Karibu tena msomaji wa AMKA MTANZANIA kwenye kipengele hiki cha ushauri kwa wahitimu ambapo unapata makala yenye ushauri kwa wahitimu na hata watu wengine kwa ujumla. Leo tutaona ni jinsi gani njaa inaweza kukusukuma kufikia mafanikio na pia ni jinsi gani njaa inaweza kukuzuia kufikia mafanikio.
Tunaishi kwenye zama za taarifa ambapo wenye taarifa sahihi ndio wanaopata mafanikio makubwa kwenye jambo lolote wanalofanya. Hivyo kama bado umekariri kuishi kwa mazoea kama ulivyodanganywa kwenye mfumo wa elimu tayari uko kwenye matatizo.
Njaa itakayokupatia mafanikio.
Njaa itakayokufanya ufikie kwenye mafanikio makubwa ni njaa ya kujifunza na njaa ya kufikia mafanikio.
Ni lazima uwe na njaa kali ya kujifunza kila kitu kinachohusiana na kazi au biashara unayofanya au unayotaka kufanya ndio uweze kufanikiwa. Lazima uwe na njaa kali ya kufanikiwa na kutokata tamaa au kuzuiwa na chochote mpaka pale utakapofikia mafanikio unayotazamia. Hii ndio njaa itakayokuletea mafanikio makubwa.
Unawezaje kuitengeneza njaa hii?
Unaweza kutengeneza njaa hii kwanza kwa kuweka malengo makubwa kwenye maisha yako. Kujua jinsi ya kuweka malengo makubwa na utakayoyafikia soma; Jinsi ya kuweka malengo makubwa utakayoyafikia.
Baada ya kuweka malengo haya weka utaratibu wa kujisomea na kujifunza kila siku, ndio namaanisha KILA SIKU. Hakikisha siku yoyote haipiti bila ya kusoma kitu chenye manufaa kwenye maisha yako. Kitu hivho kiwe cha kujifunza na kukusogeza mbele kufikia lengo lako. Ukisoma gazeti umejihabarisha hivyo usihesabu.
Unaweza kujifunza kila siku kwa kujisomea vitabu vizuri ambavyo vinapatikana hapa AMKA MTANZANIA na pia kusikiliza vitabu vilivyosomwa(AUDIO BOOK) ambapo itakuwa rahisi kwako kujifunza popote ulipo.
Kama huna kitabu chochote cha kusoma kwa sasa nitumie email kwenye amakirita@gmail.com na nitakutumia vitabu vitatu, think and grow rich, the richest man in babylon na rich dad poor dad. Na kama utapenda kupata vitabu vya kusikiliza AUDIO BOOKS bonyeza maandishi haya na utapata maelekezo ya vitabu vinavyopatikana.
Njaa hii ya kutaka kufikia mafanikio na kujifunza inaambatana na kufanya kazi kwa bidii na maarifa. Asikudanganye mtu yeyote huwezi kufikia mafanikio bila ya kufanya kazi, ni lazima ufanye kazi sana iwe ya kufikiria au ya nguvu ni lazima ufanye kazi.
Njaa inayoweza kukuondoa kwenye mafanikio.
Njaa ya chakula kama ukiitumia vibaya inaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwako kufikia mafanikio makubwa. Kama una njaa, namaanisha huna chanzo cha kipato na una mahitaji makubwa inaweza kuwa rahisi sana kwa watu wengine kukutumia wewe bila ya wewe kujua.
Hiki ndio kinatokea kwa kiasi kikubwa kwa watu wengi walioajiriwa. Wengi wanajikuta wakipata kipato cha kuendesha maisha tu na kushindwa kufanya maendeleo mengine. Na wakati huo huo wanashindwa kuondoka kwenye kazi hiyo kwa sababu wanaogopa maisha yatakuwa magumu sana. Hivi ndivyo njaa ya chakula inavyoweza kuwafanya wawe watumwa kwa zaidi ya miaka ishirini. Usikubali kuingia kwenye mtego huu au kuendelea kuwepo kwenye mtego huu.
Kuwa makini sana na njaa hii isijekuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio makubwa unayostahili kufikia. Wewe ni zaidi ya kile unachokifanya au unachofikiri kufanya.
Tumia njaa hizi mbili vizuri ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Nakutakia kila la kheri katika kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
TUKO PAMOJA.