Umewahi kuona mtu ambaye analalamikia sana kitu, mfano uongozi au jinsi watu wengine wanavyofanya mambo, halafu mtu huyo anapata nafasi hiyo na anaishia kufanya kile kile alichokuwa analalamikia? Kwa mfano mtu ambaye sio bosi kwenye eneo lake la kazi, analalamika sana jinsi ambavyo bosi anavyoshindwa kufanya mambo yaende vizuri, halafu siku moja na yeye anachaguliwa kuwa bosi na anaishia kufanya yale yale aliyokuwa analalamikia.
Mfano mwingine mzuri ni katika nafasi za uongozi ambapo mtu anaomba kuchaguliwa kwa kusema mabaya ya kiongozi aliyepo. Ila anapopata nafasi ya kuchaguliwa na yeye anaishia kufanya hayo hayo aliyokuwa anayapinga.
Hii ni mifano ambayo ni maarufu sana katika jamii zetu.
Je unajua ni nini kinasababisha hali hii kutokea kwa watu wengi?
Sababu moja kubwa inayosababisha hali hii kutokea ni wayu kukosa misingi yao ya kimaisha. Mtu anakuwa hana kanuni ambazo anazisimamia kwenye maisha yake, na hivyo mazingira yanapomsukuma kufanya kitu anashindwa kuyazuia.
SOMA; Yako Wapi Yale Maisha? Ni Wakati Wa Kulipa Deni Sasa.
Je wewe ni misingi gani ambayo umejiwekea kwenye maisha yako? Ni kanuni gani ambazo umeamua kuishi nazo kwenye maisha yako na hutozivunja hata kutokee nini?
Kama huna misingi au kanuni unazozisimamia kwenye maisha yako, ni rahisi sana kufanya jambo lolote pale mazingira yanapokusukuma kufanya.
Leo hapa utajifunza jinsi ya kujiwekea kanuni utakazozisimamia maisha yako yote na hivyo kuwa na maisha ambayo unayafurahia.
Kwa nini ni muhimu sana kuwa na misingi kwenye maisha yako?
Kuna kauli inasema kwamba kama hutasimama kwa chochote basi utaanguka kwa chochote. Hii ni kweli kabisa, katika dunia ya sasa kuna vitu vingi sana ambavyo viko tayari kukuangusha. Kama hakuna ambavyo umechagua kuvisimamia utajikuta unaanguka kwenye kila jambo unalojaribu kufanya.
Sababu nyingine muhimu ya kujijengea misingi kwenye maisha ni wingi wa fursa zilizopo kwenye dunia ya sasa. Kuna vitu vingi sana ambavyo unashawishika kufanya, lakini kwa uwezo na muda huwezi kufanya vyote. Kusema ujaribu kila kitu utaishia kushindwa hivyo ni muhimu kuwa na kanuni ambazo zitakuongoza katika kufanya maamuzi ni kitu gani ufanye na kipi usifanye.
SOMA; UKURASA WA 18; Hakuna Anayejali Maisha Yako Zaidi Yako Mwenyewe.
Jitengenezee mwongozo wako mwenyewe.
Kwa kuwa maisha ya kila mtu ni tofauti na kwa kuwa kila mtu ana vipaumbele vyake kwenye maisha, kanuni za maisha haziwezi kuwa sawa. Kila mmoja atakuwa na kanuni zake ambazo atajiwekea katika maisha yake ambazo atachagua kuishi nazo.
Tumia nafasi hii leo kuandika kanuni kumi ambazo utaishi nazo kwenye maisha yako. Kanuni hizi kumi zitakuwa ndio amri zako kumi kwenye maisha yako yote. Kabla hujasema jambo lolote, kabla hujafanya jambo lolote, utaangalia kwanza kama linaendana na kanuni zako ulizojiwekea
Hapa nitakushirikisha baadhi ya kanuni ambazo unaweza kuzijumuisha kwenye kanuni zako kumi.
