Inawezekana ukawa una malengo na mipango mikubwa ambayo umejiwekea ili kuweza kutimiza ndoto zako. Lakini, kwa bahati mbaya hata uwe na mipango na malengo mazuri vipi hutaweza kuyatimiza hata kidogo kama utakuwa ni mtu wa kutokujali afya yako. Afya ni kila kitu kwako, ndiyo itakayokuwezesha kufikia malengo yako. Kama utakuwa huna kitu hiki, hujali afya yako sana, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako.
Leo katika makala hii tutaangalia zaidi kwa upande wa afya ya binadamu kama inavyomhusu binadamu mwenyewe. Kama ambavyo inavyoweza kumsaidia na kumletea mafanikio makubwa katika maisha yake. Afya kwa maana rahisi na inayoeleweka kwa jamii ni uimara wa kinga ya mwili kwa magonjwa na madhara mengine yoyote kwa mwili.
Unapomwona binadamu kwa mara ya kwanza, unaweza kupata jibu la haraka kama afya yake ni njema au la. Mwonekano wa kwanza kabisa kwa binadamu unatoa picha kamili ya hali ya afya yake. Hii ina maana, kama hali ni nzuri au afya ni njema, basi inaonekana hata nje katika umbo au sura yote ya mhusika kwa kadri atakavyojieleza au kujionyesha.
Afya ya binadamu kwa kawaida huwa imegawanyika katika sehemu mbili muhimu. Sehemu ya kwanza ni mwili unaoonekana halisi ukiwa na viungo vyote vya fahamu. Macho,pua, masikio, ulimi na mikono. Viungo hivyo vitano vinafanya kazi kwa binadamu kama viungo vya ufahamu au wakati mwingine huweza kuitwa milango mitano ya ufahamu.
Sehemu ya pili ya afya binadamu ni akili. Hii ni muhimu sana kwa binadamu ingawaje akili haionekani kwa macho ya binadamu lakini matendo yake, mawazo yake na maneno yake yanatosha kupima uwezo wa akili yake. Akili ndiyo inayotafsiri vitu baada ya kuvipata kupitia katika viungo vya ufahamu.
Hivyo, kama kuna matatizo kwenye viungo vya fahamu itakuwa siyo rahisi kwa akili kutoa majibu sahihi na vilevile kama akili yenyewe haiko sawasawa, basi hata majibu yake yatakuwa siyo sawa. Hivyo basi, binadamu aliyekamilika anatakiwa kuwa na akili timamu nayo iliyokamilika. Panapotakiwa kuonekana furaha au huzuni ni lazima hisia hizi zionekane. Hivyo, zitajitokeza tu kama mhusika ana akili timamu.
Baada ya kutaja hizo sehemu za afya ya binadamu, hebu kidogo tuangalie umuhimu wake. Afya ni muhimu sana kwa kuwa ndiyo inayokupa nafasi katika jamii au familia. Ndiyo inayokufanya uamke kila kukicha na kuendeleza harakati za maisha yako ya kila siku. Kama mwili wako hauna afya, basi hakuna kitu ambacho unaweza kukifanya cha maana kwako.
Afya hii bora itakayoweza kutusaidia kutufikisha kwenye mafanikio tunayoyataka, tutaipata tu kama tutakuwa ni watu wa kula vyakula bora na muhimu kwenye miili yetu, yaani kula kile kinachokupa afya na siyo kula kula tu. Tatizo kubwa kwa jamii yetu ni elimu juu ya tule nini. Tulio wengi ni watu wa kula kwa mazoea ya kila siku asubuhi chai chapati au maandazi basi.
Mtu akipata supu ya kuku, ng’ombe au mbuzi, anajiona ameendelea sana na haduruki hata kumcheka aliyepata supu ya kichwa cha ng’ombe au utumbo wa ng’ombe. Sisemi kwamba eti hivi havifai, lakini msingi ni kujiuliza, je hapa mlo umekamilika au bado?
Kumbuka, kila kitu hapa duniani kina sababu na maana yake ya kufanyika au kuwepo, ni muhumu kwanza kujiuliza kwa nini nakula na nahitaji kula nini kwa muda huu. Swali hili inabidi kujiuliza kabla ya kutayarisha au kutafuta chakula. Kula ni muhimu sana na hivyo basi, inabidi tuwe makini kwenye kula ili kuweza kulinda afya zetu kwa ajili ya mafanikio yetu wenyewe.
Vilevile mwili wa binadamu ili uwe na afya bora unajengwa pia na mazoezi. Ni muhimu kufanya mazoezi mara kwa mara kwa mpangilio maalum kwa ajili ya kujenga mwili. Kuna mazoezi mengi mazuri ambayo ni rahisi kwako kuyafanya kwa kuwa hayahitaji nafasi kubwa sana. Haya huwa unaweza kuyafanyia chumbani kwako au uani.
Kuhusu kuwa na afya nzuri kwa upande wa akili zetu ni muhimu kutafuta chakula cha akili. Akili ni chombo ambacho binadamu anatumia katika maisha yake ya kila siku, kikijengeka vema kinakuwa na manufaa na msaada mkubwa kwa binadamu.
Vipo vitu vingi sana vinavyoweza kuijenga akili ikiwa ni pamoja na vyakula, mazoezi kama nilivyoeleza hapo mapema. Lakini muhimu zaidi ni kusoma vitabu mbalimbali. Kusoma vitabu mbalimbali kunasaidia kuipa changamoto akili kwa kuwa inapata muda wa kutafakari na kufikiria zaidi mawazo yaliyomo kitabuni.
Unapata pia muda wa kulinganisha na kujipima au kupima anachosema mwandishi na hali ambazo akili imeshapitia. Kusoma vitabu mbalimbali kunaipa nafasi akili kuhifadhi mambo mengi kutoka kwa watu mbalimbali na yenyewe inakuwa ni kumbukumbu nyingi sana ikiwa ni pamoja na taarifa mbalimbali kuhusu mambo mbalimbali. Hii ndiyo furaha ya akili. Akili inakuwa inafarijika sana na kujiona bora kwa kufahamu vitu vingi na hapa inasaidia kuijenga na kuipa uwezo wa kutoa majibu sawasawa.
Tatizo hapa ni uvivu wetu wa kusoma vitabu mbalimbali vya maarifa mbalimbali. Sisi watanzania tu wavivu wa kusoma hata magazeti ya maana. Uvivu huu unatufanya tuwe wazito hata kuchangia kuhusu mada mbalimbali zinazotuhusu. Akili zetu zinakuwa zimelala, hazina muda wa kufikiri. Hazitaki usumbufu au hata kujishughulisha kutafuta habari za manufaa. Zinataka habari zenye kutupa ahueni ya muda kwa kutupandisha jazba.
Hii inakuwa ni hatari kwa mtu, jamii au taifa tunapokuwa na taifa au jamii mbovu kutokana na kutokuishughulisha akili kusoma au kupata maarifa mapya ya manufaa. Tunatakiwa kuamka sasa,kuiamsha akili na kuipa chakula chake chenye afya kwa ajili ya faida ya mafanikio yetu. Vinginevyo kama hatutafanya hivyo itakuwa ngumu kwetu kuweza kufanikiwa.
Nakutakia mafanikio mema, endelea kutembelea AMKA MTANZANIA kila siku kupata maarifa bora yatakayokufanya ubadili maisha yako.
Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku, mpaka maisha yako yaimarike.
IMANI NGWANGWALU,
- 0713 048 035,