Quantcast
Channel: AMKA MTANZANIA
Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

UCHAMBUZI WA KITABU; UNLEASHING THE POWER OF RUBBER BAND (Mafunzo Ya Uongozi Unaoendana Na Uhalisia)

$
0
0
Imezoeleka kwamba kiongozi ni mtu fulani ambaye anafanya kila ambacho anatakiwa kufanya, kulingana na taratibu ambazo zipo. Lakini siyo mara zote mambo yanakwenda kama taratibu zinavyotaka. Zipo changamoto nyingi kwenye uongozi ambapo inafika wakati kiongozi anapaswa kuchukua hatua huku akiwa hana uhakika na kile anachokwenda kufanya.
 

Mwandishi Nancy Ortberg anatuma mafunzo ya uongozi yanayoendana na uhalisia, siyo miongozo wala taratibu, bali uweze wa kufanya maamuzi kulingana na hali ambayo unakutana nayo kwa wakati husika. Nacy anatushirikisha yale aliyojifunza kwa viongozi wakubwa na pia uongozi wake kwenye kazi za misheni.

Karibu tujifunze misingi ambayo itatuwezesha kuwa viongozi bora wa maisha yetu, familia zetu, jamii zetu, biashara zetu, kazi zetu na hata nafasi nyingine tunazopata kwenye jamii na hata taifa kwa ujumla. Kwa kuwa kila mmoja wetu ni kiongozi, ndiyo hata wewe ni kiongozi, basi ni muhimu sana tujifunze haya.

1. Uongozi bora unapatikana kwa watu ambao ni wakimya na wasioonekana ambao wanatengeneza mazingira mazuri kwa wengine kuweza kufanya kazi zao kwa ubora. Viongozi hawa hutawaona kwenye kurasa za mbele za magazeti au habari za kwenye tv.
Tatizo kubwa la jamii zetu ni kuamini kwamba kiongozi bora ni yule anayeonekana na kila mtu, na hivyo hili kuwasukuma watu wafanye mambo yanayoonekana hata kama siyo muhimu ili nao waonekane kwenye vyombo vya habari. Wapo watu ambao hujawahi kuwasikia kabisa, lakini kazi zao zina mchango mkubwa sana kwa hapo ulipo sasa.

2. Viongozi bora wanatengeneza utamaduni, halafu utamaduni unawabadili watu. Viongozi wa kawaida wamekuwa wanatengeneza mifumo inayowalazimisha watu kubadilika, lakini mifumo hii imekuwa inashindwa. Utamaduni unawafanya watu wawe tayari kubadilika wenyewe, na siyo kuwasukuma watu kubadilika.

3. Kiini cha uongozi ni matumaini. Uongozi ni matumaini kwamba tunaweza kubadili vitu ambavyo vinatakiwa kubadilishwa na pia kutengeneza vitu ambavyo kwa sasa tunaona hatuwezi kutengeneza. Matumaini yanawapa watu nguvu ya kusonga mbele, kusamehe na kuweza kuzishinda hofu. Viongozi bora wanaweza kuwafanya watu wawe na matumaini.

4. Viongozi bora wanafikiria kuhusu maono makubwa waliyonayo. Na hawaishii tu kuyafikiria, bali wanayaishi maono hayo kila siku, maisha yao yote yamezungukwa na maono yao. Wanajua ni wapi wanataka kufika na watawezaje kufika. Kama kiongozi hana maono, hawezi kuwa kiongozi bora na watu hawawezi kumfuata. Maono hayapaswi tu kuwa kwenye maandishi, bali yanapaswa kuwa kwenye moyo wa kila mtu anayeguswa na uongozi unaobeba maono.

5. Maono kwa kiongozi ni kitu muhimu kwa sababu ndiyo yanamchochea, yanamkumbusha na kumwezesha kuwa na ndoto kubwa za kule anakokwenda. Maono ndiyo yanawapa watu matumaini kwamba mambo yanazidi kuwa mazuri kadiri siku zinavyokwenda.

6. Viongozi bora wanachukulia taasisi wanazoongoza kama kiumbe hai. Kwa kufanya hivi wanaondoa ile hali ya watu kuchukulia ni sisi dhidi ya taasisi. Kwa sababu taasisi ni watu, basi viongozi bora wanafanya kila mtu ajione yeye ni sehemu ya taasisi. Asijione kama anapambana na taasisi, bali ajione kama yeye ni mmoja wa wanaoiwezesha taasisi kupiga hatua.