1. Kazi ndio msingi wa maendeleo.
Unajua hili, na unashangaa kwa nini nianze na kitu rahisi hivi ambacho kila mtu anajua na anafanya? Ndio kila mtu anajua kazi ndio msingi wa maendeleo, lakini ni wachache sana ambao wamejiwekea kanuni ya kufanya kazi. Nenda kwenye ofisi nyingi na utakuta wafanyakazi wakitafuta kila mbinu itakayowafanya wasifanye kazi. Nenda kwenye biashara mbalimbali na utapata huduma mbovu sana mpaka kufikiri ulikwenda kuomba.
Halafu, watu wanaofikiria kupata fedha kwa kucheza kamari, maarufu kama betting nao wanafikiri kazi ni msingi wa maendeleo? Na wanaocheza bahati na sibu wakiamini kwamba watashinda zawadi na maisha yao yatakuwa bora bado unafikiri wanaona kazi ndio msingi wa maendeleo?
Ukishaweka kanuni kwenye maisha yako kwamba kufanya kazi ndio msingi wa maendeleo yako, hutatafuta tena njia nyingine ya mkato ya kufikia mafanikio. Na hii itakuepusha wewe kutapeliwa au kupotezewa muda. Hakuna njia rahisi, ukishawishika tu hivyo, utatapeliwa, au utaingia kwenye wizi, ufisadi au kufanya uhalifu.
SOMA; Haya Ni Maajabu Ya Dunia Ambayo Unayafanya Kila Siku.
2. Uminifu ni mtaji tosha wa kufikia mafanikio.
Uminifu, neno rahisi kusema lakini utekelezaji wake ni mgumu sana. Ni kweli kwamba uaminifu ni mtaji wa wewe kufikia mafanikio, kadiri watu wengi wanavyokuamini ndivyo utakavyopata fursa nyingi zaidi. Lakini je ni wangapi ambao ni waaminifu? Ni wafanyakazi wangapi ambao wapo tayari kuwa wakweli kwa watu wanaowahudumia na hata waajiri wao? Ni wafanyabiashara wangapi ambao wapo tayari kusema ukweli kwa wateja wao, kuwatoza gharama halali na hata kuwapa ushauri ambao utawasaidia?
Kama unasema kuwa mwaminifu huwezi kupata mafanikio, hiyo ndio sababu kwa nini hutafikia mafanikio makubwa.
Weka uaminifu kama kanuni muhimu kwenye maisha yako. Na ukishaamua kuwa mwaminifu maana yake husemi tena uongo, huibi, hushiriki majungu na hata kuchepuka unaacha. Ukishaamua kuwa mwaminifu, unahitaji kufanya hivyo kwenye maeneo yote ya maisha yako, ukivunja eneo moja, utavunja kila kitu.
3. Jifunze kitu kipya kila siku.
Huu ni msingi muhimu sana wa kujijengea kwenye maisha yako, hasa wakati huu ambapo mambo yanabadilika kwa kasi sana. Kama hujifunzi maana yake unaachwa nyuma, kwa sababu biashara inayoleta faida leo, miaka michache ijayo inaweza isiwepo kabisa, kazi unayofanya leo inaweza kutoweka kabisa miaka ijayo. Ukitaka usiachwe nyuma, fanya kujifunza kila siku sehemu ya maisha yako.
Kuna fursa nyingi sana za kuweza kujifunza kila siku, jisomee vitabu, jiunge na kozi mbalimbali, hudhuria semina mbalimbali. Kila fursa ya kujifunza inapojitokeza itumie vizuri, itakulipa vizuri sana baadae.
SOMA; Kauli KUMI Za Marcus Aurelius Zitakazokufanya Uyaone Maisha Kwa Utofauti.
