Mpenzi msomaji wa AMKA MTANZANIA nakukaribisha tena kwenye kipengele hiki cha ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio. Maisha yetu yamejaa changamoto nyingi na unapokuwa kati kati ya changamoto ni vigumu sana kuona njia sahihi. Hii ni kwa sababu matatizo yanakuwa yamekusonga sana na huwezi kufikiria kwa makini huku ukiwa umeyaweka matatizo hayo pembeni kwa muda.
Ndio maana tuliona umuhimu huu wa kuwa na kipengele cha ushauri kwa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio. Hivyo kama na wewe unachangamoto yoyote inayokusumbua unaweza kuitoa kwa kujaza fomu kwa link itakayotolewa mwisho.
Leo tutajadili changamoto ya kipato. Hii ni changamoto inayowakabili watu wengi sana, hasa katika zama hizi ambazo ajira zimekuwa na matatizo mengi. Kipato cha mshahara kimekuwa ni tatizo sana, karibu kila mfanyakazi mshahara anaopata haumtoshi, hii inatokana na gharama za maisha kwenda juu kwa kasi huku mshahara kuenda juu taratibu sana.
Pia watu wengi sana wanaanza kazi kwa mshahara ambao ni kidogo sana. Leo hii kuna wahitimu wa vyuo vikuu wengi ambao wanalipwa mshahara mdogo sana ukilinganisha na viwango vyao vya elimu.
Swali ni je unawezaje kutoka kimaisha kwa kuanza kazi ambayo ina mashahara kidogo?
Kabla hatujaangalia unachoweza kufanya, tuone maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu changamoto hii.
nimepata kazi lakini mshahara naotakiwa kulipwa ni 250000 kwa mwezi je mshahara huu unaweza kunipa maendeleo ikiwemo kujenga nyumba na hata kununua gari?.naombeni mchango wenu wa mawazo tafadhali.
Najua hali hii inawatokea wengi, sasa swali la msingi kabisa kabla hatujaangalia ni nini cha kufanya ni je inawezekana kutoka kimaisah kwa kuanzia na mshahara kidogo? Jibu ni ndio inawezekana.
Baada ya kukubali kwamba inawezekana, (yaani kubali wewe kwamba inawezekana ili haya yanayofuata hapa chini yawe na maana kwako) sasa tuangalie ni jinsi gani ambavyo unaweza kutoka kimaisha kwa mshahara kidogo.
Hatua ya kwanza; Weka malengo ya maisha yako.
Hatua ya kwanza na ya muhimu kabisa ni kuweka malengo na mipango ya maisha yako. Kumbuka kwamba kazi hii yenye mshahara kidogo sio mwisho wa maisha yako, bali ni hatua tu unayopitia kufikia ndoto zako kwenye maisha. Hivyo weka malengo ya kazi au biashara gani utataka kufanya baadae, malengo ya maisha yako na kila eneo muhimu kwenye maisha yako. Kujua jinsi unavyoweza kuweka malengo ambayo utayafikia bonyeza maandishi haya na usome makala za malengo.
Hatua ya pili; Kubali kwamba kipato chako ni kidogo na anza kwakuishi maisha hayo.
Hatua ya pili na muhimu sana kwako ni kukubali kwamba kwa sasa unapata kipato kidogo na ukishakubali kipato hiko kubali kuishi maisha yanayoendana na kipato hiko kwa siku hizi za mwanzoni. Usitake kuanz akujionesha na wewe upo, uanze kumiliki siku za bei kali, kuhudhuria sehemu za gharama na vitu kama hivyo. Haya yote yatakuja baadae ukishaweka sawa kipato chako, ila mwanzo huu unahitaji kujibana ili kujenga msingi wako wa kipato. Ishi kwa kwa kupata huduma zile za msingi kabisa, kitu chochote ambacho usipokuwa nacho hutakufa, au maisha yako hayatakuwa hovyo sana, basi kwa sasa usiwe nacho. Dhibiti matumizi yako kwa kiasi kikubwa sana ili uweze kujipanga vizuri kwa ajili ya baadae.
SOMA; Huu Ndio Ushauri Muhimu Sana Wa Kuishi Nao Kila Siku Kwenye Maisha Yako.
Hatua ya tatu; Anza kuweka akiba kwenye mshahara wako wa kwanza.
Baada ya kudhibiti matumizi yako kwa kiasi kikubwa sana anza kuweka akiba haraka sana, usisubiri chochote, hakuna mabadiliko makubwa yatakayotokea hapo ulipo. Anza kwa kuweka akiba asilimia 20 ya kipato chako, ila nakusisitiza weka zaidi ya hapo. Na katika hatua hii ya kuweka akiba, weka akiba kwanz andio ufanye matumizi, na sio kufanya matumizi halafu ndio uweke akiba. Weka akiba huku ukiangalia malengo uliyojiwekea ili ujue kama utawez akuyafikia.