7. Ili kuweza kuiongoza taasisi vizuri, viongozi wanapaswa kujadili maono ya taasisi pamoja na wale wote waliopo kwenye taasisi. Ni rahisi kuwaambia watu unaowaongoza kwamba kuanzia sasa tunakwenda hivi, au lazima kila mtu afanye hivi. Wanaweza kukubaliana na wewe, lakini wasifanye. Ila unapowashirikisha katika kutengeneza maono na mipango ya taasisi kila mtu anatoa ushirikiano wa kutosha kwa sababu anajua amehusika katika kutengeneza maono na mipango ya taasisi.

8. Katikati ya maono ya taasisi na uhalisia kuna uwazi. Taasisi inakuwa na maono yake, ni wapi inataka kufika. Lakini pia kuna uhalisia, namna ambavyo mambo yanakwenda. Nafasi hii kati ya maono na uhalisia inazibwa na mikakati. Mikakati inatoa majibu ya tunafikaje pale tunapotaka kufika, tunawezaje kutoka hapa tulipo sasa na kufika kule tunakotaka kufika. Mikakati inaundwa kwa vitu viwili au vitatu ambavyo vitakuwa ndiyo mkazo wa taasisi.

SOMA; Makosa Makubwa Matano Yanayoweza Kukuharibu Wewe Kama Kiongozi.

9. Viongozi bora wanajua jinsi ya kuchagua vipaumbele ambavyo taasisi itahusika navyo. Yapo mambo mengi ambayo kila taasisi inaweza kufanya, lakini kujaribu kufanya yote ni kutengeneza njia ya kushindwa. Viongozi bora wanajua kuchagua yale muhimu na kukataa mengine ambayo siyo muhimu. Hii inaiwezesha taasisi kutumia vizuri rasilimali zake na kuweza kufanya makubwa.

10. Viongozi bora wanatambua na kuthamini mchango wa kila mtu aliyepo kwenye taasisi. Viongozi bora wanajua hata anayefanya usafi kwenye taasisi kubwa, ni mtu muhimu anayechangia maendeleo ya taasisi hiyo. Maana kama eneo lisipokuwa safi, hakuna atakayeweza kufanya kazi zake vizuri. Viongozi wa kawaida wamekuwa wakiona kazi za wengine kama za kawaida, kwa kuwa hazina upekee, viongozi bora hawafanyi hivi. Wanawajua vizuri watu wao na kazi wanazofanya, na huwasifia na kutambua juhudi wanazoweka.

11. Viongozi bora wanajua tofauti ya TATIZO na MVUTANO, na hii inawawezesha kuchukua hatua muhimu zinazowaletea mafanikio makubwa kiuongozi. TATIZO linapaswa kutatuliwa na MVUTANO unapaswa kusimamiwa vizuri. Viongozi bora wanajua kutatua matatizo na kusimamia mivutano. Viongozi wa kawaida hawajui hata tofauti ya tatizo na mvutano, hivyo wanajikuta wakichukua hatua ambazo siyo sahihi na hivyo kuongeza matatizo zaidi. Tatizo ni ile hali ambayo unaweza kuitatua mara moja na mambo yakaenda vizuri. Mvutano ni ile hali ambayo huwezi kuitatua mara moja, mara nyingi mvutano unahisisha pande zaidi ya moja na hivyo unahitaji kwenda vizuri na pande zote mbili.

12. Kusimamia mvutano siyo swala la kupata au kupoteza, bali swala la kuwa na msawazo baina ya pande zinazohusika. Unahitaji kuwa na msawazo (equilibrium) na siyo usawa (balance). Msawazo unabadilika kadiri mambo yanavyokwenda, lakini usawa haubadiliki. Viongozi wanajua kusimamia mvutano, unahitaji kubadilika kadiri mambo yanavyobadilika, na siyo kuendelea kufanya kwa mazoea.

13. Kila kiongozi huwa anapitia nyakati ngumu katika uongozi wake. Huu ni ule wakati ambapo anakumbana na hali ambayo ni ngumu na yenye changamoto. Anakuwa hajui ni hatua ipi sahihi ya kuchukua, na chochote atakachofanya, anaweza kufanikiwa au kushindwa. Viongozi bora wanachukulia nyakati hizi kama nafasi ya wao kukua zaidi, wanachukua maamuzi sahihi na wanakuwa tayari kupokea lile linalotokea.

SOMA; Dalili Kumi Kwamba Tayari Wewe Ni Kiongozi.

