Inawezekana kabisa ukawa unaona mambo yako ni magumu, malengo uliyonayo ni kama hayatimii na maisha kwa ujumla unaona hayasogei karibu katika kila eneo la maisha yako. Hali kama hii inapokutokea ni rahisi sana kuweza kukukatisha tamaa na kuona kila kitu basi tena hakiwezekani katika maisha yako na maisha yako yote yamefikia hapo.
Kitu cha kujiuliza ni kweli je, kama upo katika hali kama hiyo maisha yako ndiyo basi hayawezekani tena kubadilika? Bila shaka hapa jibu ni HAPANA. Siku zote katika maisha yako usiamini kuwa hapo ulipo ndio umeganda huwezi kutoka tena kimaisha, hiyo haiwezekani na pia na kukatalia kwa nguvu zote.
Kwa kawaida mambo yote yanabadilika ikiwa pamoja na maisha yako. Hakuna tatizo au hali yoyote ngumu utakayoweza kudumu nayo milele, labda pengine wewe mwenyewe uamue kwa kutokuweza kuchukua hatua sahihi. Kama ni hivyo maisha yanabadilika, kwa sababu hiyo tu, hata wewe unauwezo wa kubadili maisha yako bila kuzuiliwa na kitu ikiwa umeamua kweli.
Itawezekana kwako kubadili maisha yako, ikiwa utaachana na baaadhi ya mambo ambayo yamekuwa yakikukwamisha na badala yake kuchukua hatua imara unazotakiwa kuzifuata kila siku, ili kubadili maisha yako. Kama utakuwa mtu wa vitendo katika hili, tambua ni lazima maisha yako yabadilike. Je unajua ni hatua zipi muhimu za kubadili maisha yako?
Hizi Ndizo Hatua 6 Muhimu Za Kuweza Kubadili Maisha Yako Kabisa.
1. Weka nguvu zako katika kubadili kitu kimoja kwanza.
Hata kama maisha yako ni magumu sana usitake kubadili mambo yako mengi kwa pamoja na mara moja. Anza kubadili kitu kimoja kimoja ukimaliza unaanza kitu kingine. Hiyo itakusaidia kuweza kufanikisha malengo yako kwa urahisi kwa sababu nguvu zako nyingi unakuwa unaziweka pamoja, kinyume cha hapo ukishindwa usishangae sana.
2. Anza kwa kidogo.
Nina uhakika hili umewahi kulisikia mara nyingi, lakini huo ndiyo ukweli. Kabla hujakimbia mbio ndefu ni vyema ukaanza na mbio fupi kwanza ili kupata uzoefu. Ndivyo na maisha yetu yapo hivyo. Ni muhimu kuanza kidogo kidogo tena katika kile unachokifanya na mwisho wa siku utafanya kwa ukubwa zaidi baada ya kuwa na uzoefu wa kutosha.
3. Fanya mabadiliko kila siku.
Mabadiliko unayotaka kufanya yasiwe kama ya zima moto, yafanye kila siku. Kama unaandika andika kila siku. Kama unaimba imba kila siku hata kama ni kidogo. Kwa kufanya hivyo utashangaa na kuona maisha yako yanabadilika kuliko hata unavyoweza kufikiri. Acha kabisa ile tabia ya kufuata malengo yako leo kesho unayaacha kidogo tena, utakwama.
4. Jitoe kuhakikisha malengo yako yanatimia.
Hakuna utakachoweza kukitimiza katika maisha yako kama hutaweza kujitoa kikamilifu kuona malengo yako yanatimia. Kama umeamua kuna kazi utaifanya wakati fulani, ifanye acha kuahirisha. Kama umejipangia kuamka kila siku asubuhi na mapema, fanya hivyo pia. Ikiwa utajitoa katika hili, maisha yako kwa vyovyote vile ni lazima kubadilika.
5. Kuwa na ushirika na watu sahihi.
Malengo yako hataweza kutimia ikiwa wewe kama wewe. Unahitaji watu wa kuweza kukusaidia. Watu hawa kwako ni lazima wawe sahihi kwako ambao watakutia moyo na siyo kukukatisha tamaa kwa namna yoyote ile. Kwa kuwa na watu hawa watakusaidia kuweza kutimiza malengo yako kwa urahisi, pengine kuliko ambavyo ungebaki peke yako.
SOMA; Hapa Ndipo Unapoweza Kuwapata Watu Watano Wanaokuzunguka Watakaokuwezesha kufikia Mafanikio Makubwa.
6. Furahia kile unachokifanya.
Kila siku chukua dakika chache kuweza kuangalia na kufurahia kile unachokifanya. Hii ni njia rahisi kwako ya kuweza kukupa hamasa na kukusaidia kuweza kusonga mbele kwa urahisi zaidi. Hivyo, ni muhimu kwako kufanya hivyo kila siku ili kupima ni wapi hasa ulipofikia kwa kile unachokitenda.
Huu ndiyo ukweli. Kwa kufuata hatua hizo muhimu katika maisha yako uwe na uhakika maisha yako ni lazima yatabadilika kwa namna yoyoe ile pengine wewe uwe hutaki. Kitu kikubwa kwako weka katika vitendo.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza zaidi.
TUNAKUTAKIA KILA LA KHERI KATIKA SAFARI YAKO YA MAFANIKIO,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,