Katika maisha yetu mara nyingi huwa tunajikuta ni watu wa kupoteza vitu vingi sana. Vitu ambavyo huwa tunavijutia na kuumia sana pale tunapovipoteza. Kuna wakati huwa tunapoteza pesa, kazi, muda, jamaa zetu wa karibu na mengine mengi tu. Lakini pamoja na mambo hayo yote kupotea huwa kipo kitu kimoja ambacho ukikipoteza maisha yako yanakuwa yapo hatarini sana.
Kitu hiki kimefanya maisha ya wengi kurudi nyuma siku hadi siku. Na wengi kwa kutokujua huwa wanakipoteza hiki bila kujua na kujali. Kitu hiki ambacho wengi wetu huwa wanakipoteza sana ni fursa zinazojitokeza katika maisha yao. Wengi huwa wanapoteza fursa zao kwa kuzidharau na pengine kuziona ni ndogo hivyo hujikuta ni watu wa kuziachia fursa hizo.
Katika maisha yako ili uweze kufanikiwa kwa haraka ni lazima kujifunza kwako kutumia fursa vizuri zinazojitokeza mbele yako bila kujali udogo wake au ukubwa zilivyo. Watu wengi kwa kutolijua hili huwa ni watu wa kupoteza fursa nyingi ambazo kama kweli wangeweza kukaa chini na kuzitendea haki, leo hii wangekuwa mbali sana kimafanikio kuliko pale walipo sasa.
Jaribu kufikiria juu ya hili utaugundua ukweli huu ninaokwambia. Ni mara ngapi ambapo umeshawahi kuharisha kufanya jambo Fulani hivi ambalo lingeweza kukuingizia pesa kwa sababu ya sababu zako ndogo tu. Ama jiulize tena ni kipi ambacho kimekuwa kukupelekea kufanya hivyo? Pengine hata hujui lakini ukweli ndio huo umekuwa ukipoteza fursa nyingi sana ambazo zinakufanya ushindwe kufanikiwa.
Kwa kuendelea kupoteza kitu hiki ndivyo jinsi ambavyo unakuwa upo mbali na mafanikio na kufanya maisha yako kuwa magumu. Hii iko hivyo kwa sababu hauwezi kufanikiwa kama wewe utakuwa ni mtu wa kuchezea fursa kila mara. Jaribu kuangalia wale wote unaowajua ambao kwa namna moja au nyingine walichezea fursa utagundua mafanikio kwao hakuna.
Siri mojawapo kubwa ya mafanikio ambayo unaweza kuitumia na kukufikisha mbali ni kujifunza kuitumia kila fursa ambayo unayoipata katika maisha yako vizuri. Ukiweza kutumia fursa vizuri utafika mbali sana kimaisha na wengine kubaki kukushangaa. Watu wenye mafanikio ni watumiaji wazuri sana wa fursa zinazojitokeza mbele yao. Huwa hawafanyi kosa katika hilo.
Acha kupoteza muda wako bure kwa kuwa mtu wa kuchagua fursa za kuzifanyia kazi. Kuwa mtu wa vitendo kwa kuzifanyia fursa zako kazi. Kwa kadri unavyozidi kuzifanya kazi fursa hizo, ndivyo maisha yako yatakuwa bora zaidi siku hadi siku. Hivi ndivyo unavyoweza kuwa shujaa wa maisha yako kwa kutumia fursa zako vizuri na kufanikiwa.
Wakati unapoona wengine wanaziacha fursa ambazo kwa macho yako unahisi zingewaza kuwasaidia wewe zichangamkie. Kumbuka kama utakuwa unapoteza fursa tu, tambua siyo rahisi kwako tena fursa hizo kuweza kukurudia kwa mara nyingine kama unavyofikiri.
Hivyo kitu cha kuelewa hapa, kama wewe unaendelea kupoteza fursa zako, itakuwa ni ngumu sana kwako kuweza kusonga mbele kimafanikio. Kwani tabia huleta mazoea kwa mazoea hayohayo unaweza ukajikuta yamekuwa hayo ndiyo maisha yako ya kuacha fursa hii ama ile, kitu ambacho siyo kizuri kwako.
Ili kuweza kufanikiwa zaidi katika maisha yetu tukumbuke kuwa tunatakiwa kuzitumia fursa tunazozipata vizuri bila kuziacha. Hii ikiwa ni pamoja na kutumia muda na siku zetu vizuri ili kutusaidia kufikia kwenye kilele cha kimafanikio. Kwa kufanya hivyo tutakuwa kwenye njia sahihi ya mafanikio.
Kwa makala nyigine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza.
Tunakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio na endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kwa kujifunza na kuhamasika zaidi.
DAIMA TUPO PAMOJA MPAKA MAISHA YAKO YAIMARIKE,
IMANI NGWANGWALU,
0713 048035,