Kila mmoja wetu anapenda kufikia mafanikio makubwa sana kwenye maisha yake. Pamoja na hili kuwa hitaji la kila mtu bado ni watu wachache sana duniani ambao wanafikia mafanikio makubwa sana. Na mafanikio makubwa ninayozungumzia hapa ni yale ya viwango vya kimataifa.
Duniani tumeona baadhi ya wachezaji, wasanii, wafanyabiashara na hata wataalamu ambao wamefikia mafanikio makubwa sana kwenye kile wanachokifanya.
Je ni kitu gani kimewawezesha watu hawa wachache kupata mafanikio makubwa sana? Watu kama Bill Gates, Steve Jobs, Leonell Mess, Pelle, Michael Jackson na hata wengine wengi ni mifano ya watu ambao wamefikia mafanikio makubwa sana kwenye kile wanachofanya.
Je watu hawa wamefikia mafanikio hayo makubwa kwa sababu walizaliwa na vipaji vya juu sana? Bila shaka ni hapana, kuna watu wengi sana ambao wamezaliwa na vipaji vizuri ila hawajaweza kufikia mafanikio makubwa.
Je walizaliwa kwenye nchi moja ambayo ni tajiri sana. Bila shaka jibu ni hapana kwa sababu wote hao na wengine wengi wametoka nchi mbalimbali na nyingine sio tajiri.
Je walizaliwa kwenye familia tajiri? Bila shaka jibu ni hapana kwa sababu wengi waliofikia mafanikio makubwa walitoka katika familia masikini.
Je ni kitu gani kimewawezesha watu hawa kufikia viwango vya kimataifa? (WORLD CLASS PERFORMANCE).
Tafiti nyingi zilizofanywa zinaonesha kitu kimoja ambacho kila mtu aliefikia mafanikio kwa kiwango kikubwa anacho. Tafiti hizi zimekusanya watu wote ambao wamewahi kufikia mafanikio makubwa na kuangalia maisha yao na kile wanachokifanya na wote walikuwa na kitu kimoja katika utendaji wa shughuli zao.
Kitu hiko kimoja ni muda. Tafiti zinaonesha wengi waliofikia mafanikio makubwa walikuwa wakifanya kitu hiko sio chini ya miaka kumi. Utafiti uliofanywa kwa kuangalia washindi wa tuzo za Nobel wengi wao walipata tuzo hizo wakiwa na miaka kati ya 36 na 42. Hii inaonesha kwamba kama mtu ameanza kufanya kazi akiwa na miaka 25, ambapo wengi ndio wanaanza kazi basi miaka kumi baadae akiwa na zaidi ya miaka 35 anaweza kuwa amefikia ugunduzi mkubwa ambao unampatia tuzo ya NOBEL. Chini ya miaka hiyo ni wachache sana na zaidi ya miaka hiyo ni wachache pia.
MASAA ELFU KUMI(10,000)
Katika kitabu cha Outliers, Malcom Gladwell ameelezea dhana ya masaa elfu kumi. Anasema kwamba itakuchukua masaa elfu kumi ya kukifanya kitu ndio uweze kufikia kiwango cha kimataifa.Ni muda mrefu eh?
Hesabu hizi za Gladwell hazipo mbali sana na dhana ya miaka kumi, kwa sababu kama tukichukua masaa elfu kumi tukagawa kwa miaka kumi tunapata masaa elfu moja kwa mwaka. Na tukichukua masaa elfu moja kwa mwaka tukagawa kwa siku 365 tunapata masaa matatu kwa siku.
Hivyo unahitaji masaa matatu kila siku ya kufanya kitu unachotaka kubobea ndio uweze kufikia kiwango cha kimataifa. Ukiweza kufanya masaa mengi zaidi ya hayo kwa siku itakuchukua miaka kichache zaidi.
Hii iko sahihi kabisa, ulizia mchezaji yeyote mwenye mafanikio makubwa utaambiwa anafanya mazoezi kila siku na kwa muda mrefu. Ulizia wanamuziki wenye mafanikio makubwa utaambiwa wanaimba na kufanya mazoezi kila siku. Ulizia wanasayansi waliofanya ugunduzi mkubwa utaambiwa wanatumia muda mwingi kwenye maabara kufikiria, kusoma na kujaribu vitu vipya kila siku. Ulizia wafanyabiashara wenye mafanikio makubwa, utaambiwa wanajifunza na kufanya biashara zao kila siku na kwa muda mrefu.
Je na wewe unataka kufikia mafanikio kwa viwango vya kimataifa?
Kwa kuwa hapa kwetu Tanzania hatuna watu ambao wamefikia mafanikio ya viwango vya kimataifa(au tunao wachache sana) nimeanzisha harakati za kufikia viwango vya kimataifa. Hivyo kama na wewe unataka kufikia viwango vya kimataifa karibu kwenye harakati hii.
Unachotakiwa kufanya cha kwanza kabisa chagua kitu kimoja amacho unapenda kufanya. Yaani uko tayari kufanya kitu hiko kila siku bila ya kuchoka hata kama hulipwi chochote. Kama mpaka sasa hujui ni kipi unapenda kufanya soma; jinsi ya kugundua vipaji vyako. Baada ya hapo karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA ambapo tutakuwa tunajifunza jinsi ya kufikia WORLD CLASS kwenye kitu chochote ambacho mtu anafanya.
Jiunge na KISIMA CHA MAARIFA kwa uanachama wa GOLD ambapo tutakuwa tunajadili jinsi ya kufikia viwango vya kimataifa kwenye jambo lolote unalopendelea kufanya. Hakuna linaloshindikana kama ukiwa na nia ya kweli.
Nakutakia kila la kheri katika harakati za kufikia mafanikio makubwa ya viwango vya kimataifa.
TUKO PAMOJA.