SOMA; Hivi ndivyo unavyoweza kutajirika kwa kuanza na shilingi elfu moja
Hatua ya nne; Angalia fursa nyingine zinazopatikana kwenye kazi yako na hata kwenye maisha yako.
Kazi yoyote, namaanisha kazi yoyote ile ina fursa nyingi ambazo huwa hazionekani kwa wote. Bali wale wenye kiu kali ya mafanikio ndio huona fursa hizi na kuzitumia vizuri. Angalia ni jinsi gani unaweza kutumia nafasi zinazopatikana kwenye kazi yako kuongez akipato zaidi. Angalia ni changamoto gani ambazo watu wanapitia kwenye kazi hiyo na jinsi gani unaweza kusaidia kuzitatua na kujiongezea kipato. Usikae tu kwenye kazi hiyo na kuidharau kwa sababu inakulipa kidogo. Ifuatilie vizuri kazi hiyo, angalia kila fursa unayoweza kuiibua na kuitumia vizuri. Pia kuwa na moyo wa kufanya majukumu ya ziada, maliza kazi zako mapema na chukua majukumu mengine yatakayokuwa yanapatikana, hii itakufanya uongeze thamani yako na hata kuongez akipato chako.
Pia angalia fursa nyingine za kazi au biashara nje ya kazi yako hiyo. Kwa kazi yenye mshahara kidogo mara nyingi huwa haikubani sana hivyo hata kama unafanya kazi masaa kumi kwa siku bado una masaa mengine kumi na nne, ukitoa hapo masaa sita ya kulala unaweza kupata muda wa kujishughulisha na biashara nyingine. Kumbuka wewe sasa hivi upo kwenye wakati mgumu kutokana na kipato chako, sasa kama unataka utoke kazini uende ukapige story au kuangalia tv au kufanya chochote kwa madai kwamba unajipumzisha utaendelea kubaki hapo ulipo. Jitoe kwa muda huu kufanya kazi sana na kuangalia kila fursa itakayojitokeza mbele yako.
SOMA; Kitu Hiki Kimoja Ni Lazima Kitokee Kwenye Maisha Yako, Japo Hukipendi.
Hatua ya tano; Jifunze kila siku.
Moja ya sababu zinazowafanya watu kufia kwenye kazi zenye mishahara midogo ni kuridhika na mishahara hiyo kiakili na uvivu wa kujifunza. Sasa ndigu yangu wewe huna anasa hiyo. Tumia kila muda ulionao kujifunza, jifunze ujuzi wa ziada, jifunze kuhusu biashara, jifunze kuhusu maendeleao binafsi. Katika kazi yako angalia ni eneo gani ambalo lina mahitaji ya wafanyakazi ila bado halijapata wafanyakazi wa zuri. Anza kujifunza kitu hiko, soma vitabu vinavyohusiana na eneo hili, angalia video kwenye mtandao zinazoelekeza kuhusiana na kazi hiyo. Tembelea mitandao mbali mbali na pia ongea na watu waliobobea kwenye eneo hilo. Ukishaanza kupata mwanga omba kujitolea kusaidia kazi kwenye eneo hilo, hata ukinyimwa endelea kuomba na shawishi kwamba una kitu unaweza kuchangia. Ukipewa nafasi onesha sasa uwezo wako mkubwa, fanya ka viwango vizuri sana. Kama ukiwez akufanya hivi nakuhakikishia kwamba hakuna mtu atakayekubali kukupoteza na thamani yako itakua kwa kasi sana.
SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.
Hizi ndio hatua tano ninazokushauri uanze kuzifuata leo ili kuweza kutoka kimaisha kwa kuanzia na mshahara kidogo. Kumbuka kila mtu analipwa kulingana na thamani anayopeleka sokoni. Hivyo kama ukiweza kumpatia mwajiri wako thamani kubwa hatakuwa na budi bali kuhakikisha hakupoteze na hapo thamani yako itakuw akubwa sana. Mambo yote haya yatachukua muda kidogo, ila usikate tamaa na endeleza juhudi.
Pia nikupe angalizo kwamba wale utakaowakuta kazini ambao wanajiita waozefu watakukatisha sana tamaa utakapoanza kufuata ushauri huu. Watakuambia sisi tumefanya kazi hii miaka kumi, unajisumbua tu bwana mdogo/bibi mdogo. Ushauri kwa watu hao, wapuuze haraka sana, sio mfano mzuri kwako kuwaiga kwa sababu kama wamefanya kazi miaka kumi na bado mshahara wao ni wa chini sana ni kipi unaweza kujifunza kwao, usiwasikilize.
Nakutakia kila la kheri katika kuboresha kazi yako na maisha yako.
TUPO PAMOJA.
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu. Kama unahitaji ushauri wa haraka wasiliana na mimi kwa email makirita@kisimachamaarifa.co.tz au simu 0717396253/0755953887.
Kabla ya kutoa changamoto yako pitia changamoto ambazo tayari zimejadiliwa ili usirudie ambayo imeshajadiliwa. Bonyeza hapa kusoma changamoto zilizojadiliwa.