Changamoto ya ajira ni moja kati ya changamoto kubwa sana inayowakabili vijana wengi hususani wanaomaliza masomo yao ya vyuo. Si ajabu sana kusikia kijana yule kamaliza chuo kile lakini akiwa hana kazi. Hiyo ni changamoto inayowakabili vijana wengi na ni kweli ipo na inasumbua. Vijana wengi huzunguka huku na kule wakitafuta kazi bila kupata kazi hasa hizo walizozisomea.
Pamoja na changamoto hiyo kubwa ya ajira inayojitokeza, lakini kuna wakati huwa yapo makosa yanayowafanywa na vijana wengi wanaotafuta kazi. Na kwa makosa hayo hupelekea kukosa kazi hizo na kubaki mtaani kwa muda mrefu sana bila ajira yoyote. Bila shaka umeshawahi kukutana au kuonana na mtu ambaye yupo mtaani kwa muda merfu bila kazi yoyote.
Je, umeshawahi kujiuliza tatizo kwa watu hawa hasa ni nini? Unaweza ukaja na jibu rahisi tu na kuniambia hakuna kazi siku hizi. Hilo linaweza likawa ni sawa, lakini je huo ndio ukweli halisi? Ukija kuchunguza kwa makini utagundua watu hawa ambao wengi wao wanatafuta kazi kwa muda mrefu bila mafanikio, wanafanya baadhi ya makosa ambayo yana wagharimu kupata kazi hizo wanazozitafuta.
Je, unajua ni makosa gani ambayo watu hawa wanafanya na kuwanyima kazi hizo?
1. Kosa la kuchagua kazi sana.
Watu wengi ambao wanajikuta wao ni wa kubaki mtaani kwa muda mrefu kosa mojawapo kubwa wanalolifnya ni watu wa kuchagua kazi sana. Mathalani,utakuta mtu amesomea digirii ya sociology (Mambo ya jamii), lakini mtu huyu inapojitokeza kazi nyigine ambayo ingeweza kumuingizia kipato tofauti na kile alichosomea inakuwa ni ngumu sana kwake kuifanya.
Kwa mwendo huu wa kuchagua kazi siku hadi siku hujikuta ni watu wa kukosa kazi kila kukicha. Hili najua unalijua vizuri na umeshakutana na watu wa namna tena wengi tu, ambao wao ni watu wa kuchagua kazi nzuri, kazi ambayo wanavigezo nayo kichwani mwao. Hilo si jambo baya ila angalia na mzaingira ya wewe ulipo. Jitazame una kazi hadi kupelekea kuchagua kazi sana, vinginevyo utaendelea kupigika mtaani bila kuwa na chohote.
Suluhisho
Najua unailewa vyema hali ya maisha uliyonayo. Kama upo kwenye wakati wa kutafuta kazi acha kutafuta sana kazi. Fanya kazi, kama ni uchaguzi utaufanya ukisha pata kazi hiyo kwanza, itakayokufanya uishi.
![]() |
UTAUMIA SANA KILA UNAPOIKOSA KAZI YA MSHAHARA MKUBWA |
2. Kosa la kutaka kazi ya mshahara mkubwa.
Wengi wanaotafuta kazi na kujikuta kuzikosa ni watu wa kutafuta mshahara mkubwa siku zote. Utakuta mtu hana kazi lakini inapotokea anapata kazi hiyo shida inaanza kujitokeza kwenye mshahara. Anakuwa ni mtu wa kupatanisha na kutaka mshara mkubwa ambapo waajiri wengi hupelekea kushindwa kuwaajiri watu wa namna hiyo.
Kwa mazingira kama hiyo inakuwa ni ngumu kupata kazi. Kwa namna yoyote ile ili uweze kupata kazi ni muhimu kujifunza, kama hauna kazi tafuta kazi kwanza. Acha kutafuta mshahara mkubwa. Kama utaendelea kutafuta mshahara mkubwa, elewa utakosa kazi nyingi, na utaendelea kupishana na ajira kila kukicha. Hicho ndicho kitu unachotakiwa kukiepuka kama upo kwenye hali ngumu ya kutafuta kazi.
Suluhisho
Kwa kipindi ambacho huna kazi acha kuangalia sana suala la mshahara. Mshahara wako pengine utaongezeka zaidi hadi pale utakapotoa thamani inayotakiwa.
3. Kosa la kutafuta eneo bora la kazi.
Pia hili ni tatizo linawakabili vijana wengi kukosa kazi. Kuna watu wanakuwa wanapata kazi lakini tatizo linakuja pale wanapoambiwa wakafanye kazi katika eneo fulani, hapo ndipo inakuwa ngumu. Utakuta mtu anaishi Dodoma lakini anapopata kazi nakuambiwa kazi hiyo ipo Tabora, hapo ndipo ugumu unapoanza na kujikuta wanaachana na kazi hiyo.
Kwa vijana walio wengi ukija kuangalia hayo ndiyo matatizo makubwa yanayowapelekea kukosa kazi. Kama unafanya makosa hayo ni muhimu kwanza kuyaepeka ili kujipatia kazi unayohitaji.
Angalizo
Ikiwa utandelea kushikilia sababu hizo katika harakati zako za kutafuta kazi, basi hakikisha una mbadala wa kukuingizia kipato, kinyume cha hapo acha kusumbua watu kwa pesa za matumizi.
Karibu pia kwenye DIRA YA MAFANIKIO kuweza kujifunza na kujipatia maarifa ya kuboresha maisha yako.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
Ni wako rafiki katika mafanikio,
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,
E-mail;dirayamafanikio@gmail.com