. Ni lazima uwe unafundishika ndiyo uweze kunufaika na makosa unayofanya. Kama hufundishiki, utaendelea kurudia makosa yale yale au kushindwa kwenye mambo yale yale.
Maisha ni darasa, wale walio tayari kuifunza, wana kila cha kujifunza. FUNDISHIKA.

14. CHANGAMOTO; Kichocheo cha kujifunza.

Unaposhindwa unakutana na changamoto mbalimbali, unakutana na shida na magumu ambayo kwa kuyavuka unafikia mafanikio makubwa zaidi.
Hivyo unaposhindwa, au unapofanya makosa, chukulia hicho kama kichocheo cha wewe kujifunza zaidi na kuweza kufika kule unapotaka kufika.

15. MATATIZO; Fursa ya kujifunza.

Siku zote yachukulie matatizo yako kama ni fursa kwako kujifunza, usichukulie kama kikwazo, kwa kufanya hivyo hutaweza kusonga mbele. Unapoyageuza matatizo kama fursa kwako kujifunza, unaona njia nyingi za kutoka hapo ulipo na kufika unakotaka kufika.

16. UZOEFU MBAYA; Mtazamo wa kujifunza.

Unaposhindwa, hakuna shaka ya kwamba unaisikia vibaya. Umejipanga vizuri na unategemea kupata matokeo mazuri halafu unashindwa. Au umefanya makosa ambayo hukutegemea kama ungeweza kuyafanya, kama kusahau kitu ambacho ni muhimu na inakugharimu. Lazima utajisikia vibaya sana, unakuwa ni uzoefu mbaya kwako.

Tumia uzoefu huu mbaya, kujisikia huko vibaya kama mtazamo wa wewe kujifunza. Kila unapopitia hali usiyoipenda kama hiyo ya kushindwa au kufanya makosa, kumbuka ni wakati wa kujifunza.

17. MABADILIKO; Gharama ya kujifunza.

Unaposhindwa au unapofanya makosa, unapojaribu kurudia kile kile ambacho umefanya, huku ukitegemea kupata matokeo ya tofauti ni kujidanganya. Ni lazima uwe tayari kubadilika kama unataka kunufaika na kushindwa au makosa unayofanya. Mabadiliko ni magumu na watu hawayapendi, lakini wewe lazima uwe tayari kulipa gharama hii, kama unataka kunufaika na kushindwa au makosa yako.

18. UKOMAVU; Thamani ya kujifunza.

Baada ya yote hayo ni kipi unaondoka nacho kwenye kushindwa? Unaondoka na ukomavu, unaondoka na uzoefu kwamba njia ipi ni sahihi kupita na ipi siyo sahihi kupita. Usije ukarudia yale yale uliyofanya na hatimaye kurudi kwenye makosa yale yale. Hakikisha kwa kila kosa unalofanya, kwa kila unaloshindwa, basi unaondoka na somo la maisha yako, la namna unavyoweza kuwa bora zaidi.

19. Mambo matatu ya ukweli unayopaswa kujua kuhusu maisha;

Moja; maisha ni magumu, usijidanganye kwa namna yoyote ile kwamba maisha yatakuwa rahisi kwako. Lazima upambane, utaanguka, utakosea na utashindwa. Lakini mwisho wa siku kama utaendelea kusonga mbele, utafanikiwa.

Mbili; maisha ni magumu kwa kila mtu. Kitu kingine ambacho watu wanajidanganya kuhusu maisha ni kuona kama wengine maisha kwao ni rahisi. Kila mtu kuna mambo anapambana nayo kwenye maisha yake, usione kwa nje ukafikiri mambo ni rahisi, ukipewa viatu vya wengine unaweza usiweze kuvivaa kabisa.

Tatu; maisha ni magumu zaidi kwa baadhi ya watu kuliko kwa wengine. Na hili ni jambo ambalo watu wanaamua kuchagua, yaani unachagua maisha yako yawe magumu zaidi kuliko ya wengine. 

Kama kuamua kutokujifunza kupitia makosa yako mwenyewe, na hivyo kuyarudia yale yale kila siku.

20. Aina tano za watu ambao maisha ni magumu zaidi kwao.
Maisha ni magumu sana kwa watu wa aina hii;

1. Maisha ni magumu sana kwa watu ambao wamegoma kujifunza na wameacha kukua kimaarifa.

2. Maisha ni magumu mno kwa wale ambao wanajaribu kuukimbia uhalisia, au kupingana na uhalisia wa maisha.

3. Maisha ni magumu sana kwa wale ambao hawafikiri kwa usahihi, wale ambao wanafanya mambo kwa mazoea na kwa kuiga, bila ya kufikiri kwa kina.

4. Maisha ni magumu sana kwa wale ambao wanachukua muda sana kufanya mabadiliko pale mambo yanapobadilika. Wale ambao wanaendelea kung’ang’ania njia za zamani ambazo hazifanyi tena kazi.

5. Maisha ni magumu mno kwa wale ambao hawazifanyii kazi changamoto wanazokutana nazo kwenye maisha yao.

Usiwe katika kundi lolote la watu hao, usitake kuongeza ugumu wa maisha yako.

Ujumbe mkuu wa kitabu hiki ni mmoja; MAISHA NI KUSHINDA NA KUJIFUNZA. UKISHINDA FURAHIA NA JIFUNZE, UKISHINDWA JIFUNZE ZAIDI. USIKATE TAMAA PALE UNAPOSHINDWA, HUWEZI KUKWEPA KUSHINDWA KWENYE MAISHA YAKO, BALI UNAWEZA KUCHAGUA KUJIFUNZ AKUTOKANA NA KUSHINDWA NA HATA MAKOSA UNAYOFANYA.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>