Tokea mambo ya ujasiriamali yameanza kupamba moto hapa Tanzania, kumekuwa na upotoshwaji mkubwa sana ambao umekuwa unafanyika kwenye elimu ya ujasiriamali. Upotoshwaji huu umekuwa unafanywa na watu kwa kujua au wengine bila ya kujua, ila kwa kuwa unawanufaisha wao hawajali kuhusu wengine.
Kabla hata sijaenda mbali naomba niuseme upotoshaji wenyewe.
Ujasiriamali sio kutengeneza sabuni, wala sio kutengeneza mishumaa au kutengeneza mkaa wa makaratasi. Huu sio ujasiriamali na usikubali kuendelea kudanganywa tena.
Sisemi mafunzo haya ya kutengeneza vitu ni mabaya, hapana, ni mazuri sana. Ila ninachosema ni hiki; ukishajua kutengeneza sabuni haugeuki na kuwa mjasiriamali hapo hapo.
Ujuzi wa kutengeneza vitu mbalimbali mtu yeyote anaweza kujifunza, lakini sio kila anayejifunza anakuwa mjasiriamali, wengi wao wanafanya biashara zao kwa njia ambazo sio za kijasiriamali.
Ujasiriamali ni kabla na baada ya kutengeneza hiyo sabuni, lakini sio wakati unaitengeneza sabuni.
Kwa kukosa elimu sahihi ya ujasiriamali, watu wengi wamejifunza kutengeneza vitu mbalimbali ila hawajui soko liko wapi. Watu wanatengeneza sabuni zao vizuri na kuanza kuzunguka nazo, wanakosa wateja na mwishowe wanakata tamaa.
Leo nataka nikutambulishe kwa ufupi sana maana halisi ya ujasiriamali na elimu sahihi ya ujasiriamali unayotakiwa kuipata.
SOMA; Je Wewe Ni Mjasiriamali Au Mfanyabiashara Mdogo? Soma Hapa Kujua.
Nini maana ya ujasiriamali?
Ujasiriamali unajumuisha ubunifu, kutengeneza kitu kipya na kuwa tayari kukabiliana na ugumu; vilevile kuwa na uwezo wa kupanga na kuendeleza miradi ili kufikia malengo.
Ujasiriamali ni mtazamo katika akili ya mtu katika kutafuta fursa, kuwa tayari kukabiliana na matatizo na kuwa na uwezo wa kutengeneza faida, kwa kuanzisha ama biashara mpya au kuongeza tija katika taasisi.
Ujasiriamali hujumuisha shughuli nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa na wazo, kutengeneza na kuendesha biashara.
Mjasiriamali ni mtu gani?
Mjasiriamali ni mtu anayefikiri kwa ubunifu na uvumbuzi akiwa tayari kukabiliana na hatari inayoweza kusababishwa na fursa zilizopo kwa lengo la kuzalisha faida, ajira na ustawi wa kijamii na kiuchumi.
Wajasiriamali huanzisha kampuni ambazo huwa injini katika ukuaji wa uchumi na utengenezaji wa utajiri. Kompyuta, simu za mkononi, mashine za kufulia, na huduma za usafirishaji ni mifano wa mawazo ya ujasiriamali yaliyobadilishwa kuwa bidhaa au huduma.
Kwa maana hiyo ya ujasiriamali na mjasiriamali tunaona kabisa kutengeneza sabuni ni sehemu ndogo sana ya ujasiriamali, kama hata ipo.
SOMA; Unapokuwa Tayari Kuingia Kwenye Ujasiriamali Fanya Vitu Hivi Vitano.
Elimu sahihi ya Ujasiriamali Unayotakiwa Kuipata.