4. Tafuta jambo la kushukuru kila siku.
Unafikiri maisha yako ni magumu sana ya hovyo sana na huna cha kufurahia au cha kushukuru? Unakosea sana kwa kuyafanya maisha yako hivyo na ndio maana utaendelea kupata unachopata sasa. Kama unalalamika maisha yako ni mabaya kwa sababu huna viatu vizuri, mwangalie mtu ambaye hana miguu kabisa, je ni nani wa kulalamika na nani wa kushukuru?
Moja ya misingi muhimu unayotakiwa kujijengea ni kutafuta jambo la kushukuru kila siku kwenye maisha yako. Hata kama maisha yako ni magumu kiasi gani, hata kama unapitia changamoto nyingi kiasi gani, kuna jambo la kushukuru. Kwanza kitendo cha kuwa hai tu mpaka leo ni jambo kubwa sana la kushukuru, kuna watu wengi ambao wangekuwa tayari kulipa fedha nyingi sana ili wawe hai lakini haikuwezekana. Jambo jingine muhimu la kushukuru ni kuwa na watu ambao wanakupenda wewe kama wewe, pamoja na kujua mapungufu yako yote, pamoja na kujua matatizo unayosababisha lakini bado wanakupenda, watu hawa ni marafiki zako na familia yako.
Shukuru kwa kuishi kwenye dunia ambayo ni rahisi kutumia fursa zinazopatikana. Shukuru kw akuishi kwenye nchi ambayo kuna amani, na unaweza kuendesha kazi au biashara zako bila ya kuwa na hofu kubwa na usalama wa maisha yako. Kwa kuwa na mtazamo huu kila siku, utaona maisha yako ni bora sana.
5. Ishi leo.
Huu ni msingi muhimu sana kujijengea. Kwa sababu hapo ulipo unaishai jana na unaishi kesho na kwa kufanya hivi unapoteza fursa nzuri ya kuishi leo, ya kufurahia muda huu ulinao sasa, ambao ndio muda pekee unaoweza kuwa na uhakika nao.
Acha kuishi jana, imeshapita na haitarudi tena. Kama kuna jambo ulikosea, kulifikiria kila mara halitabadilika. Jifunze ni kipi ulikosea na amua kutorudia tena makosa uliyofanya, baada ya hapo achana na jana.
Acha kuishi kesho, bado haijafika. Haijalishi una hofu kiasi gani kuhusu kesho yako, hakuna kiwango cha hofu kinachoweza kuibadili. Jiandae vizuri kwa ajili ya kesho yako lakini isikufanye ushindwe kuishi na kufurahia leo.
Ishi leo, fanya kile unachofanya leo kama ndio kitu cha mwisho kufanya kwenye maisha yako. Ishi siku ya leo kama ndio siku ya mwisho kwenye maisha yako na itakuwa siku ya furaha sana kwako. Na ishi hivi kila siku, na maisha yako yatakuwa bora kila siku.
SOMA; Maisha Sio Rahisi Lakini Ni Mazuri Kama Hivi...
Ningependa kwenda mpaka msingi wa kumi, ila anza na hii mitano na jiongezee mitano mingine halafu zifanye hizo ndio amri zako utakazoishi nazo kila siku.
Ukishaongeza na kufika kumi tafadhali nishirikishe kwa kuniandikia email kwenye makirita@kisimachamaarifa.co.tz kwa kufanya hivyo utakuwa umejiwekea nafasi kubwa ya kuweza kufuata misingi yako hiyo.
Kumbuka maisha ni kuchagua, unaweza kuchagua kujiwekea misingi ambayo utaishi nayo na kufanya maisha yako kuwa bora kila siku. Au pia unaweza kuchagua kutokujiwekea misingi yoyote na kuishi kama bendera inavyofata upepo, ukiambia hiki ni bora unakifanya na ukipata hasara unaugulia mwenyewe.
Nakusihi sana leo ufanye maamuzi ambayo yatabadili na kuboresha maisha yako.
TUPO PAMOJA.