Yapo maisha ambayo kwa kawaida mtu yeyote akiwa nayo, hauhitaji uwe una digirii ya uchumi wala hahitaji uwe mtabiri, kwa maisha hayo utajua tu, ni lazima mtu huyo awe maskini hata afanyaje. Ni maisha hayo hayo ambayo nakutana nayo karibu kila siku mtaani na watu wengi wanayo.
Ni kitu ambacho huwa kinaniuma lakini huo ndiyo ukweli na hayo ndiyo maisha ambayo wengi wameyachagua na yanawepeleka kwenye shimo la umaskini. Kuna wakati huwa sielewi ni nini tatizo hasa linalowakumba wengi na kuamua kuishi maisha ya namna hiyo. Ni maswali ambayo hubaki yakiniumiza kichwa na kuniacha njia panda.
Lakini kabla sijendelea hivi ulishawahi kujiuliza ama kutambua ni kwanini watu wengi wanaishi maisha ya hovyo au kiholela. Nikiwa na maana ni maisha ya kiabunuasi, yakubahatisha na ambayo hayana uhakika wa kesho? Ni maisha hayo ambayo wengi wanayo na wanayaishi.
Hata ukija kuchunguza uhovyo huo kwa wengi huwa ni wa kujitakia au kujitengenezea, ingawa wao kubaki kusingizia mambo ambayo yako nje kwao na kuusau ukweli ulio ndani mwao ambao unawakwamisha. Haya ni maisha ambayo yamekuwa kama mazoea kwa wengi na kimekuwa kikwazo kikubwa cha mafanikio.
Kwa vyovyote vile iwavyo, hata wewe ukiwa na maisha ya namna hii nakupa uhakika hutafika popote kimafanikio hata ufanye nini. Sanasana utaishia kuwa na maisha yaleyale ambayo umekuwa nayo kila siku. Je, unajua ni maisha gani ambayo ukiwa nayo lazima ukwame na itakuwa ngumu kwako kusonga mbele?
1. Kupenda mafanikio ya harakaharaka.
Watu walio wengi wanapenda sana mafanikio ya haraka. Kwa mfano, ukitaka kumpa mtu mpango wa mafanikio na ili akuelewe vizuri na haraka, mpe mpango unaompa uhakika wa kutajirika kesho. Hili ni tatizo kubwa sana linalowakabili watu wengi. Watu wengi wanaishi kwa kutegemea mafanikio ya haraka kitu ambacho ni hatari.
Na ndio maana utakuta watu wanashindwa kujihusisha na shughuli za maana na matokeo yake wanakuwa wapo tayari kutafuta njia nyingi za mkato ili kufikia mafanikio hayo. Haya ndiyo matokeo ya michezo ya bahati nasibu na mingineyo ili kujipatia pesa. Suala la mipango ya maendeleo ya muda mrefu kwa watanzania walio wengi halipo.
Suluhisho.
“Jiwekee mipango na malengo imara ya kukufikisha kwenye mafanikio makubwa, acha kutegemea mafanikio ya haraka utakwama bila ubishi.”
![]() |
KAMA UNAAMINI UNA MIKOSI, HUWEZI KUFANIKIWA. |
2. Kushabikia mambo.
Kwa Watanzania walio wengi uzoefu unaonyesha wengi wao ni watu wa kushabikia sana mambo ambayo hata yasiyowahusu. Ni tabia ambayo imekuwa ikijengeka siku hadi siku. Sio ajabu sana kwa sasa, kukuta watu wakiongelea jambo fulani kwa muda mrefu kuzungumzia maisha ya watu wengine tena kwa ushabiki mkubwa.
Bila shaka umeshawahi kuona makundi kama haya ambayo mara nyingi yanaongelea mpira, siasa na mambo mengineyo mengi ambayo hayana msaada kwao. Kuongelewa hayo mambo inaweza isiwe mbaya ila iwe kwa kiasi. Vinginevyo utajikuta unapoteza muda wako mwingi kumzungumzia Neymar analipwa kiasi gani na kusahau maisha yako.
Suluhisho.
“Jifunze kuwa shabiki mkubwa wa maisha yako, acha kushabikia maisha ya watu wengine hayatakusaidia.”
3. Kupoteza muda.
Muda ni kitu ambacho hakina thamani kabisa kwa watu wengi. Walio wengi wengi hujikuta wakipoteza muda wao kwa mambo madogo madogo ambayo hata hayana msaada kwao. Huu ni mfumo wa maisha ambao umezoeleka na wamekuwa wakiuishi watu wengi hivi kwa mazoea na imekuwa kama utamaduni.
Mara nyingi sio ajabu sana kusikia mtu akikwambia ngoja niende mjini nikapoteze muda. Maanake mtu huyo yeye anajiona ana muda mwingi kiasi cha kwamba anao mwingine wa kupoteza. Kwa maisha haya ya kuishi kupoteza muda ambao ungetumika kukupa mafanikio, kama utayaendeleza uwe na uhakika itakuwa ni ngumu sana kwako kufanikiwa.
Suluhisho.
“Usipoteze muda wako hata dakika moja kwa mambo yasiyo ya msingi, tumia muda wako kwa mambo ya mafanikio, utakuwa mshindi na utafika mbali sana kimafanikio”
4. Kuishi bila malengo.
Kwa bahati mbaya pia watu walio wengi wana tatizo la kuishi maisha yasiyo na malengo maalum. Hapa hata ubishe vipi huu ndio ukweli. Wengi hujikuta wakiwa na malengo ya mdomoni ambayo siyo ya kuandikika na matokeo yake baada ya muda mfupi hujikuta wamesahu hayo malengo yao na kurudia maisha yao ya awali.
Bila kujiwekea malengo utajikuta unaishi maisha yaleyale. Maisha ya kuishi tu ilimradi kuna kucha na kukosa mwelekeo maalumu. Ukiona unaishi maisha hayo, elewa kabisa kuwa huna mafanikio. Kukosa malengo, hicho ndicho kitu kinachowaangusha wengi katika harakati za kufikia mafanikio makubwa.
5. Kujiona una mikosi.
Fikra nyingi za wengi wanafikiri hawafanikiwi kwa sababu wana mikosi. Hayo ndiyo mawazo yao. Kwa kadri wanavyozidi kuamini hivyo, ndivyo ambavyo huzidi kufanya mambo mengi kwa mkabala huohuo wa kimkosi na kujikuta hawafaniiwi kufika popote. Ni mawazo hayahaya ambayo wengi wetu wanayo kila kukicha na yanawaangusha.
Kwa maisha kama haya , hupelekea maisha ya wengi kwa mabaya siku hadi siku. Ni vyema kuwa makini na mawazo na maisha uliyonayo kwa ujumla ili uweze kufanikiwa.
Nakutakia siku njema na mafanikio makubwa yawe kwako na endelea kujifunza kupitia AMKA MTANZANIA kila siku.
Kwa makala nyingine nzuri pia karibu kwenye DIRA YA MAFANIKIO kwa ajili ya kujifunza na kuboresha maisha yako.
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,
E-mail;dirayamafanikio@gmail.com