Wewe kama mjasiriamali au kama ndio unataka kuingia kwenye ujasiriamali unatakiwa kupata elimu sahihi ya ujasiriamali. Elimu unayotakiwa kupata ni elimu ya kukubadili mtazamo, uache kuwa mtu wa kukata tamaa na kuogopa kujaribu na uweze kujaribu mambo mbalimbali. Pia elimu hii inatakiwa kukuandaa wewe uweze kutumia mazingira yako, vipaji vyako na matatizo ya watu wanaokuzunguka kuweza kuja na wazo ambalo litawanufaisha wote.
Kwa mfano kwenye kutengeneza sabuni kama tulivyotaja hapo juu, tumesema ujasiriamali ni kabla ya kutengeneza sabuni na baada ya kutengeneza sabuni.
Kabla ya kutengeneza sabuni kwanza unahitaji kujiuliza je kuna uhitaji wa sabuni? Kama ukitengeneza sabuni yako, nani atainunua? Mtu huyo anapatikana wapi na utamfikiaje? Na je mtu huyu ana uwezo kiasi gani wa kuweza kulipia sabuni unayotaka kuitengeneza? Na je gharama za kumfikia ni kiasi gani? Kwa kifupi unahitaji kuwa na mteja au kuweza kutengeneza mteja utakayeweza kumuuzia bidhaa au huduma unayotoa. Kama hujafikiria mteja wako ni mtu mwenye sifa gani, wewe sio mjasiriamali.
Baada ya kutengeneza sabuni yako pia kuna mambo muhimu ya kufanya. Kwa mfano tayari sabuni unayo ila mteja uliyemlenga hapatikani au hayupo tayari kununua, je unafanya nini? Au unakutana na ushindani mkubwa kwenye soko, au biashara inakuwa ngumu sana kiasi cha wewe kuingia kwenye hasara. Je unabadilishaje hali ya mambo? Hapa ndipo mjasiriamali wa kweli anapojulikana.
SOMA; Weka Pamoja Vitu Hivi Vitatu Na Tayari Wewe Ni Mjasiriamali Mwenye Mafanikio Makubwa.
Kwa kifupi elimu ya ujasiriamali ni elimu endelevu, ni elimu ambayo inatakiwa kufanyika kila siku. Yaani kama unataka kuwa mjasiriamali mwenye mafanikio, hakikisha kila siku unapata nafasi ya kujifunza kitu muhimu. Jifunze kuhusu biashara, kuhusu maisha, kuhusu mafanikio, kuhusu kujiamini, kuhusu ubunifu na mengine mengi.
Uzuri ni kwamba tunaishi kwenye dunia ambayo kujifunza ni rahisi sana. Unaweza kujifunz akw akujisomea vitabu, kusoma mtandao wa intaneti, kuhudhuria semina, kujiandikisha kwenye kozi mbalimbali na hata kujifunza kupitia uzoefu na makosa unayoyafanya.
Moja ya maeneo muhimu ambapo utapata elimu kila siku itakayokubadili mtazamo wako na kukufanya kuwa mjasiriamali bora ni KISIMA CHA MAARIFA. Kwa kujiunga na KISIMA, unakuwa kwenye mazingira ambayo kila siku yanakupatia kitu kipya cha kujifunza kuhusu mafanikio kwenye kile unachofanya na maisha kwa ujumla. Kujiunga na KISIMA CHA MAARIFA bonyeza hayo maandishi.
Nafasi moja ya kukutana na mjasiriamali mwenye changamoto.
Natoa nafasi moja ya kukutana na mjasiriamali mwenye changamoto nyingi sana kwenye kile anachofanya na anaona anaelekea kukata tamaa. Kama unataka nafasi hii andika ujumbe mfupi kwenda 0717396253 kupata maelezo zaidi.
Unapokuwamjasiriamali, elimu yako ndio kwanza imeanza na usifikiri kuna siku utaacha kujifunza. Kama umeamua kweli kuingia kwenye ujasiriamali na unataka ufanikiwe kupitia ujasiriamali basi unahitaji kupata elimu sahihi kila siku ambayo itakufanya uendelee kuwa bora kila siku.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio kupitia ujasiriamali.
TUPO PAMOJA.