14. Viongozi bora mara zote hujiuliza swali hili muhimu kabla hawajaanza kufanya chochote. Swali lenyewe ni JE HIKI TUNACHOKWENDA KUFANYA, KINATUSOGEZA KARIBU NA MAONO YETU? Hawakurupuki na kuanza kufanya kitu kwa sababu tu wanaweza kufanya au kwa sababu kila mtu anafanya. Wanaangalia maono yao kwanza, na kuhakikisha kila wanachofanya, kinawasogeza kwenye yale maono yao. Hii inawawezesha kuwa na vipaumbele bora kwenye kazi zao.

15. Viongozi bora wanajua kuna tofauti kubwa kati ya mtu asiyeweza na mtu ambaye yupo kwenye sehemu ambayo haiendani na yeye. Viongozi hawa hawawalaumu watu pale wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao, badala yake wanaangalia je ni majukumu ambayo yanaendana na uwezo wao. Viongozi hawa wanajua kila mtu ana uwezo tofauti, na kama mtu akipewa majukumu yanayoendana na uwezo wake, atayafanya vizuri sana. Hivyo viongozi bora, wanahakikisha kwamba watu sahihi wapo kwenye eneo sahihi ili kuweza kuleta matokeo bora.

16. Viongozi bora wanajua wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha taasisi zao zinakwenda vizuri. Wanajua ya kwamba wao ndiyo wanaoangaliwa kwa chochote kinachotokea, iwapo taasisi inafanya vizuri wao ndiyo wa kwanza kuangaliwa, na ikifanya vibaya wao pia ndiyo wa kwanza kuangaliwa. Viongozi bora wamekuwa hawajaribu kukimbia majukumu haya kwa namna yoyote ile, bali wanayapokea na kuhakikisha wanayafanya vizuri.

17. Moja ya kazi muhimu sana kwa kiongozi bora ni kutengeneza timu imara katika taasisi. Viongozi bora wanajua timu inaweza kutoa matokeo makubwa kuliko matokeo ya mtu mmoja mmoja yakikusanywa pamoja. Yaani ikiwa watu wawili kila mtu atafanya kazi kivyake, na ukajumlisha matokeo yao, yanakuwa madogo kuliko watu hawa wanaposhirikiana pamoja kwenye kazi. Hivyo viongozi bora wamekuwa hawaruhusu mtu mmoja kujiona ni bora kuliko wengine, bali wanahakikisha kila mtu anaona umuhimu wa mwenzake katika mafanikio ya taasisi.

18. Uongozi ni ahadi ya maendeleo kwenye taasisi. Kila kiongozi anapimwa kwa mambo mapya na makubwa ambayo amefanya. Hakuna kiongozi anasifiwa kwa kuhakikisha kila kitu kimekwenda sawa. Bali viongozi wanasifiwa kwa mapya na makubwa waliyofanya. Hivyo viongozi bora wamekuwa wanahakikisha maendeleo ni ahadi kuu na muhimu kwao.

19. Viongozi bora wanajua mtu muhimu kuliko wote kuongoza ni wao wenyewe. Ni rahisi kuwasimamia wengine, lakini ni vigumu sana kujisimamia wewe mwenyewe. Viongozi bora wanalijua hili na wanahakikisha wanalifanyia kazi ili lisiwe kikwazo kwa uongozi wao. Viongozi bora wanajijengea nidhamu imara na kujiwajibisha ili kuhakikisha wanafanya kile ambacho wamepanga na kuahidi.

20. Jukumu kubwa na gumu kwa kila kiongozi na mtu mwingine yeyote ni kujitambua. Na hili ndiyo linawatofautisha viongozi na watu wengine wa kawaida. Viongozi bora wanajitambua, wanajua ni mambo uimara wao na udhaifu wao. Wanajua ni maeneo gani wanahitaji ushirikiano wengine na wanajua ni maeneo gani wanaweza kutoa mchango mkubwa. Kazi ya kujitambua ni ngumu sana ndiyo maana wengi hawawezi kuwa viongozi bora.

Rafiki yangu, je unaweza kutumia misingi hii ya uongozi tuliyojifunza hapa na kujitengeneza kuwa kiongozi bora? Kumbuka kwamba popote ulipo, wewe ni kiongozi, huhitaji kuwa na kundi la watu ndiyo uitwe kiongozi, pale ulipo unahitaji kujiongoza wewe mwenyewe na yeyote anayekuzunguka.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

Viewing all articles
Browse latest Browse all 1010

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>